Tuesday, July 15, 2014

Bomu la Olasiti lamkata mguu


Mwalimu Fatuma Tarimo
Zilikuwa siku, wiki, miezi na sasa ni zaidi ya mwaka umepita tangu kutokea kwa mlipuko wa bomu kwenye Kanisa la Olasiti,  (Parokia ya Mtakatifu Joseph Mfanyakazi jijini Arusha na kusababisha vifo vya watu watatu na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Hata hivyo, hadi sasa hakuna kikundi wala mtu yeyote aliyekamatwa na kufikishwa mahakamani kuhusiana na tukio hili lililoua watu watatu na kujeruhi wengine zaidi ya 80.

Elizaberth Isidori (20), mmoja wa manusura katika tukio hilo, amejikuta akilazimika kurudia tena masomo ya kidato cha tatu akiwa katika Shule ya Sekondari Olasiti. Hiyo ni baada ya bomu kumlipua mguu wa kulia ambao umekatwa na kumuacha akiwa na ulemavu wa kudumu maishani mwake.

"Naumia sana nikisikia (Polisi) bado hawajafanikiwa kumkamata mtu wala kikundi cha watu waliohusika na tukio hili. Pia najisikia vibaya kila ninaposikia kuna matukio mengine ya ulipuaji yakitokea hapa Arusha huku wahusika wakifanikiwa kukwepa mkono mrefu wa serikali.... nawaombea (Polisi) ili jitihada zao zizae matunda na wote walionipa ulemavu huu na kusababisha vifo vya watu wengine wasio na hatia wakamatwe na kuchukuliwa hatua zinazostahili," ndivyo anavyoanza kusimulia Elizaberth, mmoja wa majeruhi walioumia vibaya kutokana na tukio hilo lililojiri Jumapili ya Mei 4, 2013.

Elizaberth ana kila sababu ya kujawa machungu. Taarifa za kuwapo kwa matukio mengine zaidi ya milipuko ya mabomu huku pia bado kukiwa hakuna watu au kikundi kilichokamatwa kuhusiana na tukio lililomsababishia ulemavu siyo habari njema kwake.

Aidha, rekodi zinaonyesha kuwa mbali na tukio la Olasiti, baadhi ya matukio ya mabomu mjini Arusha ni pamoja na tukio la Juni 15, 2013, likihusisha bomu lililorushwa kwenye mkutano wa kufunga kampeni wa Chadema kwenye viwanja vya Soweto ambapo watu wanne waliripotiwa kufa na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Aprili 13, 2014,  mlipuko mwingine wa bomu ulitokea katika baa ya Arusha Night Park na kusababisha kifo cha mtu mmoja huku watu wengine 14 wakijeruhiwa; Julai 4 mwaka huu akajeruhiwa Sheikh Sood Ally Sood wa Msikiti wa Qiblatan uliopo Kilombero jijini hapa alijeruhiwa  kwa bomu la kurushwa kwa mkono wakati akila daku nyumbani kwake.

Tukio la hivi karibuni ni lile lililotokea usiku wa kuamkia Jumatatu (Julai 8), kwenye  mgahawa wa Vama Traditional Indian Cuisine ulioko eneo la Arusha Gymkhana, karibu na eneo la Mahakam Kuu ambapo watu nane wamejeruhiwa, akiwamo mmoja aliyekatwa mguu katika Hospitali ya Rufaa ya Selian. 

ILIVYOKUWA
Wakati akizungumza na mwandishi wa NIPASHE katika mahojiano maalum mwishoni mwa wiki kwenye Mtaa wa Mji Mpya uliopo Olasiti, Elizaberth alisema kuwa anakumbuka vyema juu ya kile kilichotokea Siku hiyo, Elizaberth alikuwa ni miongoni mwa waumini waliokuwapo katika viunga vya Kanisa la Olasiti kwa ajili ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu ya uzinduzi wa jengo la kanisa hilo; ibada iliyokuwa ikiongozwa na Balozi wa Vatican nchini, Askofu Mkuu, Francis Padilla, akishirikiana na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki  la Arusha, Josephat Lebulu.

Elizaberth anasema kuwa siku hiyo alienda kanisani akiwa na wadogo zake wawili na kukuta waumini wengine kadhaa wakiwa tayari wameshaingia ndani ya uzio wa kanisa.

“Tulifika katika wakati ambao Askofu Mkuu Lebulu alikuwa anabariki maji ili Balozi wa Vatican nchini (Askofu Padilla), akate utepe kuashiria uzinduzi wa jengo la kanisa," anasema Elizaberth.

“Wakati anabariki, mara kuna kitu kama jiwe hivi kikarushwa. Hatukujua ni nini. Baadhi walidhani ni jiwe limerushwa na kuna mama mmoja niliyekuwa naye jirani aligongwa na kitu hicho begani kabla hakijatua chini.

“Ghafla tulisikia mlipuko mkubwa sana... na mimi nikajikuta nipo chini. Watu walianza kukimbia ovyo. Na mimi nilitaka kukimbia, lakini nikahisi mguu wangu umekufa ganzi. Sikuweza kabisa.

Nikajitajidi na kujiburuza hadi nje ya uzio. Halafu nikachukuliwa kwenye gari na kukimbiziwa Hospitali ya Mount Meru," anasema."Kufika hospitali, nikapelekwa chumba cha upasuaji. Baada ya hapo nikapoteza fahamu, sikuweza tena kujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea."

Elizaberth anasema kuwa ndugu zake wawili walisalimika, lakini baada ya hapo yeye alilazwa Mount Meru kwa siku nne. Halafu akahamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC iliyopo mjini Moshi ambako alilazwa kwa zaidi ya miezi miwili na huko ndiko alikokatwa mguu wake aliokuwa akiuhisi ganzi kabla ya kubaini baadaye kuwa umeumia vibaya sana.

"Nilienda Aprili 9 na kuruhusiwa kutoka hospitali Juni 27, 2013," anasema.Baba mdogo wa Elizabeth anayeishi naye jijini hapa, Edmund Gaspar Balaga, ambaye ni fundi ujenzi, anasema analishukuru Kanisa la Olasiti kwa msaada mkubwa iliowapatia wakati wa kumuuguza binti yake, ikiwa ni pamoja na kumnunulia mguu wa bandia uliogharimu Sh. milioni mbili. 

"Baada ya kupona, tulimhamisha kutoka Shule ya Oljoro kumleta hapa Olasiti ambako ni jirani na tunakoishi," alisema Balaga.

MWALIMU MONICA
Athari kwa watu waliokumbwa na mlipuko wa bomu Olasiti ni kubwa. Mbali na Elizaberth ambaye sasa anaishi na mguu wa bandia, mwingine aliyejeruhiwa vibaya alikuwa ni Monica Tarimo 'Mwalimu Fatuma' (40), ambaye hadi sasa anaishi na vipande viwili vya vyuma vilivyotokana na bomu hilo; kimoja kikiwa kimejikita katika sehemu ya mapafu, jirani na moyo na kingine jirani na pingili za shingo.

Anasema madaktari wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) ambako alihamishiwa kwa matibabu zaidi kutoka Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru wameshindwa kuviondoa vyuma hivyo kwavile vimekaa katika maeneo hatari ya mwili.

Akisimulia kilichotokea siku ya tukio, Mwalimu Fatuma anasema aliona kitu chenye umbile la yai, kikiwa na nyaya za rangi ya kijani na njano na kilianguka umbali kama wa mita mbili tu kutoka katika mahala alipokuwa amesimama.

“Ghafla nikasikia mlipuko mkubwa na nikapata joto kali sehemu ya mguu wangu wa kulia. Nikanyanyuliwa kwa nguvu na kudondoka chini... nilishindwa kukimbia kwa sababu kifua kilikuwa kimejaa moshi.

“Baadaye nikaanza kuomba msaada. Watu wakaja kuninyanyua na mimi na majeruhi wengine kadhaa tukapelekwa katika Hospitali ya Father Babu. Huko nilishonwa mguu, kidole cha pete na sehemu ya chini ya kidevu,” anasema.

Anasema baadaye ilipobainika kuwa hali yake inazidi kuwa mbaya, akahamishiwa katika Hospitali ya Mount Meru na baadaye akasafirishwa kwa ndege iliyogharimiwa na serikali hadi Muhimbili jijini Dar es Salaam.

“Hali yangu ilikuwa mbaya kiasi kwamba ilidhaniwa kuwa nimefariki," anaeleza.Akiwa hospitali ya mkoa, madaktari walimtoa kipande kimoja cha chuma kilichokuwa kwenye mapafu lakini walishindwa kutoa kingine kilichokuwa jirani na moyo na jirani na pingili za shingo.
“Nililazwa Muhimbili kuanzia Mei 8, 2013 hadi Juni 19, 2013.”

Anasema baada ya hapo amekuwa akiendelea na shughuli zake za kufundisha, lakini kila mara akihudhuria kliniki kuangalia maendeleo yake ya afya yake.

“Hadi sasa nimeshakwenda kliniki mara tatu, yaani Agosti na Novemba mwaka jana na pia Mei mwaka huu. Nimeelezwa kila ninapojisikia vibaya naweza kwenda tena,” anasema.

Mbali na kupata majeraha makubwa, Mwalimu Fatuma anasema vilevile kuwa ameathiriwa sana kisaikolojia na matokeo yake, kila mara anaposikia mshindo hukumbukia tukio la mabomu Olasiti na kukosa raha.

“Sikutegemea tukio kama lile litokee kanisani au sehemu nyingine ya mkusanyiko wa watu. Inasikikitisha sana kutokea kwa mambo haya (ya mabomu) ya kinyama,” anasema Mwalimu Fatuma, ambaye analishukuru kanisa la Olasiti, serikali, madaktari na watu wote waliomsadia katika kupigania maisha yake.
Naye anaiomba serikali iliwezeshe Jeshi la Polisi kwa hali na mali ili kuhakikisha kwamba linapata nguvu na uwezo wa kuwakamata watu wote wanaojihusisha na matendo ya kinyama kama hayo ya kulipua mabomu kwenye hadhara ya watu wasiokuwa na hatia.

KAULI YA POLISI
Akizungumzia matukio ya mabomu ya Arusha, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) wa Jeshi la Polisi nchini, Isaya Mngulu, amekaririwa akisema kuwa hayana uhusiano na matukio ya kigaidi yanayofanywa nchini Kenya; ambako kumekuwa na mashambulizi ya ya kigaidi ya kundi la Al Shabaab.

“Matukio ya mabomu Arusha hayana uhusiano na matukio kikagidi kama yanayotokea nchini Kenya. Pia hayana uhusiano na masuala ya kisiasa,” alisema Mngulu.

Alisema uchunguzi uliofanywa na  Polisi umebaini kuwapo kwa kikundi kinachojihusisha na matukio hayo na kwamba, jeshi hilo litahakikisha watuhumiwa wote wanasakwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo ili kufanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa wa matukio hayo kwani suala la ulinzi na usalama ni jukumu la kila mwananachi.

Aidha, watuhumiwa 16 wanaodaiwa kuhusika na matukio ya ulipuaji wa mabomu walipandishwa kizimbani wiki iliyopita katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha na kunyimwa dhamana.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, watuhumiwa wanadaiwa kulipua mabomu kati ya mwaka 2010 hadi Februari, mwaka huu, maeneo mbalimbali nchini, kinyume cha kifungu cha 118 (1) (a) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya mwaka 2002.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment