Mkuu wa utumishi Jeshi la Wananchi Tanazania (JWTZ), Meja Jenerali Harrison Masebo amekanusha taarifa zinazoenea mitandaoni kuhusu kutangazwa kwa nafasi za ajira na kwamba watu wanaotangaza hivyo ni matapeli waepukwe.
Meja Jenerali Masebo amebainisha hayo baada ya kuenea uvumi mitandaoni na mitaani kwa baadhi ya watu kujifanya wanahusika na jeshi hilo katika idara ya kutoa ajira kwa wananchi.
"Kumekuwa na vikundi ama watu ambao kwa namna moja ama nyingine wamekuwa wakijitangaza wao wanauwezo kutoa ajira, vikundi hivyo msivisikilize siyo vikundi rasmi ama watu hao siyo rasmi kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi nasema kuanzia leo mtu akisiikia kuna mtu anamfuata anamwambia kuna nafasi ya kujiunga na mafunzo ya JKT ajue huyo mtu siyo halali ni muongo na tapeli" -alisema Meja Jenerali Masebo.
Pamoja na Hayo Meja Jenerali Masebo amesema mara zote Jeshi limekuwa likitoa ufafanuzi kuhusiana na masuala ya ajira lakini wanashangazwa na kundi hilo namna wanavyofanya kutaka kupitia 'shortcut'.
"Jeshi limekuwa likifafanua mara kwa mara kuhusu taratibu za kujiunga nafasi za mafunzo JKT na taratibu za kujiunga na jeshi la wananchi lakini katika mazingira ambayo tunashindwa kuyaelewa hawa watu au vikundi ndiyo wamekuwa wajanja kiasi cha kuwarubuni vijana, wazazi na wazazi wakaamini kwamba zipo njia mbadala za kujiunga 'shortcut' napenda kusema hakuna shortcut hapa" - alisisitiza Meja Jenerali Masebo
Pamoja na hayo, Meja Jenerali Masebo aliendelea kufafanua baadhi ya mambo kwa kusema "Kwa vyombo vyote vya ulinzi na usalama hata wakiwa Uhamiaji, Zima moto, Magereza, Polisi, TANAPA na Jeshi lenyewe ukitaka kujiunga na Jeshi la Wananchi maana yake ni kwamba kuna utaratibu maalumu ambapo kwanza kuna kikao ambacho wenyekiti wa kikao hicho ni mimi Mkuu wa Utumishi Jeshini kwa hiyo vyombo vingine vya ulinzi na usalama vinaleta wawakilishi ambao ni maofisa watumishi tunakaa pamoja kila taasisi, wanaleta idadi ya watu wanaowahitaji" - Meja Jenerali Masebo aliongeza.
No comments:
Post a Comment