Thursday, May 31, 2012

Kiberenge chamuua mtu Morogoro





MKAZI wa Kijiji cha Munisagara, wilayani Kilosa, Patrick Maulid (80) amekufa baada ya kugongwa na kiberenge akiwa anatembea katikati ya reli.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Adolfina Chialo alisema kuwa ajali hiyo ilitokea wilayani Kilosa. Inasadikiwa Maulid alikuwa amelewa pombe.


Kwa mujibu wa Kamanda, mzee huyo aligongwa juzi saa 10:30 alasiri na kiberenge chenye namba za usajili HDT/Group 2 kilichokuwa kinaendeshwa na Salum Kasisila (38) mkazi wa Munisagara.


Alifariki dunia alipokuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa. Alisema kiberenge hicho kilikuwa kikitoka Stesheni ndogo ya Kidete kwenda katika Stesheni ya Kilosa mjini kabla ya kumgonga mzee huyo aliyekuwa akitembea katikati ya reli.


Wakati huo huo, mkazi wa Kijiji cha Mwidu, Tarafa ya Mikese wilayani Morogoro, Ramadhani Almasi (70) amekufa papo hapo baada ya kugongwa na basi la Saibaba wakati akivuka barabara katika Kijiji cha Maseyu, mkoani hapa.


Kamanda alitaja basi lililohusika kuwa ni Saibaba lenye namba za usajili T779BKC aina ya Scania likiendeshwa na Emmanuel Athuman (32) mkazi wa Tabata, Dar es Salaam.


Alisema Almasi aligongwa juzi saa 1 usiku katika Kijiji cha Maseyu-Gwata, kwenye barabara kuu ya Morogoro-Dar es Salaam. Basi hilo lilikuwa likitoka Mwanza kwenda Dar es Salaam.


Kwa mujibu wa kamanda, mzee huyo aligongwa na basi hilo wakati akivuka barabara. Alisema uchunguzi unaendelea ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya dereva.

No comments:

Post a Comment