Friday, March 7, 2014

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Sadiki, atoa somo Siku ya Wanawake Duniani

*Awataka wakazi wa mabondeni jijini kuhama kuepuka madhara ya mafuriko


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Sadiki, akizungumza na waandishi wa habari, jijini leo, kuhusu, maadhimisho ya Siku ya Wanawake na pia kuwataka wakazi wa mabondeni kuhama ili kuepuka madhara ya mafuriko kwenye maeneo hayo. (Picha na Aron Msigwa–MAELEZO)

Na Aron Msigwa–MAELEZO, Dar es Salaam.
6/3/2014.
ZIKIWA zimebaki siku chache Tanzania iungane na Mataifa mengine kuadhimisha siku ya Wanawake duniani , Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mh. Saidi Meck Sadiki ameeleza kuwa ipo haja ya  jamii, Asasi za kiraia na zile za kidini kushiriki kikanilifu katika  kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake nchini.

Akizungumza na  waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam  maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yatakayofanyika tarehe 8 mwezi huu Mh. Sadiki Meck Sadiki ameeleza  kuwa licha ya mchango mkubwa wanaoutoa katika maendeleo ya taifa wanawake wanakabiliana na changamoto mbalimbali kutoka katika jamii inayowazunguka.

Amesema licha ya wanawake kuwa na jukumu la kutunza familia, kuendesha shughuli za uzalishaji wa bidhaa na huduma mbalimbali kutokana na shughuli za ujasiriamali bado wanakabiliwa na changamoto za maradhi, vifo vitokanavyo na uzazi, kupigwa, kutukanwa, kutelekezwa, kubakwa, kuandamwa na vitendo vya ukeketaji na mauaji ya vikongwa.

Amezitaja changamoto nyingine kuwa ni pamoja na kunyimwa haki ya kumiliki mali, kutoshirikishwa na kutopewa haki sawa katika ngazi za maamuzi na kuongeza kuwa wakati umefika sasa kwa jamii kutambua na kuthamini mchango walio nao kijamii, kisiasa na kiuchumi kwa kuwapa wanawake fursa sawa katika nyanja zote.

 “  Siku ya Wanawake duniani inaongozwa na Kauli mbiu isemayo, Chochea Mabadiliko Kuleta Usawa Kijinsia , ujumbe huu unaelimisha na kuhamasisha jamii, Serikali, Asasi za Kiraia na za Kidini kutambua umuhimu wa kushirikiana wanaume na wanawake katika ngazi zote za maendeleo”  

Ameeleza kuwa jiji la Dar es salaam litaungana na maeneo mengine nchini katika kuiadhimisha siku hiyo muhimu kwa maadhimisho makubwa yatakayofanyika katika uwanja wa Mwembeyanga  katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke huku mgeni rasmi akiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Hawa Ghasia.

Katika hatua nyingine Mh. Meki Sadiki amewataka wakazi wa jiji la Dar es salaam hususan wale wanaoishi katika maeneo hatarishi yanayokumbwa na mafuriko mara kwa mara kutii taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kwa kuondoka katika maeneo hayo kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini ili kuepuka madhara yanayoweza kuepukika.

Akitoa taarifa kuhusu mikakati ya kukabiliana na majanga yanayoweza kutokea wakati wa msimu wa mvua kama ilivyotabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Mh. Meck Sadiki ameeleza kuwa tayari serikali imejipanga chini ya kitengo cha Maafa cha Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuwa na kikosi kazi  kinachohusisha vikosi vya ulinzi na usalama vya majeshi ya Tanzania.

Ameeleza kuwa serikali kwa kuthamini umuhimu wa maisha ya raia wake hasa wale waishio mabondeni imekuwa ikitoa taarifa za kuhama mapema lakini baadhi yao hugoma kuyahama maeno yao na pindi wanapoondolewa kwa nguvu huamua kwenda mahakamani kuishitaki serikali.

“Mara nyingi tumekuwa tukiwataka mara kwa mara wale wote wanaoishi bondeni kuhama sio tu wakati wa msimu wa mvua lakini wenzetu wamekua wakiona suluhisho lao ni kukimbilia mahakamani jambo ambalo linasababisha mahakama kusimamisha zoezi letu kama tunavyojua serikali yetu inaheshimu uhuru wa mahakama”

Kuhusu kesi zilizopelekwa mahakamani kuhusiana na zoezi la kuwaondoa wananchi wanaoishi katika bonde la mto Msimbazi amesema tayari kuna kesi nne  zinazoendelea kushughulikiwa na tayari Manispaa ya Ilala imeshinda kesi moja.

Ametoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari katika kipindi hiki ikiwemo kutoa taarifa za matukio yanayohatarisha maisha na kujenga tabia ya kushirikiana katika kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza  pia kutoa taarifa kwa mamlaka husika pindi wanapoona baadhi ya watu wanajenga katika maeneo yasiyoruhusiwa.

No comments:

Post a Comment