Wednesday, June 27, 2012

Mahakama: Makunga apewe maelezo

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeamuru upande wa mashtaka kumpa  aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Theophil Makunga na wenzake wawili maelezo ya malalamikaji ili waweze kufahamu zaidi kuhusu kesi yao.  Makunga anakabiliwa na shtaka  la kuchapisha makala ya  kuwashawishi askari na maofisa wa majeshi nchini kuacha kuitii Serikali. Uamuzi huo  ulitolewa jana na Hakimu Mkazi, Waliarwande Lema baada ya Wakili Mwandamizi wa Serikali, Elizabeth Kaganda kumaliza kuwasomea maelezo ya awali washtakiwa.  Wakili wa utetezi, Gabriel  Mnyele aliiomba mahakama hiyo iuamuru upande wa mashtaka kuwapa washtakiwa hao maelezo ya malalamikaji  ili yaweze kuwasaidia  kuifahamu vizuri kesi inayowakabili.

  Baada ya kutolewa kwa ombi hilo, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Elizabeth Kaganda alidai kuwa hana pingamizi na ombi hilo na kwamba atawapatia.  Akitoa uamuzi juu ya ombi hilo, Hakimu Lema aliutaka upande wa mashtaka umpatie kila mshtakiwa maelezo ya mlalamikaji na kwamba dhamana zao zinaendelea.

Awali akiwasomea maelezo hayo, Kaganda alidai kuwa Makunga ambaye ni Mhariri Mtendaji Mkuu wa MCL akikaimu nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji, Novemba 30, 2011 alichapisha waraka wenye kichwa cha habari 'Waraka Maalumu kwa askari wote', ambao uliandikwa na Samson Mwigamba kwenye gazeti la Tanzania Daima toleo la 2553.  Kaganda alidai Makunga alifanya kosa hilo kinyume na kifungu cha 32 (1) (c) na 31 (1) (a) cha Sheria ya Magazeti  sura ya 229 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Akiendelea kuyasoma maelezo hayo ya awali, alidai kuwa Samson Mwigamba na Abisalom waliwashawishi askari na maofisa wa Jeshi la Polisi, Magereza pamoja na Jeshi la Ulinzi la Wananchi nchini (JWTZ), kutoitii Serikali jambo ambalo ni kinyume na kifungu cha 46(b), 55(10(a) na 35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu kama ilivyorekebishwa mwaka 2002.

Inadaiwa kuwa Novemba 30, 2011, gazeti la Tanzania Daima, toleo namba. 2553 lililochini ya Kibanda (Mhariri Mtendaji), lilichapisha waraka huo ambao uliandikwa na Samson Mwigamba kupitia safu yake ijulikanayo ‘Kalamu ya Mwigamba’.

Baada ya Kaganda kusoma maelezo hayo ya awali, ambayo washtakiwa wote waliyakana na kukubali vyeo na majina yao pekee.  Kaganda aliieleza mahakama kuwa wao watapeleka vielelezo vitatu  ambavyo ni  maelezo ya onyo waliyoyatoa washtakiwa polisi, gazeti lililoandika walaka huo unaodaiwa kuwa ni wa uchochezi na maoni ya wataalam.

Hakimu Lema aliiahirisha kesi hiyo hadi Agosti 7 , mwaka huu itakapoanza kusikilizwa.  Makunga alikaimu nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi (MCL)  kwa zaidi ya miezi mitano baada ya aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo Sam Shollei kumaliza muda wake. Kwa sasa nafasi hiyo inashikiliwa na Tido Mhando.  

Awali Machi 26, mwaka huu,  kwa mara ya kwanza alisomewa shtaka hilo linalomkabili. Makunga  anatetewa na Mawakili Mabere Marando na Frank Mwalongo.  Makunga aliachiwa huru baada ya kukamilisha masharti ya dhamana ya  kuwa na wadhamini wawili waliosaini bondi ya Sh5 milioni, mmoja wa wadhamini hao atoe hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha na kusalimisha hati yake ya kusafiria mahakamani, kuripoti polisi mara moja kila mwezi na kutotoka nje ya Dar es Salaam bila ya kibali cha mahakama.
Februari 15, mwaka huu, Wakili huyo Mwandamizi wa Serikali aliieleza Mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.

No comments:

Post a Comment