Saturday, May 10, 2014

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ahitimisha Mkutano wa 12 wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani


Na Othman Khamis Ame,
Ofisi ya Makamu wa Pili 
wa Rais wa Zanzibar

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema  Zanzibar inafikiria kujenga Ukumbi Mkubwa wa Heshima ili ipate fursa zaidi ya kujitangaza katika Nyanja za Kimataifa Kiutalii. 
 Alisema Zanzibar na Tanzania kwa ujumla zimebarikiwa kuwa na mandhari nzuri sambamba na Rasilmali nyingi za kuvutia zinazoweza kutoa fursa kadhaa za kuongezeka kwa uchumi. 
 Balozi Seif alieleza hayo wakati akizungumza na Ujumbe wa Chama cha Majaji Wanawake Tanzania { TAWJA } ukiongozwa na Mwenyekiti wa Chama hicho Jaji Engera Kileo hapo katika Hoteli ya Kimataifa ya Naura Spring Mjini Arusha. Mazungumzo hayo yalifanyika mwishoni mwa Mkutano wa 12 wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani { IAWJ } uliochukuwa siku Nne na kufanyika ndani ya Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Arusha {AICC }. 
Alisema Dunia inaelewa uzuri wa Tanzania Kiutalii na kimazingira jambo ambalo Serikali kwa kushirikiana na taasisi na jumuiya za kiraia zinapaswa kujiandaa mapema katika kujenga miundo mbinu itakayosaidia kuzitumia vizuri rasilmali hizo pamoja na mandhari zilizomo. 
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alivipongeza Vyama vya Majaji Wanawake vya Dunia na Tanzania kwa uamuzi wao wa kuufanya Mkutano wa 12 wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani { IAWJ} kufanyika Nchini Tanzania. 
 Balozi Seif alisema Mkutano huo kwa kiasi kikubwa umesaidia kuongeza Uchumi na mapato ya Taifa kwa vile washiriki wa Mkutano huo wametumia fursa kubwa ya kutembelea maeneo ya historia pamoja na mbuga za Taifa. 
 Mapema Mwenyekiti wa Chama cha Majaji Wanawake Tanzania {TAWJA } Jaji Engera Kileo alisema Mkutano huo umeisaidia Tanzania kujitangaza vyema kiutalii, kiutamaduni na kimazingira. Jaji Engera alisema wajumbe wa Mataifa 50 kati ya 100 wanachama wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani { IAWJ } yaliyojumuisha washiriki wapatao 550 katika Mkutano huo wamevutiwa na hali ya mazingira ya Historia ya Tanzania. 
 Mwenyekiti huyo wa Chama cha Majaji wanawake Tanzania alieleza kwamba vikao vya Chama cha Majaji Wanawake Duniani { IAWJ } kimekuwa kikiendesha mikutano yake kila baada ya miaka miwili katika nchi mbali mbali wanachama. 
 Alisema Mkutano wa kwanza wa Chama hicho ulifanyika Nchini Argentina na huu wa Tanzania ni mara ya pili kufanyika Barani Afrika ukitanguliwa na ule wa Uganda mwaka 2008. 
Wajumbe wa Mkutano huo wa 12 wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani walipata fursa ya kujumuika pamoja katika chakula cha usiku kilichondaliwa maalum kwa ajili ya kuagana baada ya kumaliza mkutano wao. 
Tafrija hiyo ilifanyika katika Hoteli ya Maunt Meru ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiambatana pamoja na Jaji Mkuu wa Tanzania Mh. Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu wa Zanzibar Mh. Omar Othman Makungu. 
Chakula hicho cha usiku kiliambatana na ngoma za Utamaduni kutoka Kikundi cha Jeshi la Kujenga Taifa { JKT } Kambi ya Oljoro pamoja na Muziki wa waimbaji mbali mbali ndani na nje ya Nchi ambapo Wajumbe hao walipata fursa ya kujimwaga vyema uwanjani. 

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi pamoja na Mkewe Mama Pili Juma Iddi kulia wakiwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mh. Mohamed Chande Othman kwenye tafrija maalum kwenye Hoteli ya Mount Meru baada ya kumalizika kwa Mkutano wa Chama cha Majaji Wanawake uliofanyika Mkoani Arusha.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  akibadilishana mawazo na Mwenyekiti wa Chama cha Majaji Wanawake wa Philippines  Jaji Teresita Leonardo – De Castro. Kushoto Jaji Mkuu wa Tanzania  Mhe.  Mohamed Chande Othman.
 Kikundi cha Utamaduni cha Jeshi la Kujenga Taifa Oljoro kikitumbuiza ngoma maarufu ya Kibati yenye Asili ya Mkoa wa Kaskazini Pemba kwenye Tafrija ya Chama cha Majaji Wanawake Duniani iliyofanyika kwenye Hoteli ya Mount Meru Arusha.
 Baadhi ya Wajumbe wa Mkutano wa 12 wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani wakijipatia chakula cha jioni baada ya kumalizika kwa Mkutano wao wa siku Nne Mjini Arusha.
 Baadhi ya Wajumbe wa Mkutano wa 12 wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani wakijipatia chakula cha jioni baada ya kumalizika kwa Mkutano wao wa siku Nne Mjini Arusha.
 Mwenyekiti wa Chama cha Majaji Wanawake kutoka Nchini Philippines Jaji Teresita Leonardo – De Castro akifurahia  chakula murua cha kitanzania kilichoandaliwa kwa wajumbe wa Mkutano wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani Mjini Arusha Tanzania
 Mwenyekiti wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani { IAWJ } Jaji Eusebia Munuo akijipatia mlo kwenye chakula cha usiku kilichoandaliwa kwa ajili ya Wajumbe wa Mkutano huo wa 12.
 Jaji Mkuu wa Tanzania Mh. Mohamed Chande Othman akijumuika pamoja na wajumbe wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani kwenye chakula cha usiku kilichoandaliwa kwa ajili ya wajumbe hao.Kulia ya Jaji Chande ni Jaji Mkuu wa Zanzibar Mh. Omar  Othman Makungu  akipatiwa huduma za mlo na Mkuu wa Mapishi wa Hoteli ya Mount Meru Prosper Makongo.
 Bendi ya Kibo Sounds ikiendelea kutumbuiza kwenye tafrija ya chakula cha usiku kwa ajili ya wajumbe wa Mkutano wa 12 wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani hapo Mount Meru Hoteli Arusha.
 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Mahakama ya Kimataifa Jaji Sanji Mmasenono Monageng Raia wa Jamuhuri ya Botswana akifurahia Tuzo Maalum aliyokabidhiwa na Mwenyekiti wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani Jaji Eusebia Munuo kushoto yake kwenye Tafrija ya Wajumbe wa Mkutano huo iliyofanyika Mkoani Arusha.Pembeni yao kulia ni Mkurugenzi  Mkuu wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani      { IAWJ } anayefanya kazi zake  Makuu ya Chama hicho Mjini Washington Marekani Jaji J. Winship.
 Jaji Mkuu wa Tanzania Mh. Mohamed Chande Othman akitoa neno la shukrani kwenye tafrija maalum ya chakula cha usiku iliyoandaliwa kwa ajili ya Wajumbe wa Mkutano wa 12 wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani hapo Hoteli ya Mount Meru Arusha.
  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  Ali Iddi akisalimiana na Mjumbe wa Chama cha Majaji Duniani kutoka Nchini Swatzeland    Jaji Sandry kwenye Tarija maalum ya Wajumbe wa Mkutano wa Majaji Wanawake Duniani.
 Wajumbe wa Mkutano wa 12 wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani wakiserebuka kwenye Ngoma za hali ya juu zilizochaguliwa maalum kuwaburudisha baada ya kumaliza kazi ngumu ya Mkutano wao uliofanyika Mjini Arusha.
 Wajumbe wa Mkutano wa 12 wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani wakiserebuka kwenye Ngoma za hali ya juu zilizochaguliwa maalum kuwaburudisha baada ya kumaliza kazi ngumu ya Mkutano wao uliofanyika Mjini Arusha.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kati kati  akibadilishana mawazo na Mwenyekiti wa Chama cha Majaji Wanawake cha Tanzania { TAWJA } Engera Kileo alipofika kwa mafungumzo  hapo Hoteli ya Naura Spring iliyopo Arusha. Kulia ya Balozi Seif ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Majaji Wanawake Tanzania Jaji Imani Aboud.
Mwenyekiti wa Chama cha Majaji Wanawake cha Tanzania { TAWJA } Engera Kileo akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwenye Hoteli ya Kimataifa ya Naura Spring Mjini Arusha. Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.

No comments:

Post a Comment