Thursday, February 23, 2017

Rais Magufuli awapongeza madaktari Muhimbili na amsaidia Neema Mwita Wambura aliyeunguzwa moto kifuani


 Dada Neema Mwita Wambura (32) akizungunza na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kupitia njia ya Simu akimshukuru kwa msaada aliompatia wa kufanyiwa tena uchunguzi wa afya yake katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Pia Rais Dkt. Magufuli ameahidi kumpatia hifadhi mama huyo pamoja na watoto wake watatu ambao kwa sasa wapo Bunda mkoani Mara. Pia Rais Dkt. Magufuli alimpatia msaada Dada huyo kiasi cha Shilingi laki tano.  Dada Neema Mwita Wambura aliungua vibaya mara baada ya kumwagiwa uji wa moto uliokuwa unachemka jikoni na mume wake katika kijiji cha Kyagata, Tarime mkoani Mara.
 Mama Mjane Mariam Amir ( Bibi Mwaija ) ambaye amempa hifadhi Neema Mwita Wambura nyumbani kwake Tandika Davis Corner akiomba dua kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kupitia njia ya Simu kumshukuru mara baada ya kuzungumza naye kuhusiana na kumsaidia Dada Neema Mwita Wambura (32). Rais Dkt. Magufuli amempongeza Mama huyo Mjane ambaye ameonesha moyo wa kizalendo na kumpa hifadhi Dada huyo aliyemwagiwa uji wa moto na mumewe katika kijiji cha Kyagata, Tarime mkoani Mara. Pia Rais Dkt. Magufuli alimpa Mjane huyo kiasi cha Shilingi laki tano.
  Dada Neema Mwita Wambura (32) wakwanza kulia akiwa pamoja na Mama Mjane Mariam Amir ( Bibi Mwaija ) wakiwa ndani ya gari mara baada Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kumsaidaia ili aweze kufanyiwa tena uchunguzi wa afya yake katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam.
 Wauguzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wakimpokea Dada Neema Mwita Wambura (32) na kuanza mara moja kumfanyia tena uchunguzi wa afya yake katika majeraha aliyoyapata mara baada ya kumwagiwa uji wa moto uliokuwa ukichemka jikoni  kitendo kilichofanywa na mume wake.
 Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Profesa Lawrence Museru akimjulia hali Dada Neema Mwita Wambura (32) mara baada ya kufikishwa tena hospitalini hapo. Dada Neema Mwita alifanyiwa upasuaji mara nne katika siku za nyuma hospitalini hapo Muhimbili ili kutibu majeraha yake hayo ya moto.
 Daktari Bingwa wa magonjwa ya dharura na Ajali katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dkt. Juma Mfinanga akizungumza kuhusu hali ya mgonjwa Dada Neema Mwita Wambura (32) aliyefikishwa tena katika Hospitalini hapo kwa ajili ya uchunguzi wa Afya yake.
 Dada Neema Mwita Wambura (32) akiwa katika hali ya majonzi kufatia majeraha makubwa mwilini mwake kufatia kumwagiwa uji wa moto na mume wake mkoani Mara.
Daktari Bingwa wa upasuaji wa ngozi kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili  Dkt. Ibrahim Mkoma akizungumzia historia ya mgonjwa huyo ambaye yeye pamoja na jopo la madaktari bingwa walimfanyia upasuaji ili kutibu majeraha yake ya ngozi katika kipindi cha nyuma. PICHA NA IKULU.

 
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewapongeza Madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa juhudi kubwa walizofanya kunusuru maisha ya Neema Mwita Wambura ambaye alijeruhiwa kwa kuunguzwa na maji ya moto kifuani, shingoni na mkononi. 

Pongezi hizo za Mhe. Dkt. Magufuli zimetolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Bw. Gerson Msigwa muda mfupi baada ya kumfikisha Neema Mwita Waitara katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako Rais Magufuli ameagiza apelekwe kwa mara nyingine kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa maendeleo ya afya yake. 

Katika Pongezi hizo Mhe. Dkt. Magufuli amesema Madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili wamefanya kazi kubwa na ya kizalendo kuhakikisha Neema anapona licha ya majeraha makubwa aliyoyapata miaka miwili iliyopita na ambayo yalitishia uhai wake. 

Pia Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mama Mariam Amir (Bibi Mwanja) kwa upendo wake wa kumchukua Neema na kisha kumpa hifadhi nyumbani kwake huko Tandika Devis Kona Jijini Dar es Salaam. 

“Nakushukuru sana Mama na ninakupongeza, umeonesha mfano mzuri wa kujali umoja na upendo kwa Watanzania wenzako bila kujali dini, kabila wale kanda unayotoka na hivi ndivyo Watanzania wote tunapaswa kufanya” amesema Mhe. Rais Magufuli. 

Kabla ya kutoa pongezi hizo, mapema leo asubuhi Mhe. Rais Magufuli amewatuma wasaidizi wake wakiongozwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Bw. Gerson Msigwa kwenda Tandika Devis Kona katika Wilaya ya Temeke Jijini Dar es Salaam kumuona Neema Mwita Wambura ambaye alipatiwa hifadhi katika nyumba ya Mama Mjane aitwaye Mariam Amir (Bibi Mwanja) baada ya kuona picha na kusoma taarifa za mkasa uliomkuta katika mitandao ya kijamii. 

Mhe. Rais Magufuli ametoa Shilingi laki 5 kwa Neema kwa ajili ya kumsaidia chakula yeye na watoto wake waliohifadhiwa na rafiki yake huko Bunda Mkoani Mara na pia ametoa Shilingi laki 5 kwa Mariam Amir aliyejitolea kumsaidia na kumpa hifadhi nyumbani kwake. Pia ameahidi kumsaidia wakati wote wa matibabu na pia familia yake. 

Baada ya kumpokea daktari bingwa wa magonjwa ya dharula na ajali katika kitengo cha dharula cha Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Juma Mfinanga amesema wameanza kumfanyia uchunguzi ili kujua maendeleo yake na kama kumpa matibabu zaidi. 

Nae Daktari Bingwa wa Upasuaji Dkt. Ibrahim Mkoma ambaye amekuwa akimfanyia matibabu Neema Mwita Wambura tangu Julai 2015 alipofikishwa hospitalini hapo kwa mara ya kwanza amesema Neema anaendelea vizuri baada ya kufanyiwa upasuaji mara nne. 

Dkt. Mkoma amesema baada ya upasuaji huo, sasa Neema anaweza kuinua na kugeuza shingo yake na kwamba kwa sasa wataendelea kumfanyia uchunguzi zaidi ili kujua maendeleo yake. Mhe. Rais Magufuli ameagiza vyombo vyote vinavyohusika kufanyia kazi mkasa uliomkuta Neema Mwita Wambura na kuhakikisha haki inatendeka.

No comments:

Post a Comment