Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Mto Nile ni miongoni mwa mito mikubwa iliyopo upande wa Mashariki ya Bara la Afrika naDuniani kote ukiwa na urefu wa kilomita 6,695 ambapo beseni ya Nile hukusanya maji ya eneo linalojumuisha 10% za eneo la Afrika yote.
Kwa
muonekano wa juu Mto Nile unaonekana kama pembetatu wakati upande wa
chini wa eneo la Nile (Kaskazini) na upande wa juu (Kusini) kuna mimea
mbalimbali inayoota kwa wingi pia katika kipindi cha mwisho wa mwaka
eneo la mto Nile huwa linakuwa na mwonekano mwekundu na kuwa na maua
yanayojulikana kama lotus flowers.
Japokuwa
mimea hii haioti kwa wingi wakati huu kama ilivyokuwa hapo awali, mimea
inayoota kwa wingi katika eneo la Mto Nile kwa upande wa chini ni yale
yanayojulikana kama Egyptian lotus na kwa upande wa juu hujawa na mimea
inayoitwa Cyperus papyrus.
Chemchemi
za Nile ni mito yote inayopeleka maji kwenda Ziwa Viktoria katika nchi
za Tanzania, Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uganda
na Kenya na kwa upande mwingine wa Nile unaanzia Ethiopia ukiitwa Abbai
au Nile ya Buluu unatoka katika Ziwa Tana wakati chanzo cha mbali kabisa
ni mto wa Luvironza huko Burundi unaoingia katika mto wa Kagera na
kufika Ziwa Viktoria.
Mto
huo ambao unaanzia Ziwa Victoria nchini Tanzania, ni chanzo kikubwa
cha maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, viwandani, kilimo cha
umwagiliaji na kuzalisha umeme kwa wakazi wa nchi za bonde hilo.
Kutokana
na nchi nyingi kuzungukwa na mto Nile, suala la ushirikiano katika
kusimamia na kuendeleza rasilimali za Bonde la Mto huo limepewa
kipaumbele ili kuzuia migogoro inayoweza kuzuka baina ya nchi ambazo
wanatumia mto huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi inayosimamia shughuli za wanachama wa Bonde la Mto Nile (NBI), Innocent Ntabana anasema kuwa azma
ya kusimamia na kuendeleza rasilimali za Bonde la Mto Nile limepewa
kipaumbele na nchi zote zinazozungukwa na mto huo, jambo hilo ndilo
limesababisha kuanzishwa kwa Sekretarieti ya NBI mwaka 1999 jijini Dar
es Salaam.
“NBI
ina jukumu la kusimamia na kuendeleza rasilimali za maji za Bonde la
Mto Nile kwa niaba ya nchi wanachama zipatazo 10 ambazo ni Tanzania,
Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Ethiopia, Sudan, Sudan ya Kusini,
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Misri,” anasema Ntabana.
Kwa upande wa Mratibu
wa Kanda wa Kitengo cha Uratibu cha Bonde la Mto Nile (NELSAP-CU),
Elicad Nyabeeya anasema kuwa mto huo una manufaa makubwa kwa nchi
wanachama kwani muunganiko wa nchi hizo umeleta mawasiliano mazuri
ambayo yanapelekea kuinua uchumi wa nchi hizo pia kwa upande mwingine
uwepo wa ushirikiano huo umesaidia nchi wanachama kufahamu tamaduni za
watu tofauti tofauti.
Nyabeeya
anakaririwa akisema kuwa “Nchi ya Tanzania inafaidika kutokana na
uwekezaji mkubwa uliofanywa na NBI kupitia utekelezaji wa miradi
mbalimbali ikiwemo miradi ya ujenzi wa bwawa la Bisrawi na usanifu wa
bwawa la Borenga, mkoani Mara”.
Kwa
mujibu wa Nyabeeya, nchi hii itanufaika na miradi ya maji na nishati ya
umeme, pamoja na miradi mingine mingi ambayo NBI inaendelea kuitekeleza
kama vile ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa Rusumo na umwagiliaji
katika mabonde ya mito Kagera na Ngono iliyopo mkoani Kagera.
Anaendelea
kufafanua kuwa mradi wa umeme wa Rusumo utazalisha megawati 80 za umeme
ambazo zitatumiwa na nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi ambapo
Tanzania inatarajiwa kupata megawati 16.
Miradi mingine ni ya kuunganisha umeme kutoka Ethiopia, Kenya hadi Tanzania, mradi wa umeme kati ya Tanzania na Zambia.
Aidha,
NBI wanatarajia kukamilisha upembuzi yakinifu wa kina wa miradi ya Mara
na Ngono ifikapo mwezi Aprili mwaka huu ambapo wananchi 20,000 pamoja
na hekari 13,630 katika vijiji 21 vinatarajiwa kunufaika na mradi wa
Ngono wakati Bonde la Mara litanufaisha wanachi 10,000. Miradi hiyo
itahusisha usambazaji wa maji kwa ajili ya matumizi ya majumbani, mifugo
na shughuli za umwagiliaji.
Wakati
huo, Bwawa la Borenga litakuwa likisambaza maji katika Bonde la Mara
kwa wakazi wa vijiji 13 kwa ajili ya umwagiliaji na 17 vitapata maji kwa
ajili ya matumizi ya nyumbani na mifugo.
Madhumuni
ya miradi hiyo ni kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa maji ya
uhakika, kuimarishwa kwa soko na mahusiano na kukuza sekta binafsi,
kilimo, usalama wa chakula na kupunguza umaskini.
Kutokana
na kuwepo kwa umuhimu wa rasilimali za Bonde la mto huo, iliamuliwa
kuwa Februari 22 ya kila mwaka iwe ni siku rasmi ya kuadhimisha
uanzishwaji wa muunganiko wa matumizi ya pamoja ya rasilimali za mto huo
baina ya nchi 10 wanachama .
Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali za Maji kutoka Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Sylvester Matemu amesema kuwa lengo
la Siku ya Nile ni kukuza uelewa kwa watu wote kuhusu umuhimu wa
ushirikiano baina ya nchi zote wanachama, masuala yanayotekelezwa na
faida inayopatikana kutokana na matumizi bora ya rasilimali za Bonde la
Mto huo.
“Maadhimisho
ya siku ya Nile kuadhimishwa katika nchi fulani ni tukio la kihistoria
kwasababu ni tukio ambalo halifanyiki katika nchi moja kila mwaka hivyo
kwa vile nchi wanachama tuko 10 basi linatokea mara moja kila baada
miaka 10,”anasema Mhandisi Matemu.
Maadhimisho ya 11 ya Siku ya Nile kwa mwaka huu yameadhimishwa nchini Tanzania kwa ushirikiano wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji pamoja na Sekretariati ya Nile Basin Initiative (NBI) ambapo
mgeni rasmi wa maadhimisho hayo alikuwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu
Hassan na kuhudhuriwa na watu zaidi ya 600 wakiwemo Mawaziri wa nchi
wanachama kutoka kwenye nchi husika,
mabalozi mbalimbali, wabunge, watu kutoka taasisi na mashirika
mbalimbali pamoja na wanafunzi wa shule za Msingi, Sekondari na Vyuo
Vikuu.
Shughuli
hizo zilianza kwa maandamano yaliyoongozwa na Bendi ya Polisi kuanzia
Viwanja vya Mnazi Mmoja hadi Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius
Nyerere ambako maonesho pamoja na ufunguzi rasmi wa maadhimisho hayo
vilifanyika.
No comments:
Post a Comment