Thursday, October 13, 2016

WANAZUONI KUCHAMBUA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA SIKU YA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE


Mkuu wa Chuo cha Mwalimu Nyerere, Prof. Shadrack Mwakalila

Na May Simba-Maelezo
WANAZUONI nchini wanatarajia kukutana na kuchambua miiko na maadili ya viongozi wa Umma tarehe 14, Octoba mwaka huu kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 8: 00 mchana, katika ukumbi wa Chuo cha Kumbukumbu cha Mwalimu Nyerere (MNMA), ili kuenzi siku ya kumbukizi ya Mwalimu Julius Nyerere.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Chuo cha Mwalimu Nyerere Prof. Shadrack Mwakalila alipokuwa akiongea na waandishi wa habari leo, Jijini Dar es Salaam kuhusu kongamano la kumuenzi Mwalimu Nyerere.
Profesa Mwakalila amesema kuwa Chuo hicho kimeandaa Kongamano hilo ikiwa ni sehemu ya kumuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius   Nyerere ambaye aliamini kuwa kila nchi Duniani ina miiko yake na maadili inayowaongoza viongozi wa Umma.

“Chuo kimewaalika wanazuoni watano ambao ni Dkt Harun Kondo atakaye chambua Azimio la Arusha, aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mkama na Mzee Joseph Butiku watachambua Miiko ya uongozi pamoja na Ibrahim Kaduma na Mhe Philip Mangula watakaojadili maadili ya viongozi,” alisema Prof. Mwakalila.

Mbali na hayo Prof. Mwakalila amesema kuwa Miiko ya uongozi na maadili ya viongozi wa Umma ilisisitizwa na Mwalimu mara baada ya Uhuru na baadaye kusisitizwa zaidi katika Azimio la Arusha la mwaka 1967.
Vile vile Mwalimu Nyerere katika hotuba zake alikuwa akiwaasa viongozi wa Umma kuwa na maadili na kufuata miiko ya Uongozi ili kuwa mfano bora kwa jamii inayowazunguka.

Kongamano hilo linafanyika ikiwa ni maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 17 ya kifo cha Baba wa Taifa ambapo kauli mbiu ya kongamano hilo ni “Miiko ya uongozi na Azimio la Arusha”.

No comments:

Post a Comment