Wednesday, May 23, 2012

Zanzibar kujenga bandari mpya


Image
Bandari ya Malindi ya Malindi Zanzibar




SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imeazimia kujenga Bandari mpya iliyopo Kwa Mpiga Duri baada ya Bandari ya sasa ya Malindi kuzidiwa na msongamano wa mizigo.

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Miundombinu, Issa Haji Ussi amesema hayo wakati alipofanya ziara kutembelea Bandari ya Malindi na kujionea msongamano wa mizigo ikiwemo makontena ambayo huzorotesha ufanisi wa kazi.


Akizungumza na uongozi wa Shirika la Bandari ya Malindi, Issa alisema kujaa huko kwa mizigo kwa kiasi kikubwa kumefanya kazi za kushusha mizigo kuzorota na kulikosesha taifa mapato mengi yanayotegemwa kupitia bandari.


“Nia ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kujenga bandari nyingine huko Kwa Mpiga Duri baada ya Bandari ya Malindi kuzidiwa na wingi wa mizigo ikiwemo makontena,” alisema Issa.


Awali Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Bandari la Zanzibar, Abdi Omar alisema makontena

yamekuwa mengi na kusababisha kazi katika bandari hiyo kuzorota.

Abdi alitoa mfano wa bandari ya Malindi ambayo kwa sasa yapo zaidi ya makontena 11,220 yaliyohifadhiwa yaliyofanya eneo kubwa la bandari hiyo kukaa makontena hayo.


Abdi aliwataka wamiliki wa makontena hayo kukamilisha taratibu za kuyachukua katika bandari hiyo na kuonya kuwa vinginevyo shirika litatumia sheria za kuyaondoa.


“Zipo sheria za Shirika la Bandari ambazo zinataka wamiliki wa mizigo kufanya utaratibu wa

kuyaondoa katika wakati muafaka au yataondolewa kwa mujibu wa Sheria,” alisema Abdi.

Mchakato unaofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa sasa ni kutafuta wafadhili

watakaogharimia mradi huo wa ujenzi wa bandari hiyo mpya itakayokuwa na urefu wa kilometa tano.

No comments:

Post a Comment