Baadhi ya wanafunzi wanaosoma shuleni hapo wakiwa katika muda wa mapumziko
UCHUNGUZI
uliofanywa na Shirika la HakiElimu umegundua kuwa Shule ya Sekondari ya
Naura iliyoko katika kata ya Lemara , eneo la Njiro ni miongoni mwa
shule zenye maendeleo hafifu ya kielimu ukilinganisha na shule nyingine
za serikali na kata zilizoko katika Manispaa ya Wilaya ya Arusha.
Shule
hii iliyoanzishwa mwaka 2008 , inakabiliwa na upungufu mkubwa wa walimu
kwani kuna masomo hayajawahi kuwa na walimu toka shule hiyo ianzishwe mfano masomo ya Chemistry, Mathematics na Book- Keeping . Pia kuna masomo ambayo yana mwalimu mmoja mmoja mfano English, Commerce, Literature, na Civics toka kidato cha kwanza mpaka cha nne.
Tofauti
na shule nyingine ambazo hukimbiwa na walimu kutokana na kuwa mazingira
magumu shule hii iko eneo zuri na maarufu waishio watu wenye kipato cha
juu mkoani Arusha lijulikanalo kama Njiro na kuacha maswali kuwa kama
kuna tatizo la uongozi wa shule au kuna tatizo la upangaji wa walimu
unaofanywa na serikali , hili hali shule nyingine zikiwa na walimu
lukuki.
Akielezea sababu nyingine za kudorora kitaaluma shuleni hapa Mwalimu Mshobozi alisema kuna mrundikano mkubwa wa wanafunzi kushinda uwezo wa shule akitolea mfano wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka huu kufikia 307.
Tofauti na malengo ya shule ya kata kusomesha wanafunzi wa maeneo ya karibu , wanafunzi
wa shule hii wanatoka katika kata zote zilizoko manispaa hii kukiwa na
umbali mrefu na kukabiliwa na shida kubwa ya usafiri jambo ambalo pia
alilielezea kuwa ni moja ya sababu za kudorora kitaaluma kwa wanafunzi wa shuleni hapo.
Kwa
upande wake Mwalimu Mkuu msaidizi Bi Mary Shirima alisema sababu za
kudodora kitaaluma kwa shule yake ni mwako mdogo wa kielimu kwa wazazi
pamoja na watoto wenyewe akisema wengi wa wanafunzi ni kama
wamelazimishwa kuja kusoma shuleni hapo na wazazi wao hawajishughulishi
na maendeleo ya watoto wao.
“
Historia ya wanafunzi waliomaliza kidato cha nne ni tata kwani kuna
waliokuwa wameolewa na wafanyabiashara mara baada ya kumaliza darasa la
saba ,ghafla wakasikia wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza na
kulazimika kuja shuleni, sasa katika hali hiyo unatarajia nini” aliuliza
Mwalimu Shirima.
Katika mtihani wa kidato cha nne wa taifa wa mwaka jana 2011 jumla ya wanafunzi 164 walifanya mtihani huo
ambapo hakuna aliyepata daraja la kwanza wala la pili, wanafunzi 2
walipata daraja la tatu , 24 wakapata daraja la nne na 138 walifeli kwa
kupata zero. Shule hii ilishika nafasi ya mwisho kati ya shule 137
zilizofanya mtihani huo katika mkoa wa Arusha. Kitaifa ilishika nafasi
ya 2994 kati ya 3108 zilizofanya mtihani huo.
HakiElimu inatoa wito
kwa Serikali kupitia mamlaka husika kuangalia upangaji wa walimu na
uchaguzi wa wanafunzi shuleni hapo. Wazazi na wakazi wa Njiro nao
wanatikiwa kuchukua jitihada za ziada kuhakikisha wanafunzi walioko
shuleni hapa wanapata elimu bora na kuelimika .
No comments:
Post a Comment