Wednesday, June 27, 2012

Wezi waiba kompyuta, nyaraka TCU

Watu wanaodaiwa kuwa wezi wamevamia ofisi za Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na kuwalewesha kwa chakula kinachodaiwa kuchanganywa na dawa za kulevya walinzi wa kampuni ya Bulwark waliokuwa wakilinda na kisha kuvunja milango na kupora nyaraka na vitu mbalimbali vya mamilioni ya fedha zikiwemo dola za Marekani 6,000.

Kamanda wa mkoa kipolisi wa Kinondoni, Charles Kenyela, akizungumza na NIPASHE alisema tukio hilo limetokea jana Juni 25 mwaka huu majira ya saa 12:30 asubuhi.



Alivitaja vitu vilivyoibwa kuwa ni pamoja na Kompyuta 11 aina ya Dell na HP, funguo za magari, fomu za wanafunzi wanaoomba mikopo, luninga aina ya Sumsung na dola za Marekani 6,000.

Alisema walinzi wa kampuni ya ulinzi ya Bulwark ambao walikuwa wakilinda ofisi hizo walikutwa wamelala fofofo wakiwa hawajitambui baada ya kula chakula kilichosadikiwa kuchanganywa na dawa za kulevya ambao ni Japhet James (34) mkazi wa Magomeni Kagera na Shaban Simba (60) mkazi wa Manzese.

Kamanda Kenyela alisema walinzi hao wamepelekwa hospitalini kwa ajili ya matibabu na wataendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi hadi watakapopata fahamu ambapo watatakiwa kutoa maelezo ya mazingira ya tukio hilo na ikibainika kulikuwa na uzembe hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

Alisema kufuatia tukio hilo, polisi waliimarisha ulinzi katika wilaya zote za jiji la Dar es Salaam na kufanikiwa kupata baadhi ya vitu vilivyoibwa katika eneo la Temeke ambavyo ni fomu za maombi ya mikopo, funguo za magari na luninga ya Samsung.

Kamanda Kenyela alisema vitu hivyo vimepatikana baada ya kuwakurupusha wezi waliohusika katika tukio hilo ambao walivitelekeza na kwamba msako mkali umeimarishwa kuhakikisha waliohusika na wizi huo wanatiwa mbaroni pamoja na vitu vingine ambavyo havijapatikana.

Aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi watuhumiwa wa makosa mbalimbali wawe wanakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria kwani hali hii ikiachwa kuendelea itahatarisha usalama wa nchi.

Kadhalika, alitoa tahadhari kwa viongozi wa makampuni binafsi ya ulinzi kuhakikisha wanajenga utamaduni wa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika malindo wanayolinda walinzi wao kwani ni dhahiri kumekuwa na uzembe kwa baadhi ya walinzi wa makampuni hayo.

Alisema vitendo vya wizi katika malindo yanayolindwa na walinzi wa makampuni binafsi yamekuwa yakitokea mara kadhaa kutokana na walinzi hao kuwa na udhaifu kwa kupenda kupewa vyakula, vinywaji na zawadi mbalimbali ambavyo vinakuwa vimechanganywa na madawa ya kulevya na hivyo kujikuta malindo yao yakiibiwa kirahisi.

“Kuna uzembe mkubwa kwa walinzi wa makampuni binafsi ya ulinzi, tutaanza kuishawishi serikali iyafutie usajili, mfano walinzi wa kampuni ya Bulwark inaonesha kabisa kulikuwa na uzembe mkubwa, walinzi wa kampuni hii walikuwa na silaha aina ya Short gun lakini hawakuitumia kukabiliana na wezi hao na bahati nzuri tumeikuta,” alisema Kenyela.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment