Na Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.
Ali Mohamed Shein amelisisitiza Bunge la Jumuiya ya Afika Mashariki (EALA)
kuweka mikakati imara katika kukuza sekta ya utalii kwa nchi za Jumuiya hiyo kwani
idadi ya watalii wanaoingia kwenye eneo hilo hailingani na vivutio viliopo.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo huko katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Chukwani Mjini Zanzibar,
wakati akizindua Mkutano wa Pili wa Kikao cha Tano cha Bunge la Tatu la Jumuiya
ya Afrika Mashariki (EALA) unaofanyika Zanzibar.
Amesema kuwa pamoja na
kwamba eneo hilo la nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ina vivutio vingi vya
utalii, idadi ya watalii wasiozidi milioni 5 wanaoingia katika eneo hilo kutoka
nchi za nje ni ndogo ikilinganishwa na watalii Bilioni moja wanaosafiri kwa
mwaka duniani kote.
Dk. Shein ameongeza
kuwa kiasi hicho cha watalii hakilingani na umaarufu pamoja na vivutio
vilivyopo katika eneo hilo la Nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki na kueleza
matumaini yake kwamba idadi hiyo inaweza kuongezeka iwapo juhudi za makusudi
zitachukuliwa.
“Jumla ya watalii
waliotembelea Zanzibar mwaka 2014 walikuwa 311,801 ambapo lengo letu ni kufikia
watalii 500,000 mwaka 2020”,alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kueleza Miswada inayotarajiwa kujadiliwa katika kikao cha
Bunge hilo ikiwa ni pamoja kuweka Sheria kali zitakazopiga marufuku biashara
haramu ya kusafirisha binaadamu ambayo ni uhalifu na ukiukwaji mkubwa wa haki
za binaadamu.
Akizungumzia kuhusu
Mswada wa kudhibiti matumizi ya vifaa vinavyotengenezewa plastiki ikiwemo
mifuko, Dk. Shein alisema kuwa Mswada huo umekuja wakati muwafaka na kwamba
Zanzibar tokea mwaka 2011 imeshaaza kutekeleza kwa vitendo Sheria ya kupiga
marufuku uagiziaji na uzalishaji wa mifuko ya plastiki.
Alisema kuwa uwamuzi
wa kupiga marufuku bidhaa hizo Zanzibar ulichukuliwa baada ya kuona kwamba
mifuko hiyo inaharibu mazingira, yakiwemo mazingira ya bahari pamoja na
kuathiri sekta muhimu ya utalii.
Kwa upande wa Mswaada
wa Usawa wa Kijinsia na maendeleo, Dk. Shein alisema kuwa anamatumaini kuwa
Mswada huo utatoa njia ya kuinua usawa wa kijinsia na ushiriki wa wanawake katika
utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
Dk. Shein alitoa
pongezi kwa uwamuzi wa Bunge hilo kwa kuamua kuifanya Zanzibar kuwa Makao Makuu
ya Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki na kueleza kuwa uamuzi huo ni
sahihi kutokana na ukweli kwamba Kiswahili sanifu kinazungumzwa Zanzibar na
kuahidi kutoa kila ushirikiano uanostahiki kufanikisha shughuli za Kamisheni
hiyo.
Ameongeza kuwa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa upande wake imechukua juhudi za makusudi
za kukiimarisha Kiswahili kufikia kiwango cha Kimataifa na tayari imeingizwa
kwenye mitaala ya vyuo vikuu kikiwemo Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA)
hadi kufikia kiwango cha Shahada ya Uzamifu.
Aidha, Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kuishukuru nchi za Jumuiya hiyo kwa namna ilivyojali na kushiriki
kikamilifu kuwasaidia wananchi wa Tanzania walioathirika kutokana na tetemeko
la ardhi lililotokea Septemba 10, 2016 huko Kagera na kueleza kuwa hatua hiyo
inathibitisha kuwa mashirikiano baina ya nchi wanachama wa Jumuiya hiyo
hayaishii kwenye mikataba laniki imeenda mbali zaidi kwa kujali ubinaadamu.
Akizungumzia suala
zima la changamoto ya ajira ambayo inaikabili nchi zote wanachama wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki, Dk. Shein alisema kuwa nchi hizo hazina budi kuondoka zilipo
ambapo mchango wa Pato la Taifa katika nchi hizo linakisiwa kuwa ni asilimia
8.9 ambayo ni kidogo kufikia lengo la asilimia 25 ambayo nchi hizo zimejiwekea
kufikia ifikapo mwaka 2032.
Dk. Shein alisema kuwa
Zanzibar ina hiostoria ya kuwa ni kitovu kikubwa cha biashara ambapo ilitumika
na wafanyabiashara pamoja na wavumbuzi waliokuwa wakisafiri katika ukanda wa
Afrika Mashariki, hivyo Serikali ya M apinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba
inaamini kwamba inaweza kurejesha hali yake hiyo ya zamani ambapo hivi sasa
imeamua kuimarisha miundombinu ya bandari, viwanja vya ndege na barabara ili
iweze kufikia azima yake hiyo.
Kutokana na hatua
hiyo, Dk. Shein aliwataka Wajumbe wa Bunge hilo kuwa tayari kushirikiana na
Serikali katika kuifanya Zanzibar kuwa kituo muhimu cha biashara katika ukanda
huo wa Afrika ya Mashariki na Kati.
Dk. Shein ameongeza
kuwa maendeleo ya viwanda pekee ndio yatakayowezesha kuondoa changamoto ya
ajira katika eneo hillo.
Nae Spika wa Baraza la
Wawakilishi la Zanzibar Zubeir Ali
Maulid akitoa hutuba yake alipongeza kwa kufanyika mkutano huo na kueleza kuwa
kufanyika mkutano huo si tu utaimarisha mashirikiano baina ya Mabunge hayo
mawili lakini pia, utatoa fursa zaidi ya pande mbili hizo kujifunza namna ya
kuendesha shughili za Bunge kutoka kila upande.
Mapema Katibu Mkuu wa
Bunge la Jumuiya ya Afrika ya Mashariki Daniel Fred Kidega alisisitiza suala la
amani na utulivu katika eneo la nchi zinazounda Jumuiya hiyo ili wananchi wake
waweze kuendelea na shughuli zao bila ya kuhofia kupoteza maisha yao.
Aidha, alitumia fursa hiyo kuisifu Zanzibar na kueleza kuwa kuna uwezekano mkubwa kuifanya Zanzibar kuwa eneo muhimu la biashara katika ukanda wa Afrika ya Mashariki na kueleza kuwa inaweza kuwa ni Dubai ya Afrika.
No comments:
Post a Comment