Thursday, May 31, 2012

Vitambulisho vya Taifa ni lazima







MTENDAJI Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu amesema ni kosa kwa Mtanzania kukataa kitambulisho cha Taifa na ikitokea, atashitakiwa na ataweza kufungwa kwa mujibu wa sheria.

Maimu alisema hayo jana alipokuwa akijibu maswali ya wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ulinzi, Usalama na Mambo ya Nje, waliotembelea Mamlaka hiyo.


Alijibu swali la mjumbe wa Kamati hiyo, Seif Mohamed Khatib aliyehoji kama Zanzibar kwa vuguvugu lililopo, atatokea mtu akakataa kitambulisho hicho cha Taifa ni hatua gani zitachukuliwa.


Mbali na kushitakiwa, Maimu alisema Mtanzania huyo atapata wakati mgumu kupata huduma zikiwamo za kibenki kwani kitambulisho hicho ndicho kitakachotumika sehemu mbalimbali hata Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na huduma zingine.


Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Edward Lowassa aliitaka NIDA kuhakikisha haitoi vitambulisho kama njugu na kuifanya kazi hiyo nyepesi wakati ni jambo la thamani kwa Taifa.


Lowassa alisema wapo watu ambao si raia lakini watapenda wawe Watanzania ili waje kuipora nchi hii rasilimali zake na akataka NIDA iwe makini katika kutoa vitambulisho hivyo, hasa kwenye wilaya za mipakani.


“Tuwe makini mipakani, nchi zingine wanathamini sana uraia wa nchi zao, hivyo na ninyi fanyeni uraia wetu kitu cha thamani na mhakikishe anayepata kitambulisho hicho awe ni Mtanzania peke yake,” alisema Lowassa.


Akijibu hoja hiyo ya hadhari ya kutoa vitambulisho hivyo kwa watu wasio raia, Maimu aliwaomba wanasiasa waache kuingilia Mamlaka hiyo itakapoanza kuchukua hatua katika utambuzi wa raia na watu wasio raia.


“Tutakapoanza kuchukua hatua msije kutunyoshea vidole, naomba mtuache tutekeleze majukumu yetu,” alisema Maimu.


Alisema Mamlaka hiyo itakamilisha utoaji vitambulisho nchi nzima ndani ya miaka miwili na kuwa mwezi ujao wataanza usajili kwa wakazi wa Dar es Saalam baada ya kumaliza kutoa mafunzo kwa watendaji wa kata, mitaa na vijiji.


Waliokuwa mawaziri wa Mambo ya Ndani ambao ni wajumbe katika Kamati hiyo, walikiri kuwa mradi huo umechukua muda mrefu kukamilika kutokana na kugubikwa na fitina na watu wa kada mbalimbali kuutolea macho.


Mawaziri hao John Chiligati na Seif Khatib, walisema wakiwa mawaziri walikuta mradi ukiwa kwenye mpango wa wizara; lakini fitina zilijaa kwenye mradi huo.


Walidai kuwa fitina hizo zilitokana na mradi huo kuwa na fedha nyingi na kufanya macho ya wafanyabiashara hasa kampuni zilizokuwa zinashindana kupata zabuni, kupigania na wakati mwingine kufikishana mahakamani.


Walidai kutokana na mvutano mkubwa uliokuwapo wa nani apewe zabuni hizo, mradi huo ulishindwa kuanza kwa wakati kutokana na vikumbo vya kampuni hizo ambazo baadhi yao zilikimbilia mahakamani kulalamika kuwa hazikutendewa haki.


“Mimi niwashukuru kwa kupiga hatua hapa mlipofika, kwa kweli ni pazuri, mimi wakati wangu nilishindwa kwa vile mradi huu ulikuwa umejaa fitina nyingi mno,” alidai Khatib.


Kampuni ambayo sasa imepewa zabuni ya vitambulisho hivyo ni Iris-Corporation Behad na kampuni mshauri mwelekezi ni Gotham International Ltd (GIL). Chiligati aliuliza:


“Nikiwa Waziri nilishuhudia fitina nyingi sana kwenye mradi huu, hii ni kwa sababu una fedha nyingi, hivyo kila mfanyabiashara alitaka apate zabuni ya vitambulisho hivi.”


Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Abdallah alisema mradi huo uligubikwa na maneno na hatua ambayo umefikia ni jambo la kushukuru Mungu kuwa Watanzania wataanza kupata vitambulisho vyao hivi karibuni.

 
     

 

No comments:

Post a Comment