Saturday, April 26, 2014

Katibu wa CHADEMA Jimbo la Mufindi Kusini, Emannuel Ngwalanje , Ahamia CCM

MZIMU wa aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto Kabwe umeelezwa kumkimbiza hadi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Katibu wa Chadema jimbo la Mufindi Kusini, Emannuel Ngwalanje.


Hatua ya Ngwalanje kujitoa Chadema na kujiunga na CCM imeelezwa na baadhi ya wafuasi wa Chadema kuwa ni pigo kubwa kwa chama hicho.



Akizungumzia kujitoa kwa Ngwalanje, mwanachama wa Chadema Michael Ngimbusi alisema; “Ngwalanje alikuwa nguzo kuu ya Chadema wilayani Mufindi, aliogopwa na wana CCM, hiyo ikiwa ni kutokana na uwezo wake mkubwa wa kushawishi na kujenga hoja.



Katika kipindi cha zaidi ya miaka minne ambacho Ngwalanje amekuwa Katibu wa Chadema jimbo la Mufindi Kusini ameweza kushawishi zaidi ya wakazi 600 katika maeneo mbalimbali jimboni humo kujiunga na chama hicho.



Katika mkutano wa mapokezi yake uliofanyika kijijini kwake Kimilinzowo kata ya Itandula alisema; “Kazi ya kuibomoa Chadema haitaishia katika wilaya ya Mufindi pekee, bali nitaiendeleza hadi Jimbo la Iringa Mjini linaloongozwa na Mchungaji Peter Msigwa kupitia Chadema.” Ngwalanje alisema utawala mbovu na matumizi mabaya ya fedha za ruzuku utaisambaratisha Chadema katika kipindi kifupi kijacho.



Alisema chama hicho kinapata fedha nyingi zinazotokana na ruzuku ya serikali na michango ya wanachama, wafuasi na marafiki zake wa ndani na nje ya nchi lakini zimekuwa zikiwanufaisha wachache.



Alisema wakati kundi kubwa la viongozi wa chama hicho likifanya kazi kwa kujitolea, kundi la wachache walioko makao makuu wamekuwa wakitafuna fedha hizo bila woga huku wakiwatishia wanaohoji.



Alisema demokrasia inayohubiriwa kutafutwa na chama hicho nchini ina walakini kwa kuzingatia kwamba ndani ya chama hicho zipo nafasi za uongozi ambazo kwa wengine ni uhaini kuziwania.
Kwa hisani ya Habarileo.
Emmanuel Ngwalanje akitoa yake yaliyokuwa moyoni kwa wananchi kabla ya kujiunga na CCM.


Katibu wa Chadema Jimbo la Mufindi Kusini, Emannuel Ngwalanje akikabidhi vitendea kazi vyake na kadi ya Uanachama wa CHADEMA kwa katibu wa CCM wilaya ya Mufindi Miraji Mtaturu (kushoto ) baada ya kukihama chama hicho na kujiunga na CCM



Aliyekuwa Katibu wa CHADEMA Jimbo la Mufindi Kusini, Emannuel Ngwalanje akipewa vitendea kazi vya CCM na kadi ya Uanachama baada ya kujiunga na chama chenye umoja na mshikamano, CCM.

No comments:

Post a Comment