Saturday, June 9, 2012

Wahariri wawashitaki Waziri, Katibu Mkuu kwa Kikwete

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limeamua kuwasilisha rasmi malalamiko yake kwa Rais Jakaya Kikwete kuhusiana na mwenendo wa viongozi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ambao unaelekea kukwaza ustawi wa tasnia ya habari nchini.


Wahariri hao kwa kauli moja waliazimia kufikisha kilio chao kwa Rais Kikwete na kumuomba aingilie kati suala hilo kwa nia ya kuiokoa tasnia ya habari, ambayo ni muhimu kwa ustawi na afya ya taifa hili.

Taarifa hiyo ya TEF ilisema kwamba Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Seth Kamuhanda, hawakushiriki hata kwa kufungua Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Mwaka wa Mashauriano kati yao na Baraza la Habari Tanzania (MCT) uliofanyika Juni 3-5 mwaka huu, mjini Morogoro kama walivyoombwa na MCT na wao wenyewe kuthibitisha kwa nyakati tofauti.

“Kwa masikitiko makubwa, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Seth Kamuhanda, hawakushiriki hata kwa kufungua mkutano huu kama walivyoombwa na Baraza la Habari Tanzania na wao wenyewe kuthibitisha kwa nyakati tofauti.

“Kwa mshangao wa wahariri na wadau wengine waliohudhuria mkutano huo, viongozi hao wawili mbali ya kutumiwa rasimu ya hotuba ambayo ilipaswa kusomwa kwanza na waziri ambaye ndiye alipaswa kuwa mgeni rasmi, kabla ya yeye mwenyewe (waziri) kutoa taarifa MCT kwamba, angewakilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara hawakutokea katika mkutano huo wala kutuma mwakilishi mwingine yoyote, huku wakitoa udhuru kwamba walikuwa na kazi nyingine,” limesema tamko hilo.

Viongozi hao wa wizara waliombwa na MCT, kufungua mkutano huo.

Jukwaa hilo lilisema hatua ya viongozi hao kushindwa kufika katika mkutano huo muhimu kwa maendeleo ya tasnia ya habari nchini ikiwa ni pamoja na kushindwa kwao kutuma mwakilishi mwingine kutoka wizarani, siyo tu iliwashtua wahariri, bali iliwasononesha na kuwashangaza.

“Kitendo cha wiki hii kinatupa shaka iwapo tunastahili kuendelea kuwa na uongozi wa Waziri na Katibu Mkuu wa sasa katika wizara hii. Tunasema hivyo kwani tuna shaka sana kama siku zijazo watatoa ushirikiano wa kutosha, hasa katika mchakato wa kupata sheria nzuri za Huduma za Vyombo vya Habari na ya Haki ya Kupata Habari,” tamko hilo lilisema.

Tamko hilo lilisema kuwa tukio hilo limepunguza imani ya wahariri kwa viongozi hao iwapo wataweza kuvusha tasnia ya habari katika mabadiliko ya kitaaluma na yale ya kimfumo katika kukusanya na kutoa habari nchini.

“Kwa maana hiyo tumeazimia kwamba kwanza; Tunatoa taarifa rasmi ili umma wa Watazania uweze kufahamu hali hii, lakini pili tutawasilisha rasmi malalamiko yetu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete aweze kuingilia kati hali hii kwa nia ya kuiokoa tasnia ya habari, ambayo ni muhimu kwa ustawi na afya ya taifa hili,” tamko lilisisitiza.

Wahariri hao walisema wanawahakikishia Watanzania na serikali kwa jumla kuwa vyombo vya habari vimejizatiti na kujipanga kuwatumikia Watanzania kwa kuzingatia maadili na weledi wa hali ya juu pia kwa kuzingatia matakwa na maslahi ya umma.

“Tunachoomba ni zana za kufanyia kazi hii. Zana hizi si nyingine bali ni Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari na Sheria ya Haki ya Kupata Habari, ambazo mchakato wake umedumu kwa zaidi ya miaka 10 sasa bila sheria hizi kupatikana,” tamko lilisema.

Walitaka mikingamo inayokwamisha sheria hiyo imalizwe ili sheria nzuri ipatikane na kutoa fursa kwa wanahabari kufanya kazi kwa uhuru na uhakika zaidi na kuongeza: “Hili la Waziri na Katibu Mkuu wizarani linaongeza wasiwasi wa kupatikana kwa sheria hizi.”

Walisema taarifa walizozipata zinaonyesha kuwapo kwa msuguano usio na afya kwa tasnia ya habari, kwa wizara na kwa serikali nzima kati ya Waziri na Katibu Mkuu.

Waliongeza kwamba kitendo cha viongozi hao kushindwa kutuma mwakilishi, ni ushahidi wa namna hali ilivyo mbaya na tete kimahusiano na kikazi katika wizara hiyo.

Tamko hilo la TEF lililosainiwa na Katibu wake, Neville Meena, lilisema mkutano huo ulihudhuriwa na wahariri watendaji na waandamizi wa vyombo vya habari nchini ukiwashirikisha wahariri kutoka vyombo vya serikali, binafsi na vile vinavyomilikiwa na vyama au taasisi za kidini pamoja.

Alisema pamoja na mambo mengine ulijadili hali na mwenendo wa vyombo vya habari nchini kwa sasa na kwa siku zijazo ambako mada zilizowasilishwa zililenga kusaidia kazi ya uandishi wa habari kufanyika kwa kuzingatia maadili, wajibu na weledi wa kitaaluma.

Pia mada hizo zililenga kuimarisha, weledi wa kitaaluma, uwajibikaji utendaji wa kazi na uhuru wa vyombo vya habari na zaidi kujenga mfumo wa usimamizi wa maadili ndani ya vyombo vya habari.

Wahariri hao na wadau wengine pia walijadili kuhusu mchakato wa sheria ya haki ya kupata habari na huduma za vyombo vya habari nchini ambao umekuwa ukisuasua kwa takriban miaka 10 sasa.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment