Thursday, April 10, 2014

Serikali yajipanga kupunguza tatizo la ajali nchini


Kamanda wa Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani DCP Mohammed Mpinga akiongea na waandishi wa Habari (hawapo pichani), mikakati ya kupunguza ajali za Barabarani ikiwemo kuongeza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kuendelea kununua vifaa vya kisasa vitakavyosaidia kupunguza tatizo la ajali nchini, wakati wa mkutano uliofanyika leo, jijini Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani DCP Mohammed Mpinga akiwaonesha waandishi wa Habari (hawapo pichani), vipima mwendo vya magari. Kushoto ni Kipima mwendo cha kisasa kinachotumiwa na jeshi hilo na kulia ni kipima mwendo cha zamani, wakati wa mkutano uliofanyika leo, jijini Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani DCP Mohammed Mpinga akiwaonyesha waandishi wa Habari (hawapo pichani), kitabu cha mwongozo cha askari kwa usalama barabara juu ya yale wanayopaswa kufanya na yale wanayokatazwa wawapo kazini, wakati wa mkutano uliofanyika leo, jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya waandishi wa habari, wakiangalia Kipima mwendo cha kisasa kinachotumiwa na askari wa usalama barabarani, wakati wa mkutano, uliofanyika leo, jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya waandishi wa habari waliohudhuria mkutano mkutano wa kikosi cha usalama barabarani, wakati wa mkutano uliofanyika leo, jijini Dar es Salaam. (Picha zote na Hassan Silayo)

Na Frank Mvungi
SERIKALI imejipanga kuondoa ajali za barabarani hapa nchini kwa kushirikiana  na wananchi.

Hayo yamesemwa na Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani  Mohamed Mpinga wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.

Akieleza kamanda Mpinga amesema kwa sasa kikosi cha usalama barabarani kinashirikiana na vituo vya redio vipatavyo 70 vilivyopo takribani katika mikoa yote hapa nchini.

Akifafanua alisema kikosi chake kimekuwa kikiendesha vipindi vya Televisheni na pia kuendelea kutoa elimu mashuleni ili kuwajengea wananchi uelewa kuhusu sheria za barabarani.

Kamanda Mpinga alisema mchakato wa kuanza kuweka nukta kwenye leseni (point system) kwa madereva watakaovunja sheria za usalama barabarani upo katika hatua za mwisho na tayari umeridhiwa na Wizara ya Katiba na Sheria.

Pia Kikosi cha Usalama barabarani kimeongeza matumizi ya Tehama kudhibiti ulevi na mwendokasi ikiwa ni sambamba na kuhifadhi takwimu za matukio ya uvunjaji wa sheria kwa njia ya kielektroniki.alisema Kamanda  Mpinga.

Kamanda Mpinga alisema Kikosi chake kimekwishatoa mwongozo wa utendaji utakaotumika na askari wa Kikosi cha usalama barabarani ukiwa na lengo la kuweka kiwango cha utendaji kinachofanana na chenye tija.

Kamanda mpinga alibainisha kuwa Kikosi chake kimekuwa kikitoa elimu kwa madereva wa Bodaboda kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama vile chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ambapo waendesha bodaboda 4000 wameshapatiwa mafunzo.

Katika hatua nyingine Kamanda Mpinga amesema Kikosi chake kimekuwa kikifanya utambuzi wa maeneo hatarishi (Black spot areas) kwa kutumia takwimu za matukio ya ajali za barabarani.

Kikosi cha usalama barabarani kimeboresha taratibu za ukaguzi wa magari kwenye barabara kuu ili kudhibiti madereva wasiozingatia sheria  na kanuni za usalama barabarani.

No comments:

Post a Comment