Katibu Mkuu wa CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiwasilisha taarifa ya chama hicho kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita kwenye mkutano mkuu wa chama hicho unaofanyika Ubungo, Plaza Dar es Salaam jana.
Baadhi ya wajumbe wa mkutano mkuu wa CUF Taifa, wakimsikiliza Katibu Mkuu wa CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, wakati akiwasilisha taarifa ya chama hicho, kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita kwenye mkutano mkuu wa chama hicho, unaofanyika Ubungo Plaza Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad (kushoto), akimkabidhi kadi ya CUF mmoja kati ya vijana wanaomaliza Vyuo, Dar es Salaam leo.
Baadhi
ya vijana wanaomaliza vyuo vikuu wakimsikiliza Katibu Mkuu wa CUF Mhe.
Maalim Seif Sharif Hamad, katika ukumbi wa Lamada Dar es Salaam. (Picha
na Salmin Said, OMKR)
Na Hassan Hamad, OMKR
DAR ES SALAAM 24/06/014.
DAR ES SALAAM 24/06/014.
Katibu Mkuu wa Chama
Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesema mafanikio na changamoto
za chama hicho katika kipindi cha miaka mitano iliyopita viwe vitendea kazi kwa
uongozi mpya wa chama utakaopatikana baada ya uchaguzi mkuu wa chama hicho unaoanza
rasmi kesho tarehe 25/06/2014.
Maalim Seif ametoa
kauli hiyo wakati akiwasilisha taarifa ya kazi za chama kwa kipindi cha miaka
mitano iliyopita kwenye mkutano mkuu wa chama hicho unaoendelea katika ukumbi
wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam.
Amesema katika
kipindi hicho chama kimepata mafanikio makubwa, licha ya kuwepo changamoto
nyingi, na kwamba kila mjumbe anapaswa kuzingatia maslahi mapana ya chama na
kuweza kutafakari juu ya uwezo wake, uzalendo na uwajibikaji kwa maslahi ya chama
hicho.
Ametaja baadhi ya
mafanikio yaliyopatikana katika kipindi hicho cha miaka mitano iliyopita kuwa
ni pamoja na kuendelea kumiliki kampuni inayochapisha gazeti la FAHAMU
linalochapishwa kila siku ya Jumanne, ambapo kampuni hiyo sasa inakamilisha
mchakato wa kukifanya chama hicho kianze kumiliki vituo vya redio kabla ya
uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Maalim Seif ambaye
pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amefahamisha kuwa chama chake pia kimefanikiwa
kushiriki chaguzi mbali mbali zinazofanyika nchini, sambamba na kuendelea
kujifunza mabadiliko ya mbinu za uchaguzi kutoka kwa wapinzani wao, na hivyo
kujizatiti zaidi katika chaguzi zijazo.
Aidha amesema chama
hicho kimefanikiwa kufanya ziara kwa asilimia 70 kwa Wilaya za Tanzania Bara na
asilimia 100 kwa Wilaya za Zanzibar, zikiwa na lengo la uimarishaji na ujenzi
wa chama katika ngazi za chini.
Kuhusu changamoto
Maalim Seif amesema ni pamoja na ukosefu wa vyanzo vya mapato ambapo kwa sasa wanategemea vyanzo vichache
vya mapato vikiwemo ruzuku kutoka serikalini pamoja na michango ya wabunge na
wawakilishi ambavyo havimudu kutekeleza hata nusu ya vipaumbelea vya chama,
ukiachilia mbali matumizi ya kawaida ya chama.
Hivyo amewataka
wajumbe wa mkutano mkuu Taifa kubuni vyanzo vyengine vya mapato ili kuongeza
mapato ya chama na kuweza kutekeza majukumu mengi zaidi.
Ametaja changamoto
nyengine kuwa ni upungufu wa vitendea kazi vikiwemo vyombo vya usafiri katika ngazi
zote za uongozi na hivyo kuzorotesha utendaji wa chama hicho.
Aidha amesema baadhi
ya viongozi na wanachama wamekuwa wakitishwa, kubambikiziwa kesi na wengine
kufungwa, jambo ambalo limekuwa likiwavunja moyo watendaji wa ngazi mbali mbali
katika chama.
Mapema wakichangia
taarifa hizo za chama, baadhi ya wajumbe wa mkutano huo wamewaomba viongozi wa
kitaifa wa chama hicho kufanya juhudi za ziada ili kuhakikisha kuwa
wanazitembelea Wilaya zote za Tanzania, bila kujali wingi au uchache wa
wanachama katika Wilaya hizo.
Wakati huo huo
akizungumza na vijana wa CUF wanaomaliza vyuo vikuu, Maalim Seif ameahidi
kuiimarisha Jumuiya ya vijana ya chama hicho (JUVI CUF), ili kuiwezesha kuwa na
program endelevu zitakazosaidia kuwajengea uwezo zaidi vijana ili waweze
kushika hatamu za uongozi.
Jumla ya vijana 54 wanaomaliza
vyuo vikuu walijiunga na CUF kwenye hafla hiyo iliyofanyika ukumbi wa Lamada
Dar es Salaam, na kuahidi kushirikiana
na chama hicho katika kuleta ufanisi zaidi.
No comments:
Post a Comment