Saturday, December 10, 2016

MAKAMU WA RAIS WA JICA ATEMBELEA KITUO CHA KUPOZA NA KUSAMBAZA UMEME CHA ILALA-MCHIKICHINI JIJINI DAR ES SALAAM


Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Mhandisi Felchesmi Mramba, (kushoto),  akimwelezea jambo Makamu wa Rais wa Shirika la  Serikali ya Japan, linaloshughulikia uratibu wa misada ya maendeleo ya kimataifa, (JICA), Suzuki Noriko,  kuhusu hatua iliyofikiwa na TANESCO katika uboreshaji wa miundombinu ya kupoza na kusambaza umeme alipotembelea kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Ilala-Mchikichini jijini Dar es Salaam, ambapo JICA inashirikana na serikali katika kukiboresha kituo hicho.
Jengo jipya la kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Ilala-Mchikichini jijini Dar es Salaam, ambacho JICA imechangia ujenzi wake.

NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID
MAKAMU wa Rais wa Shirika la Serikali ya Japan linaloratibu Misada ya Maendeleo laKimataifa (JICA), Bw. Suzuki Noriko ametembelea kituo kipya cha kupoza na kusambaza umeme cha Ilala-Mchikichini kinachoendeshwa na Shirika la Umeme nchini Tanesco.

Ziara hiyo aliifanya Desemba 9, 2016 ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Mhandisi Felchesmi Mramba, alimtembeza kujionea hatua mbalimbali zilizofikiwa katika uboreshaji miundombinu ya TANESCO ikiwemo jingo na mitambo.

Ziara hiyo inakuja mwezi mmoja tu baada ya Waziri Mkuu wa Tanzania, Mh. Kassim Majaliwa, kuzindua kituo cha udhibiti na usimamizi wa mifumo ya usambazaji umeme katika jiji la Dar  es salaam kilichoko Mikocheni jijini Dar es Salaam ambapo kituo hicho cha Ilala, ni sehemu ya mradi wa uboreshaji miundombinu ya umeme kwenye jiji hilo.

JICA na mashirika mengine ya kimataifa yanafadhili mradi huo wa uboreshaji umeme jijini ambapo lengo ni kuwapatia wakazi wa jiji umeme ulio bora na wa uhakika zaidi, ambapo utekelezaji wa mradi huu umehusisha ujenzi wa kituo cha kupoza nguvu za umeme chenye ukubwa wa 100MVA (2X50MVA), 132/33KV cha City Centre, ujenzi wa mfumo wa njia ya usafirishaji umeme chini ya ardhi (Underground Transmission Line) na kwa kutumia minara (Overhead Line) ya msongo wa wa kilovolti 132 kutoka kituo cha Ilala hadi kituo cha City Centre umbali wa Kilomita 3.4, vile vile ujenzi wa mfumo wa njia ya usafirishaji umeme chini ya ardhi, (Underground Transmission Line) kutoka kituo cha Makumbusho hadi kituo cha City Centre umbali wa kilomita 6.67.

Mafundi wa TANESCO kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Japan, wakimalizia kazi ya kufunga mitambo kwenye kituo hicho cha Ilala.


Mhandisi Mramba akizungumza na mwakilishi wa JICA Tanzania Bi.Toshio Nagase.


Mhandisi Mramba, akiongoza ujumbe wa JAICA kutembelea kituo hicho.
Mhandisi Mramba akimshukuru bi Nagase baada ya kutembelea kituo hicho. Katikati ni Meneja Mwandamizi wa TANESCO kanda ya Dar es Salaam na Pwani Mhandisi, Mahende Mgaya.
Wataalamu wa mitambo ya umeme kutoka Japan, wakijadliana.

PSPF WATOA RAI KWA WAJASIRIAMALI KUJIUNGA NA MPANGO WA HIARI

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Bw. Charles Mwijage akisikiliza maelekezo kuhusu usajili wa wajasiriamali katika fao la hiari kutoka kwa Afisa Uendeshaji wa Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF) Bw. Hadji Jamadar wakati wa hafla ya ufunguzi wa maonesho ya kwanza ya Viwanda vya Tanzania  katika viwanja vya Mwalimu Nyerere Sabasaba leo Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tan Trade) Bw. Edwin Rutageruka. (Picha zote na Frank Shija – Maelezo)
Afisa Uendeshaji wa Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF) Bw. Hadji Jamadar akielezea jambo kwa wateja waliotembelea banda la mfuko huo katika maonesho ya Viwanda yanayoendelea katika viwanja vya Sabasaba Jijini Dar es Salaam.

Na Jacquiline Mrisho 
MFUKO wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF) umetoa rai kwa wajasiriamali kujiunga na mpango wa uchangiaji wa hiari ili kuweza kupata huduma ya hifadhi ya jamii.

Rai hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Afisa Uendeshaji wa mfuko huo, Hadji Jamadary wakati wa uzinduzi wa maonesho ya kwanza ya viwanda vya Tanzania uliofanyika katika viwanja vya sabasaba jijini humo.

Jamadary amesema kuwa mpango huo utawawezesha wananchi wasio na ajira rasmi kupata fursa ya huduma ya hifadhi ya jamii kama wapatavyo wanachama wenye ajira rasmi  pia unawawezesha wanachama walio katika mfuko huo kuweza kujiwekea akiba ya ziada.

“Mpango huu wa hiari ni mfuko ulio huru ambao unamruhusu mwananchi yoyote mwenye umri kuanzia miaka 18, mwenye uraia wowote hata kama anafanya kazi ndani au nje ya nchi, hivyo tunawaomba wananchi wote kuchangamkia fursa hii kwa manufaa ya maisha yao ya baadae,”alisema Jamadary.

Ameongeza kuwa hadi sasa mfuko una jumla ya wananchi 98,733 ambao tayari wamejiunga na mfuko huo lakini kwa kutambua umuhimu wa mfuko huo zaidi ya wananchi 102 wameshajiunga wakati maonyesho hayo yanayotarajiwa kumalizika mnamo Disemba 11 mwaka huu yakiendelea.

Aidha, Afisa huyo ametaja jumla ya mafao 6 yaliyopo katika mfuko huo yakiwemo ya elimu, ujasiriamali, uzee, kifo, ugonjwa au ulemavu, matibabu na fao la kujitoa pia mfuko huo unatoa fursa kwa mwanachama kukopa nyumba na viwanja.

Kuhusiana na fao la matibabu, Jamadary amefafanua  kuwa mwanachama atapatiwa bima ya afya yenye gharama ya shilingi 76,800 kwa mwaka mzima pia ataruhusiwa kuwaingiza wategemezi watano ambapo kila mmoja atalipiwa kiasi hicho cha fedha kwa mwaka mmoja.


Mpango wa hiari umeanzishwa mwaka 2013 ukiwa na lengo la kupanua wigo wa uanachama kwa kuandikisha wananchi waliojiajiri au kuajiriwa  katika sekta rasmi au isiyo rasmi.

No comments:

Post a Comment