Friday, June 29, 2012

Mshirika wa Gbagbo ahofia maisha yake


Charles Ble Goude

Kiongozi wa vijana mwenye msimamo mkali nchini Ivory Coast Charles Ble Goude ameambia BBC anahofia maisha yake mwaka mmoja baada ya kwenda mafichoni.
Ble Goude alienda mafichoni mwezi Aprili mwaka jana alipokamatwa Rais wa zamani Laurent Gbagbo ambaye sasa anazuiliwa katika mahakama ya kimataifa ya jinai- ICC iliyoko The Hague.


Serikali ya Ivory Coast imetoa kibali cha kuwakamata washirika wa karibu wa Bw Gbagbo.Kiongozi huyo wa vijana amekanusha kujificha na kusema watu wamekuwa wakimsaka ili kumuua.

Umoja wa Mataifa ulisimamia uchaguzi mkuu wa mwezi Novemba mwaka 2010 na kutangaza Alassane Ouattara kama mshindi lakini upande wa Gbagbo ulikataa kushindwa hali iliyosababisha machafuko ya kisiasa. Watu 3000 waliuawa na mamia wakakimbia makaazi yao.

Charles Ble Goude ni miongoni mwa watu waliowekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa mwaka wa 2006 kwa kuchochea mashambulio dhidi ya wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa.Kwenye mahojiano na BBC Ble Goude alikataa kusema aliko japo alikiri kua nje ya Ivory Coast.

No comments:

Post a Comment