Sunday, October 9, 2016

TANZANIA KUENDELEZA KILIMO NA UTALII


Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango alipohotubia katika mkutano wa Benki ya Dunia, Jijini Washington DC, Marekani. 

Benny Mwaipaja, MoFP 
Washington DC, Marekani
8.10.2016
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amesema kuwa Serikali imedhamiria kuimarisha sekta ya kilimo na Utalii ili ziweze kutoa mchango mkubwa kuinua uchumi wa Taifa pamoja na kuwaondoa wananchi wake kutoka katika lindi la umasikini.

Waziri Mpango ameyasema hayo Jijini Washington DC, nchini Marekani, wakati akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Kanda ya Afrika, Louis Rene Peter Larose, ambapo viongozi hao wamezungumzia masuala yanayohusu utekelezaji wa miradi mbalimbali inayofadhiliwa na taasisi hiyo.

Amesema kuwa kilimo kinaajiri asilimia kubwa ya watanzania hivyo mapinduzi yanayokusudiwa katika sekta hiyo ni kuendesha kilimo biashara kwa kuongeza uzalishaji na  thamani ya mazao ya wakulima.

Kuhusu sekta ya Utalii, Dkt. Philip Mpango anayeongoza ujumbe wa wataalamu wa Uchumi na Fedha katika Mkutano wa Mwaka ulioandaliwa na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani, IMF, amesema kuwa serikali inakusudia kupitia upya kodi zinazoleta kero mbalimbali katika sekta hiyo pamoja kilimo.

Eneo jingine alilotaka Benki ya Dunia kuingilia kati, ni kuipatia Tanzania Mkopo na ruzuku utakaosaidia kukabiliana na madeni yake makubwa inayodaiwa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii pamoja madeni ya Shirika la Ugavi wa Umeme nchini, TANESCO, ili shirika hilo liweze kujiendesha kwa faida na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa haraka.

Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Kanda ya Afrika, Louis Rene Peter Larose, ameihakikishia Tanzania kuwa pamoja na miradi mingine, itafadhili mradi mkubwa wa kilimo wa ukanda wa kusini “Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania (SAGCOT)” ili kukifanya kilimo kuwa na tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

“Mimi nimefika Tanzania na ninaifananisha nchi hiyo kuwa itafikia ama kuzidi hadhi ya Dubai kutokana na rasilimali nyingi ilizonazo ambazo zikisimamiwa vizuri zitaibadili kabisa nchi hiyo kimaendeleo” alisema Larose.

Ameitaka Tanzania kutosita kuitumia ipasavyo benki hiyo kufanikisha malengo yake ya maendeleo na kwamba yeye mwenyewe binafsi pamoja na kwamba anaongoza kundi la nchi 22 za kiafrika katika Benki hiyo, atahakikisha Tanzania kama zilivyo nchi nyingine, inanufaika na uwepo wa Taasisi hiyo.

Mkurugenzi huyo Mtendaji amepongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli, namna anavyosimamia mambo kwa nguvu zake zote na ametoa pole kwa nchi hiyo kutokana na madhara iliyoyapata kufuatia tetemeko kubwa la ardhi lililoukumba mkoa wa Kagera na mikoa mingine jirani.


Ameahidi kuwa Benki hiyo itatuma wataalamu watakaosaidia kufanya utafiti na kuishauri nchi kitaalamu na kimiundombinu namna ya kukabiliana na majanga ya matetemeko pamoja na vifaa vitakavyosaidia kutoa tahadhari kabla ya kutokea kwa majanga kama hayo.

No comments:

Post a Comment