Mkutano
Mkuu wa marekebisho ya baadhi ya vipengele kwenye Katiba ya Yanga
umefanyika na kumalizika salama na furaha kwenye Ukumbi wa Bwalo la
Polisi -Oysterbay huku wanachama wakipitisha kipengele cha kuundwa kwa
kamati ya maadili.
Mwenyekiti wa klabu ya Yanga SC Yusuf Manji
amewaongoza wanachama hai wapatao 1,560 kupitisha kipengele hicho kipya
kwa ajili ya maslahi na faida ya Wana Yanga kwani bila kufanya hivyo
timu isingeweza kuruhusiwa kushiriki Ligi Kuu msimu ujao.
Aidha katika mkutano huo Manji amewatoa hofu
wanachama kwa kuwaambia kuwa usajili unaendelea kufanyika na nafasi
zilizobakia ni nne tu hivyo pindi utakapokamilika basi wataweka wazi
kila kitu.
Kuhusu nafasi ya Kocha Mkuu Manji amesema
Kamati ya Mashindano imemkabidhi mapendekezo yao na kwa sasa yupo kwenye
mazungumzo na Marcio Maximo aliyewahi kuwa kocha mkuu wa timu ya Taifa
Tanzania kuja kukinoa kikosi cha Jangwani.
Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini Mama Fatma
Karume aliongoza kikao cha waachama kilichomuomba Bw Manji kuendelea na
uongozi ambapo mwenyeikti alitoka nje na kamati yake ya utendaji na
pindi waliporejea walikubali ombi hilo na kusema watafuata taratibu za
kikatiba.
Mwisho kupitia mkutano mkuu wa leo wa
wanachama umeazimia kuwaongezea muda wa mwaka mmoja Mwenyekiti Yusuf
Manji pamoja na Makamu wake Clement Sanga ili waweze kukamilisha masuala
ya katiba na kuweza kuandaa mkutano wa uchaguzi baada ya katiba
kupitishwa na TFF.
No comments:
Post a Comment