Sunday, June 17, 2012

Al-Shabaab wadai kuhusika na mashambulizi ya Afgoye

Mshambuliaji wa kujitoa muhanga nchini Somalia amejiripua kwenye kituo cha ukaguzi wa barabarani hivi leo, na kusababisha maafa makubwa, kwa mujibu wa polisi na mashahidi.

 Kundi la kigaidi la Al-Shabaab limedai kuhusika na mashambulizi hayo ambalo liliwalenga wanajeshi wa serikali ya Mpito ya Somalia mjini Agfoye, umbali wa kilomita 30 kaskazini magharibi mwa mji mkuu, Mogadishu.


 Polisi imethibitisha kutokea kwa mashambulizi hayo, ingawa bado haijatowa idadi kamili ya waliouawa au kujeruhiwa. Afisa wa ngazi za juu wa kundi hilo, Abdi-Asis Abu Muskab amekiambia kituo chao cha redio kuwa wamefanikiwa kuwaua wanajeshi wengi wa serikali. Kwa mujibu wa Abu Muskab, mshambuliaji wao wa kujitoa muhanga aliliingiza gari lenye miripuko katika jengo la skuli ya Afgoye, ambako majeshi ya serikali yameweka makaazi yake.

 Mashahidi wanaelezea kusikia mripuko mkubwa na kushuhudia moshi kutoka eneo hilo, ambalo baadaye lilizingirwa na vikosi vya serikali na vya Umoja wa Afrika. Mji huo, ambao ulikuwa ukitumiliwa na Al-Shabaab kama ngome yao ya kuushambulia mji wa Mogadishu, ulitwaliwa na majeshi ya serikali na Umoja wa Afrika mwezi uliopita.

No comments:

Post a Comment