SIKU
ya Agosti 8, mwaka huu kutakuwa na bonge la mechi litakalopigwa katika
Uwanja wa Taifa jijini Dar ambapo wabunge wanaoshabikia Yanga, watakuwa
dimbani kupepetana na wenzao wa Simba.
Hebu
jaribu kuvuta picha katika ubongo wako, waheshimiwa wabunge watakapoweka
kando masuala ya ‘Ukawa’ na ‘Tanzania Kwanza’, kisha kukutana katika
uwanja kuonyeshana umwamba kwa kusakata gozi la ng’ombe katika mchezo
huu wa kihistoria.
Kila
timu tayari imeingia mafichoni kujiwinda na mchezo huo ili kuhakikisha
inaibuka kidedea na kujenga heshima mbele ya watani wao huku Simba
wakiahidi kulipiza kisago cha bao 1-0 walichokipata mwaka jana kutoka
kwa Yanga.
“Tayari
tumeingia kambini kujiwinda na mchezo huu ili kuziba midomo na kelele
za Yanga ambao wamekuwa wakitamba tangu watubahatishe mwaka jana,”
alijinasibu Hamis Kigwangala ambaye ndiye nahodha wa Simba.
Kwa
upande wa mlezi wa Yanga ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Temeke, Abassi
Mtemvu, alijigamba kuwa ni lazima waendeleze moto wa ushindi kwa kuwa
wapo na kikosi imara na tayari wameshaingia kambini kwa kuwa mchezo huu
ni siriazi kwao.
“Kwa
kweli mchezo huu tumeuchukulia kwa mtazamo wa juu kabisa na lazima
tuwapige kwa kuwa tuna damu changa nyingi, hatuna masihara, maana
wakitufunga hatutakaa bungeni.
“Tupo katika maandalizi ya mwisho kwa sasa ingawa tulipoweka kambi yetu itabaki kuwa siri,” alisema Mtemvu kwa kujiamini.
Baadhi
ya wabunge wanaounda timu ya Yanga ni pamoja na Abassi Mtemvu,
Ridhiwani Kikwete, Freeman Mbowe na Mwigulu Nchemba, huku kikosi cha
Simba kikiundwa na wakali kama Zitto Kabwe, Hamisi Kigwangalla, Wiliam
Ngeleja, Juma Nkamia, Amos Makalla na Ismail Aden Rage.
Mbali
na mchezo huo ambao utakuwa kivutio kikubwa kwa wadau wa soka, pia
kutakuwa na mchezo mwingine wa kusisimua pale Bongo Fleva chini ya mkali
wao, Peter Manyika itakapopepetana na Bongo Movie FC chini ya Jacob
Steven JB.
Mkurugenzi
wa Ufundi wa Bongo Movie, Fatuma Makongoro ‘Bi Mwenda’, tayari ameanika
wachezaji wake huku akisema kuwa hahofii kwani kikosi chake kipo
kamiligado kuelekea mchezo huo ambao wameuchukulia kwa umakini mkubwa.
“Sisi
tumeuchukulia ‘serious’ sana mchezo huu kwa kuwa mashabiki wetu watakuja
wengi na hatutakubali kuwaangusha.“Wachezaji waliopo kambini mpaka sasa
ni Mzee Majuto, Kingwendu, Bambo, JB, Steve Nyerere, Dk Cheni, Ray,
Mtitu, Cloud pamoja na Muhogo Mchungu,” alisema Bi Mwenda.
Akijibu
mapigo ya wapinzani wao, kocha wa Bongo Fleva ambaye pia anakinoa
kikosi cha Yanga, Juma Pondamali ‘Mensah’, alisema Bongo Movie wajiandae
kupata kipigo cha mshangao kwa kuwa wao hawatakwenda kuigiza uwanjani.
“Hawa
waigizaji wajiandae na kipigo cha ‘sapraizi’, maana pale sisi hatuendi
kuigiza, tunaenda kupiga kazi kwa kuwa mpira hauigizwi, unachezwa kila
mmoja anaona, sasa acha wapige domo wataona kitakachowakuta,” alisema
Pondamali.
Baadhi ya mastaa wanaounda kikosi cha Bongo Fleva ni pamoja na Peter Manyika, H-Baba, Ali Kiba, Rich One, Kalapina na wengineo.
Ukiachana
na soka, pia kutakuwa na burudani mbalimbali ambapo mastaa kibao kutoka
ndani na nje ya nchi watakuwepo kulipamba jukwaa la Usiku wa Matumaini.
Baadhi
ya mastaa hao ni pamoja na Yemi Alade kutoka Nigeria, Madee, Ali Kiba,
Roma Mkatoliki, Shilole, Menninah, Juma Nature na kundi zima la TMK
Wanaume Halisi.
Mgeni
rasmi katika tamasha hili atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Dk Mohammed Gharib Bilal.Tamasha la Usiku wa Matumaini
limedhaminiwa na Clouds FM (88.5), Times Fm (100.5), Vodacom, Pepsi,
Azam TV pamoja na Syscorp.
JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS
No comments:
Post a Comment