Tuesday, May 22, 2012

Nato kukabidhi jukumu la ulinzi Afghanstan 2013

Jumuiya ya kujihami ya NATO imesema kuwa itakabidhi jukumu la ulinzi wa Afghanistan kwa nchi hiyo katikati ya 2013 pamoja na kutangaza kuanza mfumo wake mpya wa kinga ya makombora barani Ulaya utakaokamilika 2020.

Kutangazwa kwa hatua hiyo kumezusha hali ya kutoelewana baina ya NATO na Urusi ambayo imeendelea kusisitiza ipatiwe uhakika wa kisheria unaothibitisha kuwa mpango huo hauilengi nchi hiyo. Marekani yenyewe imeweka bayana shabaha yake katika mpango huo ni kuwa ni kujilinda dhidi ya Iran.

Akizungumza baada ya kutangazwa rasmi kwa mpango huo kwenye mkutano wa kilele wa jumuiya hiyo unaoendelea mjini Chicago Marekani, Katibu Mkuu wa NATO Anders Fogh Rasmussen amesema kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa Urusi haina haja ya kuhofia hatua hiyo.

Baadae Rasmussen aliwaambia waandishi wa habari kwamba jumuiya hiyo ina lengo la kuendelea na mazungumzo na Urusi ikiwa na matumaini kuwa nchi hiyo itaielewa hatua yake hiyo kuwa ni sehemu ya mpango wake muhimu na wa muda mrefu katika kujihami na makombora

Mapema siku ya Jumapili Naibu Waziri wa Ulinzi wa Urusi Anatoly Antonov aliionya NATO kuhusu hatua hiyo ya kuendelea na mpango wake wa kutengeneza mfumo mpya wa kujikinga na makombora kwa nchi za ulaya akisema kitendo hicho kitavuruga amani ya dunia. Antonov alitishia pia kuwa nchi yake itachukua hatua za kijeshi kama mpango huo utaendelezwa.

No comments:

Post a Comment