Monday, April 21, 2014

Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu Dar es Salaam watoa Tamko la kulaani vurugu zinazojitokeza katika Bunge Maalum la Katiba


Mwanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Gulatone Masiga akifafanua jambo kwa waandishi wa Habari (hawapo pichani). Kushoto ni Asbert Sweya kutoka Chuo Kikuu cha Kampala, wakati wa mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) leo jijini Dar es Salaam. (Picha zote na Idlkara ya Habari, Maelezo)
Mwanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Gulatone Masiga akifafanua jambo kwa waandishi wa Habari (hawapo pichani). Kushoto ni Asbert Sweya kutoka Chuo Kikuu cha Kampala, wakati wa mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) leo jijini Dar es Salaam.

TAMKO LA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU
SISI wanafunzi  wasomi katika Vyuo Vikuu mbalimbali vilivyoko Dar es Salaam (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM); Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU); Dar es Salaam University College of Education (DUCE); USTAWI WA JAMII; Chuo Kikuu cha Mtakatifu John (St. John); Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM); Open University of Tanzania (OUT); Kampala International University (KIU); Dar es Salaam Institute of Technology (DIT); Institute of Adult Education (IAE); Tanzania School of Journalism (TSJ); College of Business Education (CBE) na Chuo cha kumbukumbu ya Mwl JK Nyerere. Sisi sote  tunalaani mwenendo uliyojengeka kwa wanasiasa wanaojiita “UKAWA“ kuvuruga Bunge Maalum la Katiba kwa sababu ambazo si za msingi. Kwanza walianza kudhalilisha wanazuoni wanaoonekana kutofautiana nao kimawazo kuhusu msimamo wao wa kutaka serikali tatu. Wanazuoni ambao wamekuwa wakidhalilishwa na kutungiwa uongo ni pamoja na Profesa Issa Shivji, Profesa Teddy Malyamkono, Profesa Nehemia Osoro, Dk. Francis Michael, na Dk. Kitila Mkumbo. Tungependa kuwataarifu  kuwa wanataaluma wana uhuru wa kutoa mawazo yaani academic freedom na kamwe hawawezi kukaa kimya wanapoona kuna jambo linaloweza kuifanya  nchi ikaangamia na kusambaratika. Wanazuoni  huamini katika “no research,  no data, no right to speak” kwani data zao za kiuchumi, kihistoria, kisiasa na kidiplomasia zinakataa muundo wa serikali tatu. Hoja ya kimsingi ni kuwa “UKAWA”imeanza juzi, je tafiti (research) wamezifanya lini za kuzipa nguvu hoja zao za kutaka serikali 3?
Tatizo lingine tunaloliona kwa “UKAWA” ni kujaribu kuwadhalilisha waasisi wa taifa letu hasa Mwl JK Nyerere na Sheikh Abeid Aman Karume. Je tusipomuamini Mwl Nyerere na Sheikh Karume tumuamini nani kati ya hawa ambao hatuna ushahidi wa uzalendo wao? kwani wapo wanasiasa ya aina yao ambao wametumika na mataifa ya kibeberu kuvuruga nchi zao na mpaka leo wananchi wao wanataabika mfano hai ni Misri, Tunisia, Morocco, Sudan Kusini, Somalia, Libya, Mali Na Afrika ya Kati.Heshima walionayo  waasisi wetu Mwl Nyerere na Sheikh Karume ndani na nje ya Tanzania, sio ya kupuuzwa wala kufananishwa hata kidogo na yeyote yule miongoni mwa waliounda “UKAWA” zaidi ya kutumika kama mfano na kielelezo. Tunawashangaa baadhi ya wanasiasa wa “UKAWA” kuwakejeli waasisi wa taifa letu. Wanasiasa hawa ni Makamu wa kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Profesa Ibrahim Haruna Lipumba, Mh. Tundu Lissu na Halima Mdee kwani wamesoma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilichoasisiwa na waasisi wakuu wa taifa letu, Mwl JK Nyerere na Sheikh Karume. Hata wale wanasiasa wengine ambao hawakupata bahati ya kusoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wamesoma kwenye shule za awali na vyuo vya elimu ya juu ambavyo vina msingi wa utawala bora wa waasisi hawa wakuu wa taifa letu. Hivyo tunaona sio busara hata kidogo kukejeli mchango wao katika harakati za kuliendeleza taifa letu. Tunapenda kuwathibitishia watanzaia kuwa mawazo ya waasisi wa taifa letu hajachakaa na walahayapitwa na wakati hata mara moja.
Sisi kwa mtazamo wetu kama vijana wasomi wazalendo wa vyuo vya elimu ya juu tunashauri yafuatayo;
  • Katiba bora haiwezi kupatikana kwa kususia vikao halali vya bunge maalum la katiba na maandamano, hivyo tunawasihi warejee bungeni ili waendelee na mchakato kutengeneza katiba. Hatua hii ya kurejea bungeni ikishindikana, warejeshe posho za vikao ambavyo hawajahudhuria.
  • Kutofautiana kimawazo kwa njia ya kujenga hoja ndio demokrasia pevu yenye dhana ya “wachache wasikilizwe na wengi wapewe” ambayo ni moja ya misingi mikuu ya demokrasia itakayotupatia “Katiba Bora” ya sasa na vizazi vijavyo.
  •  Lazima wafahamu kuwa maridhiano ndio njia pekee ya kupata “Katiba Bora” yenye kuleta “Elimu Bora”; “Kilimo Bora”; “Afya Bora”; “Uchumi Bora” na “Utawala Bora” kwa maisha bora ya mtanzania na pia kuifanya Tanzania kuendelea kuwa kisiwa cha amani na utulivu ili kupigiwa mfano na kuwa kimbilio la waafrika wenzetu wengi wanaotaabika kwa kuzikimbia nchi zao kwa machafuko yanachochewa na mabeberu wa siasa na uchumi duniani. 
  • Tunawasihi wenzetu wazingatie umuhimu wa kulinda, kudumisha, kustawisha na kuiendeleza amani katika kipindi cha kutengeneza katiba na baada ya mchakato. Tusipojiangalia tutakuwa kama wenzetu Misri, Tunisia, Morocco, Sudan Kusini, Somalia, Libya, Mali na Afrika ya Kati. Tunaamini kwa kuangalia hali za kisiasa za nchi nyingi za Afrika tunaamini kuwa siasa ya Tanzania ni safi na hakuna haja ya kuhamasisha chuki, uzandiki, uzushi, uongo maandamano na uasi ambao ni sumu kali ya umoja (muungano), amani na uhai wa taifa letu tukufu la Tanzania.
  • Watanzania na wanasiasa wafahamu kwamba mataifa kama Marekani na Uingereza yametawala dunia kwa sababu ya umoja wao. Tunaomba tujifunze kwa yaliyotokea Urusi, leo hii imeona umuhimu wa kuzirudisha nchi ambazo zilisambaratika kutoka kwenye serikali ya umoja wa nchi za kijamaa za kisovieti (USSR). Sisi vijana wa kizazi kipya tunawashauri wenzetu waulinde muungano kwa gharama yeyote na muungano huwa haupitwi na wakati. Tunajiuliza kwa wenzetu wa Ulaya na Marekani ambayo miungano yao imedumu kwa karne zaidi ya tano na sita. Je huko hakuna vijana wa vizazi vipya? Sisi tunaona kuwa wanaodai Utanganyika na Uzanzibari ni wakabila na wabaguzi wanaotaka kuturudisha enzi za ukoloni.
  • Tunamuomba Mwenyekiti wa Bunge Maalum azingatie kwamba Bunge Maalum la Katiba si la “UKAWA” ni la watanzania. Hivyo basi liendelee kwa kasi na ufanisi zaidi na lisiyumbishwe na hasira za wachache wanaojiita “UKAWA” kutokana na ukweli kwamba gharama, muda na nguvu  kubwa vimetumika mpaka sasa. Tunaomba bunge liendelee ili kuwapatia watanzania katiba iliyo bora.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika
Imetolewa na Gulatone Masiga, Mwanafunzi UDSM

Kwa niaba vijana wazalendo wa Vyuo vya elimu ya juu Dar es Salaam

No comments:

Post a Comment