Wednesday, May 23, 2012

Waomba kujengewa uzio, kukwepa adha ya kinyesi




UONGOZI wa Shule ya Mto Pepo iliyopo katika Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, umewaomba wafadhili kujitokeza kusaidia ujenzi wa uzio utakaolinda mazingira ya shule hiyo baada ya baadhi ya watu kupaka kinyesi katika kuta za shule hiyo.

Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Saada Rajab Ali alisema hayo wakati alipozungumza na waandishi wa habari waliotembelea shule hiyo kujua maendeleo ya elimu.

Alisema moja ya tatizo lililokuwa likileta usumbufu mkubwa kwa wanafunzi ni kukosekana kwa uzio ambao hulinda mazingira ya shule hiyo.

“Tunahitaji uzio wa shule ambao utasaidia kuimarisha ulinzi na kuepuka watu kuiba viti na
meza za shule,” alisema Saada.

Aliiomba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuwapatia mlinzi atakayesaidia kuweka
ulinzi wa shule hiyo ili kuokoa mali za shule.

Awali alisema Shule ya Mto Pepo kwa sasa inakabiliwa na tatizo la ukosefu wa walimu wa
masomo ya sayansi na hivyo kurudisha nyuma juhudi za wanafunzi kufaulu vizuri masomo
hayo.

“Tunakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa walimu wa masomo ya sayansi ikiwemo Fizikia,
Kemia pamoja na Baiolojia,” alisema.

Alisema kwa sasa shule imechukua juhudi za kutafuta walimu waliomaliza masomo ya kidato cha sita ambao hawajaajiriwa kusomesha wanafunzi.

Hivi karibuni Shule ya Mto Pepo ilifanikiwa kufaulisha zaidi ya wanafunzi 35 kwenda kidato
cha kwanza kwa ajili ya masomo ya sekondari.

Kwa mujibu wa maelezo ya Mwalimu Saada, mafanikio hayo yamepatikana kutokana na
ushirikiano mzuri kati ya walimu na wazazi wa shule hiyo.

No comments:

Post a Comment