Thursday, June 21, 2012

Mgomo wa madaktari wanukia Jumamosi

KUNA dalili ya mgomo wa madaktari kuanza upya kuanzia Jumamosi kutokana na Serikali kushindwa kutekeleza madai yao.Tayari madaktari hao wameitisha mkutano Jumamosi jijini Dar es Salaam, unaotarajiwa kuwa na wawakilishi kutoka mikoa mbalimbali nchini, kujadili hatima yao na kutoa uamuzi wa nini cha kufanya, huku habari za ndani zikieleza kuwa upo uwezekano wa kuweka zana zao chini.

Hali hiyo inakuja ikiwa ni miezi mitatu tangu nchi kushuhudia mgomo mkubwa wa wanataaluma hao mapema mwaka huu, ambao ulisababisha kung'olewa kwa vigogo wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

Kutokana na mgomo huo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Blandina Nyoni na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Deo Mtasiwa walisimamishwa kazi; na baadaye aliyekuwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda na naibu wake, Dk Lucy Nkya waling’olewa kwenye nyadhifa hizo, katika mabadiliko ya mawaziri mwezi uliopita.

Kishindo hicho kikiwa hakijasahaulika, madaktari wa mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza na Kilimanjaro wametoa matamko ya kutaka uitishwe mgomo mwingine nchi nzima ikiwa Serikali haitaweka jitihada za makusudi kukutana nao kabla ya Juni 23, mwaka huu, siku ambayo mkutano wao utafanyika.

Madaktari wa Bugando mkoani Mwanza wametoa msimamo kwamba watashiriki kikamilifu katika hatua yoyote itakayoamuriwa na mkutano huo, yenye lengo la kushinikiza utekelezaji wa madai yao.

Katika mkutano uliondaliwa na Chama cha Madaktari (MAT), madaktari hao walipinga ripoti ya hatua zilizofikiwa na wakilishi wao na Serikali wakidai imepuuza madai yao.Mkutano huo ulitoa wiki mbili kwa Serikali kuchukua hatua, la sivyo wangetangaza mgogoro nayo.

Katibu Mkuu wa MAT, Dk Rodrick Kabangila aliliambia gazeti hili jana kuwa muda walioipa Serikali umemalizika na hakuna hatua zilizochukuliwa.“Sisi tulishatoa msimamo wetu, tunasuburi muda huo ufike tufanye mkutano. Katika mkutano huo ndipo tutakapoamua cha kufanya,” alisema Dk Kabangila.

Dk Kabangila alifafanua kwamba Serikali inalishughulikia suala hilo kisiasa na ndio sababu inashindwa kulipatia ufumbuzi wa kudumu.“Sisi tulishakubaliana kujadiliana nao, lakini wenzetu wanaingiza siasa katika suala hili kwani tangu tulitoa tamko hadi sasa hakuna hatua iliyochukuliwa na Serikali,” alisisitiza.

Hata hivyo, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi amekwishaeleza dhamira ya Serikali ya kutaka kushughulikia suala hilo kwa njia ya majadiliano.Mwinyi alikaririwa na gazeti hili Jumatatu akisema kuwa Serikali itakutana nao kujadili na kufikia mwafaka juu ya madai yao, huku akiwasiii madaktari kutojihusisha na mgomo.

Kamati ya Bunge imeiomba Serikali kuchukua hatua za kuzuia mgomo wa madaktari kabla haujaanza.Kauli hiyo ilitolea juzi na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, Margaret Sitta katika Bunge la Bajeti linaloendelea mjini Dodoma.

Madai ya madaktari
Baadhi ya madai ya madaktari ni kupandishwa kwa mshahara, ongezeko la posho ya kulala kazini, posho za kufanya kazi katika mazingira magumu, bima ya afya, nyumba, usafiri na pia kuboreshewa mazingira ya kufanyia kazi kwa kupeleka vifaa na dawa katika Vituo vya Afya na hospitali.

Tamko la Mwanza
Kamati Ndogo ya Madaktari inayoshughulikia malalamiko yao Kanda ya Ziwa, imetoa tamko la kuungana na wenzao nchini, katika uamuzi wowote ambao utatolewa keshokutwa.Wakizungumza na waandishi wa habari jana katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC), Dk Kiriti Richard katika kikao chao wamefikia uamuzi huo baada ya Serikali kutokuwa na majibu ya malalamiko yao.

Alisema wamepokea taarifa kutoka serikalini ambayo imetokana na vikao sita vilivyofanywa baina ya pande mbili lakini hawajaridhika maamuzi ya Serikali.

Naye Dk Geogre Adriano alisema mbali na taarifa ya Serikali kutokuwa na majibu ya kuwaridhisha, hata Bajeti ya Wizara ya Afya 2012/13 haijaonyesha kama itatatua matatizo hayo.

KCMC nao wa
Madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC iliyopo Moshi mkoani Kilimanjaro wameiomba Serikali kutekeleza malalamiko yaliyotolewa na MAT ili kuepusha mgogoro usio wa lazima baina yao na Serikali, ambao utawaumiza wananchi wasio na hatia.

Madaktari hao ambao walikutana Juni 15, mwaka waliazimia kutounga mkono taarifa iliyotolewa na Serikali kuhusiana na mgogoro uliokuwepo baina ya pande hizo mbili kwa kile walichodai kuwa taarifa hiyo haijakidhi mahitaji.

Wakizungumza na waandishi wa habari katika kikao cha pamoja, Dk Rosemary Mrina, Dk Mugisha Nkoronko na Annette Kessy walisema wanaungana na MAT kutangaza mgogoro upya na Serikali kuanzia Jumamosi, kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake.

Wito kwa madaktari
Serikali imetakiwa kuwabana wanaharakati wa haki za binadamu ambao hawajali haki ya wagonjwa kwa kuwa ndio chanzo cha mgomo wa madaktari nchini.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Wakili wa Kujitegemea ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Chama Cha Mapinduzi (UV-CCM), Emmanuel Makene alisema Serikali inatakiwa kubana taasisi za wanaharakati kwa kuwa wana lengo la kuliangamiza taifa.

“Wanajiita wanaharakati wa haki za binadamu na kutoa ushauri wa kisheria kwa madaktari, lakini hata siku moja uharakati wao sijawahi kuwaona makahamani wakishinda kesi hata moja, pia sijawahi kuona wakipewa leseni ya uwakili,”alisema Makene.Habari hii imeandaliwa na Sheilla Sezzy, Mwanza na Geofrey Nyang’oro, Rehema Matowo Moshi na Zaina Malongo

 



No comments:

Post a Comment