UONGOZI
wa klabu ya Yanga umehofia panga la Shirikisho la Soka la Kimataifa
‘FIFA’ katika harakati zake za kutaka kuwatema wachezaji wake wawili wa
kimataifa Davis Mwape pamoja na Kenneth Asamoah ambao msimu uliopita
walishindwa kuonyesha cheche zao.
Woga huo wa viongozi ahao wa
Yanga umekuja mara baada kukumbuka msukosuko walioupata kutoka FIFA
baada ya kumtema beki John Njoroge wakati akiwa bado ana mkataba wa
kuitumika klabu hiyo na kushindwa kumlipa haki zake.
Hivi
karibuni mara baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu baadhi ya viongozi wa
Yanga walisikika wakisema kuwa watawatema Mwape na Asamoah kwenye
usajili wa msimu ujao kutokana na wachezaji hao kuonyesha kiwango cha
chini.
Akizungumza na Mwananchi jana Katibu Mkuu wa Yanga,
Celestine Mwesigwa alisema kuwa ndoto za kuvunja mkataba na wachezaji
hao hazipo na watandelea kuitumika hadi pale watakapokuwa wamemaliza
mikataba yao.
“Mwape na Asamoah bado ni wachezaji wetu na hatuna
mpango wa kuwatema kwa sababu bado tuna imani nao na wataendelea
kuitumika klabu yetu hadi watakapokuwa wamemaliza mikataba yao,” alisema
Mwesigwa.
Hata hivyo habari za uhakika kutoka ndani ya klabu
hiyo zinasema kuwa uongozi wa Yanga umeshindwa kufikia uamuzi huo wa
kukatisha mikataba ya wachezaji hao kutokana na kutokuwa na fedha za
kuwalipa kama ilivyokuwa kwa Njoroge ambaye hadi sasa hajalipwa madai
yake licha ya FIFA kuitaka Yanga kumlipa mchezaji huyo raia wa Kenya.
Mwape
na Asamoah wote kwa pamoja bado wana mkataba wa mwaka mmoja wa
kuitumikia Yanga ambayo msimu uliopita ilishika nafasi ya tatu na kukosa
nafasi ya kushiriki katika mashindano ya kimataifa.
Wakati huo
huo klabu ya Yanga imeweka bayana majina ya wagombea ambao
wamepitishwa kwa ajili ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika
klabu hiyo, mpaka jana mchana hakuna pingamizi lolote ambalo
limewasilishwa.
Kamati ya uchaguzi ya Yanga, juzi ilibandika
majina ya waliopitishwa kuwania kinyang’anyiro hicho ambacho uchaguzi
wake umepangwa kufanyika Julai 15 jijini Dar es Salaam.
Hata
hivyo kuna habari kuwa uchaguzi huo utafanyika kwenye ukumbi wa Diamond
Jubilee, huku taarifa za chini kwa chini zikidai kuwa wagombea Ally
Mayai ‘Tembele’ na Sara Ramadhani ni miongoni mwa watakaowekewa
pingamizi.
Mmoja wa wanachama wa Yanga alisema kuwa Tembele
watamuwekea pingamizi kwa madai kuwa alijiuzuru kwenye uongozi uliopita
kabla ya kumaliza muda wake huku Sara wakimtuhumu kwa masuala mbali
mbali.
Katibu wa kamati ya uchaguzi, Francis Kaswahili alisema
kuwa mpaka jana mchana hawajapokea pingamizi lolote na ameonya wanachama
kutowasilisha mapingamizi feki kwa sababu ya chuki binafsi na
atakayebainika kufanya hivyo atatozwa faini ya Sh500,000 sambamba na
kufungiwa kwa miaka miwili kujihusisha na masuala ya soka. |
|
No comments:
Post a Comment