Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila. |
Mahojiano hayo ambayo yaliingia siku ya pili jana, yalifanyika zikiwa zimepita siku sita tangu mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo ambaye ni Mbunge wa Bahi (CCM), Omary Badwel, kukamatwa na taasisi hiyo na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kupokea rushwa
ya Sh. milioni moja.
Mahojiano yalianza juzi na yanafanyika baada ya Kafulila ambaye pia ni mjumbe wa LAAC, kuitisha mkutano na waandishi wa habari Jumapili wiki iliyopita jijini Dar es Salaam na kuituhumu kamati hiyo kwamba, imekithiri kwa rushwa.
Habari zilizothibitishwa na baadhi ya wajumbe wa LAAC, zinaeleza kuwa mahojiano hayo yaliendelea jana, baada ya wajumbe kadhaa wa kamati hiyo, akiwamo Kafulila, kuhojiwa jana.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Takukuru, Alex Mfungo, alipoulizwa jana, alisema hadi jana alikuwa hajui kama kuna wajumbe wa LAAC wanaohojiwa na taasisi yake.
Hata hivyo, alisema walipomfikisha mahakamani Badwel Jumatatu wiki hii, walisema uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili unaendelea na kwamba, kazi hiyo inafanywa na maofisa wake.
“Sijui wanamhoji nani. Wakikamilisha uchunguzi na kuniletea taarifa ndio nitajua kama kuna waliohojiwa au la ambao wanastahili kuwa mashahidi katika kesi husika (ya Badwel),” alisema Mfungo.
Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, Mbunge wa Mtwara Mjini (CCM), Hasnain Murji, alithibitisha kwenda Takukuru jana kuitikia wito wao uliomtaka aende kuhojiwa.
Hata hivyo, alisema hakuweza kuhojiwa baada ya kufika na kukuta maofisa wa Takukuru wanaohusika wakiwa wamebanwa na kazi nyingi za kuwahoji watu wengine, hivyo akapangiwa kuhojiwa leo.
Murji alisema hayo alipotakiwa na NIPASHE kueleza kama alikwishahojiwa na Takukuru au la.
“Mimi zamu yangu (ya kuhojiwa) itakuwa kesho (leo). Nilikwenda (Takukuru) leo, lakini (maofisa wanaohusika) walikuwa busy kwa wengine,” alisema Murji.
Awali, NIPASHE iliwasiliana na Kafulila kwa njia ya simu jana, lakini alikataa kuthibitisha kama alihojiwa na Takukuru au la.
Badala yake, aliishia kusema kuwa leo atapeleka barua kwa Spika wa Bunge, kumjulisha kuwa hatahudhuria tena vikao vya LAAC mpaka Spika atakapochukua hatua, ikiwamo kuivunja kamati hiyo na kuipanga upya.
Habari zaidi zinasema hadi kufikia jana, kulikuwa na taarifa za Takukuru kuwaita wajumbe watano tu wa LAAC kwa ajili ya kuhojiwa.
Mbunge wa Mbozi Mashariki (CCM), Godfrey Zambi, alisema anachojua yeye ni kuwa wajumbe walioitwa na Takukuru kwenda kuhojiwa ni watano tu na kwamba, kati ya wajumbe hao yeye hayumo.
Hata hivyo, Zambi alipotakiwa na NIPASHE jana kuwataja wajumbe hao, alikataa kufanya hivyo badala yake alimtaka mwandishi kwenda kwa Katibu wa Bunge.
“Majina yao (wajumbe hao) nimeyaona. Wengine walihojiwa jana (juzi), wengine wamehojiwa leo (jana) na nadhani wengine watahojiwa kesho (leo). Nenda kwa Katibu wa Bunge ndiko summons (hati za kuitwa) zao zilikopelekwa. Najua ni watano, lakini katika hao mimi simo,” alisema Zambi.
Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, hakupatikana jana ofisini kwake kuzungumzia suala hilo na hata alipopigiwa simu yake mkononi, muda wote jana ilikuwa imezimwa.
Mmoja wa maofisa waandamizi wa Bunge, ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini kwa kuwa siyo msemaji, aliliambia NIPASHE jana kuwa wito wa kuitwa wajumbe hao wa LAAC kwenda kuhojiwa na Takukuru, ulipelekwa moja kwa moja kwa wajumbe husika.
Kwa mujibu wa habari hizo, wa kwanza kuitwa na Takukuru na kuhojiwa ni mmoja wa maofisa waandamizi wa LAAC mwenye jukumu la kuwezesha shughuli za kamati hiyo.
Mmoja wa wajumbe wa LAAC, alisema taarifa za kuaminika alizonazo ni kwamba, mahojiano yanafanywa na Takukuru kwa kuwahoji wajumbe kadhaa wa kamati hiyo kama siyo wote.
Mbunge wa Kilombero (CCM), Abdul Mteketa, naye aliliambia NIPASHE kwa njia ya simu juzi na kusema kuwa alimuuliza Makamu Mwenyekiti wa LAAC, Iddi Azzan, ambaye alimthibitishia kwamba, Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Suzan Kiwanga na Katibu wa LAAC, Mswige Bisile, walihojiwa na Takukuru juzi.
“(Makamu Mwenyekiti, Azzan), ameniambia pia kuwa hana uhakika, lakini huenda kamati nzima (LAAC) watakwenda (Takukuru kuhojiwa),” alisema Mteketa.
Hata hivyo, Mteketa alisema haogopi kuhojiwa na Takukuru kwa sababu wezi wanajulikana na kwamba, hana tamaa ya Sh. milioni moja.
Hata hivyo, Kiwanga alipoulizwa na NIPASHE kwa njia ya simu juzi, alisema bado hajajua kama atahojiwa au la na kusema: “Labda nitaitwa.”
Spika wa Bunge, Anne Makinda, hakupatikana ofisini kwake kuzungumzia suala hilo na alipopigiwa simu zake zote, zilikuwa zikiita bila kupokewa.
Juzi Makinda aliliambia gazeti hili kuwa angezengumzia suala hilo jana, lakini hakutimiza ahadi yake baada ya juhudi za kumtafuta ofisini kwake kukwaa kisiki.
Jumapili wiki iliyopita, Kafulila akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam, aliituhumu LAAC kuwa imekithiri kwa rushwa.
Kutokana na tuhuma hizo, alimtaka Spika Makinda, kuivunja kamati hiyo, vinginevyo yeye atajiondoa.
Pia aliitaka Kamati ya Maadili kulitumia Bunge kumvua ubunge, Badwel, kutokana na tuhuma za kupokea rushwa zinazomkabili kwa madai kwamba wananchi hawatakuwa na imani tena na kamati hiyo.
“Ikumbukwe Juni 13, 2011 nilieleza bungeni namna wabunge wa Kamati ya LAAC wanavyoomba rushwa kwa watumishi wa serikali, huku nikimtaja kwa jina Mbunge wa Bahi, Omary Badwel kuwa ni miongoni mwao,” alisema Kafulila ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo.
Kafulila alisema licha ya kutoa taarifa hiyo bungeni na kumwandikia Spika kuhusu vitendo vya rushwa vya baadhi ya wajumbe, hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa.
“Nilijitoa mhanga kwa kutaja majina ya wabunge wanaoomba rushwa kwa watumishi wa Serikali, lakini hatua hazikuchukuliwa, sasa leo Takukuru wamemtia mbaroni mmoja wao, bado hamuamini,” alisema Kafulila.
“Sasa naomba niweke wazi kwamba kama Spika hataivunja kamati hii na kuunda nyingine nitajiondoa kwenye kamati kwa sababu itakuwa imepoteza imani kwa wananchi,” alisema Kafulila.
Alisema kamati hiyo imepoteza uhalali na sifa za kuendelea kuzikagua hesabu za serikali za mitaa kwa sababu wajumbe wake wanatuhumiwa kwa rushwa.
Kafulila alisema ni wajibu wa Spika kutafakari upya kuhusu hadhi ya kamati hiyo na kuipanga upya kwa kuzingatia maslahi ya umma.
Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine Mrema, ndiyo yenye jukumu la kusimamia hesabu za serikali za mitaa.
“Serikali legelege ni matokeo ya Bunge legelege kwa kuwa ni kazi ya Bunge kusimamia na kuidhibiti serikali kikatiba,” alisema Kafulila.
Mbunge huyo wa Kigoma Kusini aliitaka Bunge kuweka azimio la kumvua ubunge Badwel kwa tuhuma za rushwa zinazomkabili.
“ Kamati ya Maadili ya Bunge ifanye hivyo ikiwa ni hatua za kinidhamu kuchukuliwa kwa mbunge huyo kwa tukio hilo la aibu,” alisema.
Kafulila alisema hata mabunge ya Jumuiya za Madola ambalo Tanzania ni miongoni mwao, huchukua hatua za kinidhamu za kuwavua wabunge wanaotuhumiwa kwa makosa ya aibu kabla ya mahakama hazijatoa uamuzi.
Kwa mujibu wa Kafulila, Bunge la Uingereza limeshachukua hatua za kuwavua ubunge watuhumiwa zaidi ya 59 ili kujenga imani ya wananchi kwa Bunge lao.
“Kwa hiyo nafahamu kwa kutumia azimio, Bunge lina uwezo wa kumvua madaraka mbunge yeyote ambaye amefanya vitendo vya aibu vya kuliaibisha Bunge,” alisema.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 71(1) (d) Mbunge anaweza kupoteza nafasi yake ikiwa itathibitishwa kwamba amevunja masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Badwel na Zambi, ni miongoni mwa wabunge waliotajwa na Kafulila katika Bunge la bajeti la mwaka jana kwamba, aliwaona wakichukua rushwa kwa viongozi wa halmashauri ambayo hakuitaja.
Badwel, ambaye alikamatwa na Takukuru akidaiwa kupokea rushwa kutoka kwa watumishi wa serikali katika hoteli moja jijini Dar es Salaam, alifikishwa mahakamani Juni 4, mwaka huu, kujibu tuhuma hizo.
HABARI NA NIPASHE
No comments:
Post a Comment