Friday, August 1, 2014

Mwanamke 'aliyeasi dini' awasili Marekani



Mumewe Meriam ni raia wa Marekani
Mwanamke wa Sudan aliyetoroka kutoka nchini humo baada ya kunusurika hukumu ya kifo kwa kosa la ‘kuasi dini ya kiislamu’,Meriam Yahia Ibrahim Ishag, amewasili Marekani.
Alihukumiwa kunyongwa mapema mwaka huu lakini baadaye akaachiliwa huru mwezi Juni baada ya ulimwengu mzima kukemea uamuzi huo uliotolewa na mahakama moja nchini humo.
Babake Bi. Ibrahim ni muislamu na hivyo basi inavyoambatana na sheria za kiislamu za Sudan Bi. Meriam pia ni muislamu na hawezi kuasi dini ya kiislamu.
Lakini Meriam amesisitiza kuwa hajawahi kuwa muumini wa dini ya kiislamu kwani alilelewa na mamake ambaye ni Mkiristo.
Kufuatia malalamiko kutoka kote ulimwenguni, aliachiliwa huru mwezi Juni. Bintiye Meriam, Maya, alizaliwa gerezani mwezi Mei. Baada ya kuachiliwa kutoka gerezani, Meriam alizuiliwa kutoka nchini Sudan na familia yake ikalazimika kutafuta hifadhi katika ubalozi wa Marekani uliopo Khartoum.
Bi. Ibrahim aliwasili Philadelphia kwa ndege Alhamisi jioni kutoka Rome, Italia akiwa na mume wake wa kimarekani.
Mumewe Bi Meriam, Daniel Wani, pia ni muumini wa kikiristo na pia ni mzaliwa wa Sudan kusini lakini ana uraia wa kimerakani.
Meriam aliponea kifo baada ya mahakama kubatilisha uamuzi wa kumnyonga kwa kuasi dini
Meriam alikaribishwa kwa njia ya kipekee alipopitia Philadephia na kutajwa kuwa “mpigania uhuru wa kimataifa’ na mayor wa Philadelphia, Michael Nutter. Nutter pia alisema watu watakumbuka Meriam kama ‘wengine waliotupigania kuwa huru,’ na kumlinganisha Meriam na Rosa Parks.
Rosa Parks alisifika na kutazamwa kuwa ushujaa wa harakati za haki za kiraia nchini Marekani alipokataa kuondokea mwanamme mzungu kitini wakiwa ndani ya gari huko Alabama.
Hatimaye Nutter alimkabidhi Meriam mfano wa ‘kengele ya uhuru,’ ishara ya uhuru wa Marekani. Aidha, kwa mujibu wa msemaji wa Vertican, Bi Meriam akiwa Rome alikutana na papa ‘aliyemshukuru kwa kuwa imara katika Imani yake.”
Safari ya Bi Meriam ilifikia kikomo New Hampshire kwani alikuwa anasubiriwa kwa hamu na ghamu na jamaa na wafuasi wake katika uwanja wa ndege.
Alipoondoka Sudan alipitia Italy ambako alikutana na Papa Francis
Kwa mujibu wa mwanahabari wa BBC aliyeshuhudia tukio hilo, Meriam alikaribishwa na halaiki ya watu, wengine wao wakiimbia “Marekani iishi milele.”
Aidha mwanahabari wetu alituarifu kuwa mume wa Bi Meriam alitoa hotuba fupi na kushukuru serikali ya Marekani na maseneta wa New Hampshire kwa kumpigania na kwa kufanya mipango ya kumpa mke wake hifadhi. Pia alishukuru watu wa Sudan kwa usaidizi wao.
Familia ya Meriam inakusudia kuishi New Hampshire kwani jamaa wa mume wake wako huko.

No comments:

Post a Comment