Sunday, August 12, 2012

Mzozo wa mpaka wajaza Wamalawi ubalozini Dar


Hofu  ya mzozo wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi, jana ulisababisha kundi kubwa la raia wa nchi ya Malawi wanaoishi Tanzania kujazana kwenye ofisi ya ubalozi wao uliopo barabara ya Rose Garden Mikocheni B jijini Dar es Salaam, baada ya kutumiwa ujumbe kuwa wanahitajika kuonana na balozi.

Raia hao walijazana ubalozini hapo tangu saa 3 asubuhi wakisubiri kuambiwa kile walichoitiwa na balozi wao.

Hata hivyo, raia hao baada ya kusubiri kwa muda mrefu bila kuambiwa lolote, mmoja wa maafisa wa ubalozi huo, aliwateuwa wawakilishi watatu ili kuweza kuzungumza na Balozi Flossie Chidyaonga.

Wawakilishi hao baada ya kukutana na Balozi Chidyaonga, walimfahamisha wameenda hapo ili kuitikia wito uliowataka kufika ubalozini ili kukutana naye, kutokana na taarifa zilizosambazwa kwa ujumbe wa simu kuwa Wamalawi wote waishio jijini Dar es Salaam, wanahitajika.



Lakini Balozi Chidyaonga alisema taarifa hizo si za kweli, kwani hakuna afisa yeyote wa ubalozi aliyetumwa kutoa taarifa hiyo.

“Hapana taarifa hizo si sahihi, hakuna aliyetumwa kuwaita kufika hapa…nashangaa kuwaona mmejazana katika ofisi hii, naomba muwataarifu wenzenu balozi hajatoa taarifa hizo walizozisikia,” alisema Balozi Chidyaonga kwa lugha ya kinyasa.

Balozi huyo alisema, kama mwakilishi wa Rais wa Malawi, Joyce Banda, anafanya kazi kupitia taarifa toka kwa bosi wake huyo, lakini mpaka sasa hajapewa taarifa zozote za kuitisha kikao cha kukutana na raia wake.

Hata hivyo, Balozi Chidyaonga alisema kutokana na taifa la Tanzania kuingia katika zoezi la Sensa kwa watu wake, aliwashauri raia wa Malawi waishio nchini kuhakikisha wanapata vibali vya kuishi katika nchi hii ili wasitibue hesabu za Watanzania.

“Naomba muwafahamishe na wenzenu, kama hawana vibali vya kuishi Tanzania waje hapa kujitambulisha kisha waende ofisi za Uhamiaji kule Posta kulipia dola 50 (sawa na Sh.80,000 za kitanzania), wawe na amani zaidi ya kuishi,” alisema balozi huyo.

Aidha, balozi huyo alisema Tanzania ni nchi nzuri yenye amani ambayo hakuna raia anayeulizwa utambulisho wake, labda anaweza kuulizwa hayo iwapo atafanya kosa litakalomfikisha kwenye vyombo husika.

Hivi sasa raia wa Malawi waishio nchini, wameingiwa na woga kutokana na utata wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi ambapo kuna utata kuhusu mpaka katika Ziwa Nyasa  huku kila upande ukidai ni mali yake.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment