Wednesday, May 7, 2014

Dowuta chaitaka Serikali kuwachukulia hatua wanaopandikiza chuki za kikabila na kidini Bandarini


Na Lucy Ngowi
CHAMA cha Wafanyakazi wa Shughuli za Meli na Bandari Tanzania (Dowuta), kinatoa rai kwa serikali kuchukua hatua za kisheria kwa wote wanaopandikiza chuki za kikabila kwa habari zinazohusu bandari kwa kuwa wanachochea chuki ya kikabila na kidini miongoni mwa wafanyakazi wa taasisi hiyo.

Mwenyekiti wa Dowuta Taifa, Edmund Njowoka alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kutoa ufafanuzi kuhusiana na habari mbalimbali zinazohusu wafanyakazi wa taasisi hiyo ambazo zimekuwa zikichapishwa mfululizo katika gazeti moja la kila wiki.

Alisema kama mwenyekiti wa chama hicho, amekuwa akisoma habari mbalimbali kuhusu madai ya kunyanyaswa, kudanganywa, kubaguliwa  na hata kutishwa kwa wafanyakazi kunakodaiwa kufanywa na mtendaji mkuu wa taasisi hiyo.

“Ilinishangaza sana kama kweli matendo hayo yanaweza kufanyika mbele ya Dowuta ninayoiamini kwa umakini wa kusimamia maslahi na haki za wafanyakazi na yenyewe ikakaa kimya,” alisema mwenyekiti huyo na kuongeza kuwa, habari hizo baada ya kuzifuatilia amegundua kuwa hazina ukweli.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, habari zilizoandikwa kuhusu bandari inakufa, wafanyakazi kunyanyaswa, wafanyakazi kustaafu kabla ya umri, uteuzi wa mjumbe wa bodi na mradi wa ujenzi wa nyumba ya mapumziko katika fukwe ya Matema, hazina ukweli wowote.

Alisema, taasisi ya bandari ni nyeti kwa uchumi wan chi, izingatiwe kuwa chuki hii ikiachwa itasambaa na kusababisha madhara makubwa kwa taifa, “Tujifunze yaliyotokea Rwanda mwaka 1994,”.

No comments:

Post a Comment