Mwanosa aliikataa taarifa hiyo mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika jengo hilo ambalo ujenzi wake ulianza Juni mwaka jana na mpaka sasa zaidi ya Sh milioni 28 zimetumika.
Awali akisoma taarifa ya ujenzi kwa niaba ya Ofisa Tarafa, Ofisa Mtendaji wa kata ya Chimala alisema hadi kukamilika kwa ujenzi huo zaidi ya Sh milioni 31 zitatumika.
Mwanosa alipinga matumizi hayo ya fedha akisema kiasi kilichotumika ni kikubwa ikilinganishwa na kazi inayoonekana kufanyika, hivyo ipo haja ya wahusika wa ujenzi huo kutoa majibu yatakayoondoa hoja ya matumizi mabaya ya fedha zilizotengwa.
Alizitaja kasoro zinazoonekana katika jengo hilo pamoja na udogo wake ikilinganishwa na fedha zilizotengwa kuwa ni kuta kuanza kupasuka nyufa hata kabla ya ofisi kuanza kutumika, fremu za madirisha na milango kutokuwa na vigezo vinavyostahili kwa jengo kama hilo.
“Hata kwa hesabu ya kawaida mtu binafsi ukampa milioni 30 hawezi kujenga kajengo kama haka, lazima ataibuka na jengo kubwa, la kisasa na linalopendeza sasa mpaka leo zimetumika zaidi ya milioni 28 kwa jengo hili dogo namna hii. Hapa napata sababu ya kuwa na shaka kuwa huenda kuna mbinu chafu ya mtu kupitia ujenzi huu na yeye akawa anajenga kwake,” alisema.
Aliendelea kusema, “Tumepita pale Vwawa wilayani Mbozi kule tulizindua jengo pia la ofisa tarafa ambalo wametumia fedha kidogo sana mpaka kukamilisha pamoja na samani za ndani. Linapendeza na kweli ukiona unaridhika kuwa kazi imefanyika sasa iweje ninyi mtumie fedha zote hizo kwa jengo kama hili na bado halijakamilika,” alihoji.
Aliuagiza uongozi wa halmashauri ya wilaya hiyo kujipanga upya kwa kuhakikisha mkandarasi aliyehusika na ujenzi wa jengo hilo anarudia kazi yake vinginevyo hatua zaidi za ufuatiliaji zitachukuliwa.
Aliwaasa viongozi kuwa makini katika ufuatiliaji wa maendeleo ya miradi mbalimbali kwenye maeneo yao badala ya kubaki ofisini na kusababisha Serikali iendelee kupakwa matope kutokana na miradi kutoendana na fedha zinazotumika.
No comments:
Post a Comment