Wednesday, October 12, 2016

Balozi Seif Ali Iddi akutana na uongozi wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali Tanzania (TSN) na Gazeti la Zanzibar Leo


 Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali Tanzania (TSN) Dr. JimYonazi wa Tatu kutoka Kushoto akifafanua jambo wakati Ujumbe wake ulipofanya mazungumzo na Balozi Seif.
----------------------------------------------------------
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alivikumbusha vyombo vya Habari Nchini kuanzisha utaratibu maalum wa kutumia sehemu ndogo ya ukurasa wa Magazeti wanayochapisha kwa lugha za Kigeni ili kuwapa fursa wageni pamoja na Watalii wanaohitaji kujifunza Lugha ya Kiswahili. 
Alisema lazima ufike wakati kwa Lugha ya Taifa Tanzania ya Kiswahili ienziwe kwa nguvu zote chini ya usimamizi wa wataalamu wa lugha hiyo pamoja na wana Habari kupitia vyombo wanavyofanyia kazi. 
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kumbusho hilo wakati akibadilishana mawazo na Uongozi Mpya wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali Tanzania {TSN } ulioambatana na Uongozi wa Gazeti la Zanzibar Leo mazungumzo yaliyofanyika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. 
Alisema kazi ya vyombo vya Habari wakati wote ni kuelimisha Jamii inayovizunguuka vyombo hivyo. Hivyo lazima watendaji wake wanapaswa kujitahidi kutumia kalamu zao katika kuupatia Habari, Taarifa pamoja na Taaluma njema Umma. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza watendaji wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali Tanzania {TSN }wanaochapisha magazeti ya Dailynews, Sundaynews na Habari leo kwa kazi kubwa wayaoendelea kuitekeleza kwa kipindi kirefu sasa Nchini Tanzania. 
Alisema Dailynews na Sundaynews ni mama wa magazeti Nchini Tanzania yaliyofungua tasnia ya Magazeti ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki kwa miaka mingi iliyopita. 
Balozi Seif alisema kwa kuzingatia ukongwe wa Magazeti hayo aliuomba Uongozi Mpya wa Taasisi hiyo ya Habari Tanzania kuongeza Kuchapisha zaidi Habari zinazolihusu Baraza la Wawakilishi Zanzibar ili zieleweke upande wa Tanzania Bara. 
Akilizungumzia Gazeti la Zanzibar Leo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali inaangalia mbinu za fedha zitakazoliwezesha Gatei hilo kuwa na mtambo wake wa kuchapisha Magazeti yao wenyewe. 
Mapema Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali Tanzania { TSN } Dr. JimYonazi alimueleza Balozi Seif kwamba Kiswahili kinaweza kuuzwa Kimataifa kwa vile hadi sasa hakuna Gazeti linalofundisha Lugha ya Kiswahili katika ukanda wa Afrika Mashariki. 
Dr. Jim Yonazi alisema Lugha hiyo ambayo tayari inazungumzwa Kimataifa katika maeneo mengi Duniani inaweza kutafsiriwa ndani ya magazeti katika lugha nyengine za Kigeni kwa lengo la kutoa nafasi kwa Watu wanaotaka kujifunza Lugha hiyo.
Mhariri Mtendaji huyo wa Magazeti ya Serikali Tanzania aliitaka Jamii ibadilike kufanya biashara ya kisasa kwa kutumia vyombo vya Habari kama magazeti na hata Redio na TV kwa lengo la kukabiliana na mfumo wa Teknolojia ya kisasa ya Habari na Mawasiliano. 
Dr. Jim alisema hivi sasa yapo mabadiliko makubwa ya mfumo wa Teknolojia ya Mawasiliano kiasi kwamba wananchi wanastahiki kujifunza ili kuwepuka kupita na wakati wa sasa unaokwenda kwa kasi Ulimwenguni. 
Alieleza kwamba Kapuni za Habari za Tanzania zinapaswa zikue zaidi kwa kusambaza kazi zao nje ya Tanzania ili kupata fedha za kigeni zitakazosaidia kumudu gharama za uzalishaji.

No comments:

Post a Comment