Jeshi
la Polisi mkoani Kagera linawashikilia watu 30 wakazi wa Wilaya ya
Muleba kwa tuhuma za vurugu na uharibifu wa mali uliotokea wilayani
humo, ikiwemo kuvunja chumba cha kuhifadhia maiti katika Kituo cha Afya
Kaigara na kuchoma nyumba moto.
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Kagera, George Mayunga, aliwaambia waandishi wa habari
jana kuwa chanzo cha uharibifu huo ni kifo cha Asera Triphone (16)
kilichotokea Juni 12, mwaka huu katika Hospitali ya Mount Meru mkoani
Arusha.
Alisema kuwa
baada ya kufariki kwa mtoto huyo, mwajiri wake, Valentina Maxmilian,
alichukua jukumu la kusafirisha mwili wa marehemu kwenda kwa wazazi wake
wilayani Muleba kwa ajili ya mazishi.
Alisema
wakati mwili unafikishwa nyumbani kwa baba wa marehemu, Triphone Joseph,
alikuwa na taarifa kuwa mwanae ameuawa kwa mateso, ikiwa ni pamoja na
kuondolewa baadhi ya viungo vyake vya mwili, zikiwemo sehemu za siri.
Alisema
wazazi hao walitoa taarifa kituo cha polisi wakiomba mwili wa marehemu
upelekwe kituo cha afya cha Kaigara kwa ajili ya uchunguzi wa kidaktari
ombi lililopingwa na polisi ambao walitaka mwili huo ukafanyiwe
uchunguzi katika Hospitali ya Mkoa wa Kagera.
Alisema
kutokana na msimamo wa polisi, kundi la wananchi lilihamasishwa na
kuamua kubeba jeneza la marehemu kutoka Kijiji cha Bukono na kulipeleka
Muleba kisha kulitelekeza barabarani, lakini mwili huo ulichukuliwa
ukahifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha kituo cha Kaigara
ili kusubiri utaratibu wa kufanya uchunguzi.
Kwa mujibu
wa kamanda, wazazi wa mtoto bado walikuwa wakishinikiza uchunguzi wa
kidaktari ufanyike kubaini chanzo cha kifo cha binti yao.
Alisema
kabla ya utafiti huo kufanyika, wananchi wakaamua kuvunja mlango wa
chumba cha kuhifadhia maiti cha kituo hicho ambapo polisi waliingilia
kati na kutumia nguvu kuwadhibiti.
Alisema wazazi
wa marehemu walikubali kuchukua mwili wa mtoto wao kwa ajili ya
taratibu za mazishi huko kijijini kwao Bukono na kuwa tayari
wameshazika.
Aliongeza
kuwa ilipofika usiku saa mbili, uhamasishaji uliendelea, likatoka kundi
la watu na kwenda nyumbani kwa Veronica Maxmilian, mama wa mwajiri wa
marehemu katika Kijiji cha Buyango, na kuchoma moto nyumba mbili.
Alisema
hatua za kisheria zimechukuliwa kwa kuwakamata waliohusika na uvunjaji
wa kituo cha afya, kutelekeza maiti barabarani na uchomaji wa nyumba
mbili za familia ya mwajiri wa msichana huyo.
Alisema watu
30 wanashikiliwa kwa lengo la kuwahoji ili kuwabaini vinara wa vurugu
hizo na kuwa ukamataji huo ulifanyika baada ya kupata taarifa mbalimbali
zilizolifikia jeshi hilo.
Hata hivyo,
alisema mwajiri wa marehemu anashikiliwa na jeshi hilo kwa ajili ya
upelelezi wa kina ambao utafanyika hapa Kagera na mkoani Arusha pamoja
na jirani wanaomzunguka.
No comments:
Post a Comment