Saturday, June 16, 2012

Serikali yashindwa kupeleka mashahidi kesi ya Mattaka

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Ndege (ATCL), David Mattaka
 
Upande wa Jamhuri katika kesi ya matumizi mabaya ya madaraka na kununua magari ya mitumba kinyume na Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2004 inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Ndege (ATCL), David Mattaka na wenzake jana ulishindwa kupeleka mashahidi mahakamani dhidi ya mshtakiwa


Kutokana na hali hiyo, kesi hiyo iliahirishwa na Hakimu Mkazi Ritha Tarimo hadi Julai 13, mwaka huu itakapoanza kusikilizwa.

Mbali na Mattaka washtakiwa wengine ni, Kaimu Ofisa Mkuu wa Kitengo cha Fedha, Elisaph Mathew Ikomba na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Ndani, William Haji, wote kutoka shirika hilo.

Kabla ya kuahirishwa kesi hiyo, Wakili wa Serikali Mkuu, Oswalid Tibabyekomya, alidai kuwa kesi hiyo ilipangwa kuanza kusikilizwa ushahidi wa Jamhuri lakini kwa bahati mbaya hakuna shahidi aliyepatikana.

Hakimu Tarimo aliutaka upande wa Jamhuri upeleke mashahidi mahakamani na kesi hiyo itaanza kusikilizwa Julai 13, mwaka huu.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka ya kushindwa kutunza kumbukumbu za mawasiliano ya manunuzi waliyokuwa wakifanya na mtoa huduma kinyume na kifungu cha cha Sheria ya Manunuzi ya Umma Namba 21 ya mwaka 2004 na kanuni ya 17(1) ya Sheria ya Manunuzi.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment