Thursday, February 23, 2017

RAIS MSTAAFU ALI HASSAN MWINYI ASHIRIKI MAADHILISHO YA MIAKA 25 YA CSSC


 Rais Mstaafu Alhaji Ally Hassan Mwinyi akitembelea  mabanda mbalimbali katika maadhimisho ya miaka 25 ya Tume ya Kikristu ya Huduma za Jamii (CSSC) yaliyofikia kilele siku ya tar 22/02/2017 katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam
   Rais Mstaafu Mzee Mwingi akiwa katika Banda la Elimu la "Life Oriented Approach (LOA)" , njia ya ufundishaji wa Elimu ya awali, katika mradi unaotekelezwa na Kanisa Katoliki katika Majimbo ya Arusha na Same
 Mkuu wa Shirika la "Pressures Blood" Tanzania Padre Chesco Msanga, akimkabidhi zawadi ya picha Rais Mstaafu Mzee Mwinyi kama kumbukumbu alipoifungua Hospital ya St. Gaspar Itigi inayoendeshwa na shirika hilo
 Mzee Mwinyi akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Tume ya Kikristu ya Huduma za Jamii (CSSC)
 Rais Mstaafu Alhaji Ally Hassan Mwinyi akitoa hotuba yake katika siku ya kilele ya kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 25 tangia kuanzishwa kwa Tume ya Kikristu ya Huduma za Jamii Tanzania
Mzee Mwinyi akitoa Cheti kwa  Profesa Costa Mahalu, moja ya watu waliyotoa msaada mkubwa wa masuala ya Sheria kipindi Tume hiyo ilipokuwa inaanzishwa


Rais Mstaafu wa Serikali ya awamu ya pili, Alhaji Alli Hassan Mwinyi, ameipongeza Tume ya Kikristu ya Huduma za Jamii (CSSC) kwa kutimiza miaka 25 tangu ilipoanzishwa mwaka 1992.  Akiongea katika maadhimisho hayo, Mzee Mwinyi amesema kuwa Serikali imekuwa ikitambua na kuthamini mchango wa makanisa na Taasisi za dini katika kuboresha huduma za Jamii.

“Nimefarijika sana kwa kupata taarifa kuwa hadi kufikia Septemba 2016, hospitali za Kanisa 87 na vituo vya afya 45, vimeingia Mkataba na Serikali katika kutoa huduma za afya”, alisema Rais Mstaafu Mwinyi.

Katika hatua nyingine, Mzee Mwinyi aliongeza kuwa kwa upande wake yeye amekuwa mstari wa mbele kwa kuwaasa ndugu jamaa na marafiki zake na Watanzania wote kwa ujumla, kutumia huduma zitolewazo na hospitali za kanisa kwa kuwa wanatoa huduma bora, kwa kuzingatia upendo
“ Ikiwa mnaona kazi zinawazidia na mnafikia sehemu mnanung’unika kwa kuzidiwa na kazi nyingi, basi ningesema mgomvi wenu ni mie. Maana nawaambia ndugu na Watanzania wenzangu, kuwa huduma nzuri za afya zinapatikana katika hospitali za Kanisa, kwa kuwa unahudumiwa kwa upendo pamoja na tabasamu,” aliongeza Rais Mstaafu, Mwinyi.

Rais Mstaafu Mwinyi alimuomba Rais wa Tume aendelee kupanua na kuboresha huduma za jamii, kwa utaalamu na ubunifu huku akiwaasa watumishi wa sekta hiyo, kutofanya kazi kwa mazoea.  Aliongeza kuwa uamuzi wa kuanzisha Tume hiyo ulikuwa ni wa busara sana kwa manufaa ya Watanzania walio wengi.

Mheshimiwa Rais Mstaafu pia aliongezea kuwa Tume imefanya kazi kubwa ya kutekeleza majukumu na malengo yake, kwani kwa taarifa alizo nazo ni kuwa katika sekta ya elimu, idadi ya shule za makanisa imeongezeka  kutoka 350 mwaka 1997, na kufikia takribani 1000 mwaka 2016, wakati katika Afya kutoka idadi ya taasisi za afya 500 mpaka 900 kwa sasa.  Alipongeza kwa mafanikio haya makubwa yaliyopatikana ndani ya miaka hii 25 ya utendaji wa Tume.

Katika hatua nyingine, ameiomba Tume kuendelea kushirikiana kwa ukaribu na Serikali katika kuboresha uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali kwani ni chache na zinahitajika kutumiwa na Watanzania wengi wenye uhitaji pia.

Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii (CSSC) ni chombo kilichoundwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) mwaka 1992 kwa dhumuni la kuratibu na kusimamia huduma za kijamii zitolewazo na Taasisi za Makanisa husika za Elimu na Afya nchini.

No comments:

Post a Comment