Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi
akizungumza na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika katika viwanja vya bunge
jana. Mnyika amerejea kuhudhuria vikao vya bunge baada ya juzi
kutimuliwa bungeni na Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai. Picha na Edwin
Mjwahuzi
Moses Mashalla, Arusha MWASISI wa Chadema, Edwin
Mtei amemtetea Mbunge wa Ubungo, John Myika kuwa alikuwa sahihi kusema
kwa Rais Jakaya Kikwete ni dhaifu, kwa kuwa kuna matukio mengi
yaliyohitaji uamuzi wake na hakuutoa kwa wakati.
Pia Mtei amelaumu Kanuni za Bunge zilizomwezesha Naibu Spika, Job Ndugai kumtoa nje ya ukumbi wa Bunge mbunge huyo.
Juzi, Mnyika alitolewa nje ya ukumbi wa Bunge, baada ya kukukataa kufuta kauli yake kuwa ‘Rais Jakaya Kikwete ni dhaifu’. Akitetea
kauli hiyo, Mtei alirejea baadhi ya matukio aliyodai yanaonyesha
udhaifu huo, ukiwamo uamuzi ya Rais Kikwete juu ya hatua za kuwachukulia
walioiba fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), katika Benki Kuu
ya Tanzania (BoT).
Mtei alifafanua kwamba, kitendo cha Rais
Kikwete kuwataka wezi hao warudishe fedha walizoiba badala ya
kuwakamata, kinadhihirisha udhaifu mkubwa wa kiongozi huyo.
“Rais Kikwete ana udhaifu wa kuwachukulia hatua za kisheria watu ambao
wanahujumu taifa kwa ufisadi…udhaifu wa Rais ni kama kutowadhibiti wezi
wa fedha zetu kama fedha za EPA. Aliwaambia wezi warudishe fedha,
badala ya kuwatia ndani wanabaki wanatamba kwa kuiba fedha zetu,”
alisisitiza Mtei aliyewahi kuwa Gavana wa Benki Kuu.
Alisema
kibaya zaidi ni kwamba, nchi inayumba kutokana na uongozi mbovu kuanzia
ngazi ya urais hadi chini, kwa kuwa tunaongozwa na watu wasiojua na
kuisimamia Katiba.
Kauli kuhusu Bajeti Akitoa maoni yake juu
ya Bajeti ya Serikali ya mwaka huu, Mtei alisema Bajeti hiyo haina
jipya kwa kuwa haishughulikii matatizo na kero za wananchi.
Alisema Bajeti hiyo ambayo mjadala wake unahitimishwa kesho, haiwezi kukabilina na mfumuko wa bei unaolikabili taifa.
Kuhusu
suala la deni la Taifa linalofikia Sh20.2 trilioni, alisema nchi ipo
njia panda, hali ambayo ni hatari kwa kuwa ni mzigo kwa taifa na
linazidi kuongezeka kila mwaka.
Mwanasiasa huyo ambaye ni
Mwenyekiti wa kwanza wa Chadema, aliponda vitendo vya Serikali kukopa
fedha kila mara kwenye mabenki ya kibiashara nchini, na kuomba kwa
wahisani. |
No comments:
Post a Comment