Mwimbaji na mtunzi mwenye sifa tele nchini Canada, Leonard Cohen, amefariki akiwa na umri wa miaka 82.
Alizaliwa huko Montreal na kuanza taaluma ya utunzi wa mashairi na kuandika riwaya, kabla ya kuwa sehemu ya waimbaji wa nyimbo za tamaduni mbalimbali miaka ya sitini.
Sauti yake ya ninga, utunzi wenye haiba na sifa, ulimpa umaarufu kote duniani, akifahamika kwa utunzi wa nyimbo kama vile Suzanne, I'm Your Man na Hallelujah, ambazo zilipendwa pakubwa kwa miaka mingi.
Alitoa albamu yake ya 14 kwa jina You Want It Darker, mwezi uliopita
Alijumuishwa kwenye orodha ya wanamuziki mashuhuri ya muziki wa Rock and Roll, Rock and Roll Hall of Fame, mwaka 2008.
"Hili ni tukio ambalo si la kawaida kwangu. Ni heshima ambayo niliitaka sana lakini sikuwahi kudhani ningepokea," alisema wakati huo.
Alizaliwa kwenye familia ya Kiyahudi lakini baadaye akawa mwanafunzi wa dini wa Ubuddha wa Zen.
Kwa miaka mitano, kuanzia 1994 hadi 1999, alichukua likizo kutoka kwenye muziki na akaishi katika kituo cha Zen cha Mount Baldy, mashariki mwa Los Angeles.
Baadaye, alirejelea uimbaji.
Wengi wamekuwa wakimuomboleza kwenye mitandao ya kijamii.
No comments:
Post a Comment