Afisa
Mradi wa Elimu ya Afya na VVU/UKIMWI kutoka UNESCO, Bw. Herman Mathias
akitoa mada kuhusu tabia hatarishi zinazochangia maambukizi mapya ua VVU
kwa Vijana katika warsha ya siku tatu ya Mradi wa SHUGA Redio
inayofanyika katika Kituo cha Redio cha Nuru FM mjini Iringa.
Na Mwandishi wetu
Idadi
kubwa ya Vijana hususan wa kike wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24
wanaanza kufanya mapenzi katika umri mdogo jambo ambalo linaashiria
hatari ya maambukizi ya VVU ikilinganishwa na idadi ya Vijana wa Kiume.
Akitoa
mada kuhusu tabia hatarishi zinazochangia maambukizi mapya ua VVU kwa
Vijana katika warsha ya siku tatu ya Mradi wa SHUGA Redio inayofanyika
katika Kituo cha Redio cha Nuru FM mjini Iringa, Afisa Mradi wa Elimu ya
Afya na VVU/UKIMWI kutoka UNESCO, Bw. Herman Mathias, amesema hadi sasa
kuna Asilimia 3.9 ya wasichana wenye umri huo wamepata maambukizi ya
VVU ikilingaishwa na asilimia 1.7 ya wavulana.
Kufanya
mapenzi pia katika umri mdogo kunachangia kwa kiasi kikubwa mimba za
utotoni na kuathiri ustawi wa maisha ya wasichana. Wastani wa watoto wa
kike 6,000 huachishwa masomo kila mwaka kutokana na mimba za utotoni.
Mratibu
na Mkufunzi wa Redio Jamii kutoka UNESCO, Bi. Rose Haji Mwalimu
akichangia mada iliyotolewa na Afisa Mradi wa Elimu ya Afya na
VVU/UKIMWI kutoka UNESCO, Bw. Herman Mathias (hayupo pichani) katika
warsha ya siku tatu ya Mradi wa SHUGA Redio inayofanyika katika Kituo
cha Redio cha Nuru FM mjini Iringa.
“Wasichana
wengi wamekatishwa masomo kwa ajili ya kupata Mimba za utotoni
zinazochangiwa na kufanya mapenzi katika umri mdogo tabia ambayo pia
inachangia maambukizi ya VVU”, alisema Bw. Mathias.
Amezitaja
tabia nyingine hatarishi zinazochangia maambukizi ya VVU kuwa ni kuwa
na wapenzi wengi kwa wakati mmoja, kuwa na wapenzi wenye umri mkubwa na
ngono wenzi.
Nyingine
ni matumizi duni na yasiyoendelevu ya Kondomu, kufanya ngono wakati
umelewa, ngono kinyume na maumbile na ngono ya jinsia moja.
Akichangia
suala hilo Mratibu na Mkufunzi wa Redio Jamii kutoka UNESCO, Bi. Rose
Haji Mwalimu amesema tamaduni zinazoendelezwa katika jamii pia
zinachangia kumuweka msichana katika kundi hatarishi la kupata
maambukizi ya VVU.
Afisa
Mipango VVU/UKIMWI kutoka UNICEF, Bi. Alice Ijumbe akitoa mada ya Afya
ya Uzazi kwa Vijana na mahusiano yake na maambukizi ya VVU wakati wa
warsha ya siku tatu ya Mradi wa SHUGA Redio inayofanyika katika Kituo
cha Redio cha Nuru FM mjini Iringa.
Amezitaja
tamaduni hizo ikiwa ni pamoja na kumbagua Mwanamke katika majukumu
mbalimbali Kijinsia kutokana na tabia inayofundishwa na kutolewa kwa mtu
kulingana na jinsi yake.
“Jinsia,
Utamaduni na VVU ni masuala yenye mahusiano yanayomuweka Mwanamke
katika hali ya hatarishi kupata maambukizi ya VVU, na kubadili tabia si
jambo rahisi kwa sababu limejikita katika tamaduni zetu zinazoelekeza
majukumu mbalimbali ya mwanamke na mwanaume kijinsia na hivyo kuchangia
maambuki ya VVU” amesema Bi. Mwalimu.
Amesema
ni jukumu la Wanahabari Vijana kuhakikisha kuwa wanahamasisha
kubadilisha tabia hatarishi zinazochangia maambukizi ya VVU ambazo
zimemzunguka mwanamke.
Baadhi
ya mifano halisi ya kijinsia kwa wanaume na wanawake katika Afrika
ikiwemo Tanzania ni kumuona mwanamume kama kiongozi katika kaya, jamii
na kuwajibika kufanya maamuzi yote wakati mwanamke huonekana ni mlezi na
kulinganishwa na mtoto mdogo.
Mfano
mwingine ni mitala. Mahusiano ya kimapenzi hata katika jamii
isiyokumbatia mitala kutoka na tamaduni zilizojikita katika jamii
inakubalika kwamba mwanaume ana haki ya kuwa na wapenzi wengi wakati
wanawake wanatakiwa kuwa waaminifu kwa mtu mmoja ambao ni waume zao.
“Wanawake
pia wanatarajiwa kuwa watiifu kwa waume zao lakini utiifu huo
hautegemewi wapewe wanawake kutoka kwa waume zao. Wanawake watakaokwenda
kinyume na kanuni hiyo hunyooshewa vidole na kuambiwa kuwa wazinzi na
wanaweza kuadhibiwa na jamii kwa namna yoyote ile hususani kupigwa,
kutolewa maneno makali na kupewa talaka lakini wanaume hawafanyiwi
hivyo”.
Kutokana
na tamaduni hizo yanajengwa mazingira ambayo mwanamke anakuwa hana
uwezo wa kujadili masuala ya ngono salama au ya kuridhisha kwa sababu
kunakuwa hakuna mawasiliano katika nyumba kuhusu ngono kati ya mume na
mke.
Mshiriki wa warsha hiyo Veronica Mtauka kutoka Kitulo FM Redio Makete akishiriki kuchangia mada wakati wa warsha hiyo.
Mradi
wa SHUGA Redio unaotekelezwa kwa ushirikiano wa Mashirika ya Kimataifa
moja linaloshughulikia Huduma za Watoto (UNICEF), Elimu, Sayansi na
Utamaduni (UNESCO) na Redio Jamii 10 nchini Tanzania una lengo la
kuendeleza kampeni za hamasa kwa vijana kupunguza maambukizi mapya ya
VVU.
Redio
hizo ni kutoka Karagwe, Kahama, Kyela, Kitulo na Kwanza Jamii. Nyingine
ni kutoka Iringa, Simanjiro, Ifakara, Sengerema na Uvinza.
Mtangazaji wa Uvinza FM Redio, Mwinyi Mtulla akichangia hoja wakati wa warsha hiyo ya siku tatu inayoendelea mjini Iringa.
Mratibu
na Mkufunzi wa Redio Jamii kutoka UNESCO, Bi. Rose Haji Mwalimu
akiwaelekeza jambo baadhi ya washiriki wakati wa warsha hiyo
inayoendelea kwenye kituo cha Redio Nuru FM mjini Iringa.
Pichani
juu na chini ni baadhi ya washiriki wa warsha ya siku tatu ya Mradi wa
SHUGA Redio inayofanyika katika Kituo cha Redio cha Nuru FM mjini Iringa
inayolenga kuendeleza kampeni za hamasa kwa vijana kupunguza maambukizi
mapya ya VVU.
Baadhi ya washiriki kutoka Redio za Jamii mbalimbali watakaotekeleza Mradi wa SHUGA Redio wakiwa kwenye vikundi kazi.
No comments:
Post a Comment