Sunday, June 17, 2012

Umoja wa Mataifa wasitisha shughuli za waangalizi wake Syria

Umoja wa Mataiafa umesitisha shuguli za waangalizi wake nchini Syria leo hii kutokana na kupamba moto kwa umwagaji damu wakati vikosi vya serikali vikishambulia kwa mizinga ngome kuu za waasi. 

Waangalizi hao, ambao hawana silaha, wenyewe wamekuwa wakilengwa kwa mashambulizi kila siku tokea waingie nchini humo hapo katikati ya mwezi wa Aprili, kusimamia mpango wa kusitisha mapigano unaoungwa na Umoja wa Mataifa, ambao umekuwa ukipuuzwa kwa kiasi kikubwa na pande zote za
mgogoro huo.
 Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Susan Rice, amewafanananisha waangalizi hao na " watu wanaosubiri maafa bila ya kujitambuwa katika uwanja wa shabaha "

Akifafanuwa juu ya uamuzi huo, mkuu wa timu ya waangalizi hao, Meja Jenerali Robert Mood,

amezungumzia juu ya kupamba moto kwa mapigano, hatari inayowakabili waaangalizi hao 300 na halikadhalika kutokuwepo kwa nia ya kusuluhisha mzozo huo kwa njia ya amani kati ya pande mbili zinazohasimiana.

Siku 10 za mapigano


Waangalizi wa Umoja wa Mataifa nchini Syria wakiwa kazini. Waangalizi wa Umoja wa Mataifa nchini Syria wakiwa kazini.
Jenerali Mood amesema katika katika taarifa kwamba mapigano yanayohusisha matumizi ya silaha yamekuwa yakipamba moto nchini Syria katika kipindi cha siku 10 zilizopita na kwamba mapambano hayo yanapunguza uwezo wao wa uangalizi, kuyakinisha, kuripoti na pia kusaidia katika mazungumzo kati ya wenyeji na kushughulikia mpango wa kuleta utulivu.
Amesema kimsingi mambo yanayotendekea nchini humo yanakwamisha uwezo wao wa kutekeleza shughuli zao kwa mujibu wa mamlaka waliyopewa.
Kwa mujibu wa Jenerali huyo, kukosekana kwa nia ya makundi husika kutafuta usuluhishi wa amani kwa mzozo huo na shinikizo la kuteka maeneo kunasababisha kuongezeka kwa maafa kwa pande zote mbili ambapo raia wasiokuwa na hatia, wanaume na wanawake halikadahalika watoto wanauwawa kila siku. Hali hiyo pia inawaweka katika hatari kubwa waangalizi wao.
Mood ameongeza kusema kwamba waaangalizi hao hawatopiga doria na watabakia kwenye vituo vyao hadi hapo itakapotolewa taarifa zaidi.
Kusitishwa kwa shughuli hizo za waangalizi wa Umoja wa Maataifa nchini Syria kutafanyiwa atahmnini kila siku na kwamba shughuli hizo zinaweza kuanza tena wakati hali itakaporuhusu kwa waangalizi hao kuweza kutekeleza shughuli zao kwa mujibu wa mamlaka yao.
Watu zaidi ya 30 wauawa

Mji wa Homs ukiwa kwenye mashambulizi. Mji wa Homs ukiwa kwenye mashambulizi.
Wakati uamuzi huo ukitolewa inaripotiwa kwamba watu 31 wameuawa nchini kote Syria wakati vikosi vya serikali vikizishambulia kwa mizinga ngome kuu za waasi, ukiwemo mji wa Douma karibu na mji mkuu wa Damascus na kitovu cha mapambano cha mji wa Homs.
Zaidi ya watu 14,000 wameuwawa tokea kuanza kwa upinzani dhidi ya utawala wa Rais Bashar al-Assad hapo mwezi wa Machi 2011.
Kwa mujibu wa Rami Abdel Rahman wa Kituo cha Uangalizi wa Haki za Binaadamu nchini Syria katika mapigano ya umwagaji damu ya hivi karibuni kabisa, familia zimenasa kwenye mapigano hayo katika miji ya Khalidiyeh, Jourat al-Shiah, Qrabees na Qasoor - maeneo ya mji wa Homs ambao ni ngome kuu ya wapinzani.
Watu hao hawana chakula na hawapatiwi huduma za matibabu. Kituo hicho cha haki za binaadamu kimetowa wito wa daharura kwa Katibu Mkuu wa Mataifa, Ban Ki-moon, na wale wenye hisia ya ubinaadamu kuingilia kati katika kukomesha mashambulzi ya mizinga ya vikosi vya serikali.

No comments:

Post a Comment