Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe
Mazoezi hayo yanayoonekana kufanywa kwa udharura, yameleta wasiwasi mkubwa kwa wananchi kutokana na vishindo vikubwa vilivyo kuwa vikisikika mithili ya radi huku mingurumo ya vifaru ikisikika kwa nguvu.
Wakati mazoezi hayo yakifanyika, mvua ilikuwa ikinyesha na umeme katika makazi ya watu ulikatika na kuzidi kusababisha hofu kubwa.
Askari wa kambi hiyo walifanya mazoezi ya kushitukiza usiku wa kuamkia jana ikiwa ni pamoja na kuzijaribu zana zao nzito kama vile mabomu na mizinga ya kurushwa kwa vifaru huku ikitoa milio mizito.
Vishindo hivyo vya majaribio ya silaha hizo nzito vilisababisha wananchi wanaoishi jirani na kambi hiyo wakiwemo wa Kiluvya, Kibamba na maeneo ya Mbezi, kupatwa na taharuki huku wakikumbushwa milipuko ya mabomu ya kambi za Mbagala na Gongo la Mboto yaliyosababisha vifo vya watu wengi na uharibifu mkubwa wa mali.
Wakazi wengi wa maeneo hayo walilazimika kutoka nje ya nyumba zao na familia zao huku wakiwa hawajui hatma yao huku wengine wakizungumza kwa tahadhari wakiwa wamefunga nyumba zao na kukaa maeneo ya wazi huku wakifanya mawasiliano na ndugu zao walio nje ya maeneo hayo.
Akizungumza na gazeti hili jana, Msemaji wa JWTZ , Kanali Kapambala Mgawe, alisema mazoezi hayo ni ya kawaida kabisa.
“Huwa yakifanyika tunatoa taarifa, haya ya jana taarifa zilitolewa kwa wananchi wale wa jirani sana lakini kwa kuwa mazoezi yenyewe yalifanyika usiku, kelele zilisikika mbali sana tofauti kama mazoezi yangefanyika mchana,” alisema.
Wasiwasi mkubwa uliwakumba wananchi kufuatia kauli za serikali bungeni dhidi ya chokochoko zinazofanywa na nchi jirani ya Malawi ya kugombea mpaka katika ziwa Nyasa.
Pamoja na serikali kusisitiza kuwa jeshi limejiandaa kwa lolote litakalotokea nchini Malawi, Kanali Mgawe alisema mazoezi hayo hayahusiani na chokochoko za Malawi.
Mwanzoni mwa wiki hii, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, aliionya Serikali ya Malawi juu ya utata wa mpaka uliopo katika Ziwa Nyasa kati ya Tanzania na nchi hiyo na kusisitiza kuwa Serikali ya Malawi hairuhusiwi kutumia eneo la mpaka unaogombaniwa hadi mwafaka utakapopatikana.
Alisema tatizo hilo ni la muda mrefu ambapo Malawi wanadai Ziwa lote Kaskazini ya Msumbiji kuelekea Ruvuma na Mbeya ni mali yao kwa mujibu wa Mkataba wa Heligoland uliowekwa saini Julai mwaka 1890.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, Edward Lowassa, naye alitoa msimamo wa kamati yake na kusisitiza kuwa JWTZ wako tayari kwa lolote ingawa aliomba Mungu kuepusha kutokea kwa vita na badala yake suala hilo liamuliwe kwa njia ya kidiplomasia.
Msimamo huo wa serikali umekuja baada Serikali ya Malawi kutoa kandarasi kwa kampuni kadhaa za kigeni zinazoendesha utafiti wa mafuta na gesi katika eneo la ziwa Nyasa linalogombaniwa na pande hizo mbili.
Ndege za kuangaza katika mipaka ya baharini zimeripotiwa kuzunguka mara kwa mara katika eneo la ziwa hilo kwa kile Tanzania inachokiita ukiukwaji wa makubaliano ya pande zote mbili.
Wakati Serikali ya Tanzania ikiweka tishio hilo, serikali ya Malawi kupitia Waziri wake wa Mambo ya Ndani na Usalama wa Ndani, Uladi Mussa alisema Watanzania hawana mamlaka ya kuzuia utafiti wa mafuta uliokuwa ukiendelea katika ziwa hilo na kwamba shinikizo la Tanzania likiendelea watalazimika kwenda katika mahakama ya kimataifa.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment