Wednesday, June 27, 2012

'Mashangingi' yafikia ukomo


Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
Serikali imetangaza kuachana na matumizi ya magari ya kifahari hususani mashangingi ili kupunguza gharama zisizo na tija na za lazima.

Alisema kuanzia mwaka mpya wa fedha wa 2012/2013, hatua zaidi zitachukuliwa kwa kuweka ukomo wa ukubwa wa injini za magari, ambayo yanaweza kununuliwa na serikali kuu na taasisi zake pamoja na mamlaka za serikali za mitaa.



Akisoma hotuba ya Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema chini ya utaratibu huo, magari yatakayonunuliwa yatakuwa ni yale yasiyozidi ukubwa wa injini wa cc 3,000 kwa viongozi na watendaji wakuu na yasiyozidi cc 2,000 kwa watumishi wengine, ambao wanastahili ya kutumia magari ya serikali.

Alisema vilevile, ili kupunguza matumizi ya magari kwa viongozi na watendaji wakuu kwa safari za mikoani, serikali itaanzisha vituo vya kanda vya magari ya serikali yatakayotumika mikoani kwa shughuli za kikazi na kwamba, mwongozo utatolewa.

"Inategemewa kuwa utaratibu huu utapunguza matumizi ya fedha za serikali kwa kiwango kikubwa," alisema Pinda.

Kadhalika, Pinda alitangaza 'kiama' kwa watumishi wa umma watakaothibitika kuhusika na ubadhirifu wa fedha za umma, hawatahamishwa, badala yake watachukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria, ikiwamo kuvuliwa madaraka na kufikishwa mahakamani wakiwa kwenye vituo vyao vya kazi.

Katika hotuba hiyo, Pinda aliliomba Bunge likubali kuidhinisha zaidi ya Sh. trilioni 3.8 kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ikiwa ni matumizi ya kawaida na fedha za maendeleo za ndani na nje, kwa mwaka mpya wa fedha wa 2012/2013.

Alisema hatua dhidi ya watumishi wa aina hiyo, ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi aliyoitoa katika Mkutano wa Saba wa Bunge, mwaka huu, kwamba serikali itayafanyia kazi maoni, ushauri na mapendekezo yaliyotolewa na wabunge wakati wakijadili taarifa mbalimbali za kamati za kudumu za Bunge.

"Sambamba na hatua hiyo, watumishi wa umma watakaotuhumiwa kufanya ubadhirifu wa fedha za umma watachunguzwa na tuhuma zikibainika ni za kweli watavuliwa madaraka waliyonayo na kufikishwa katika vyombo vya sheria," alisema Pinda na kuongeza:

"Napenda kusisitiza kwamba, serikali haitawahamisha watumishi wa aina hiyo, bali hatua za kinidhamu na kisheria zitachukuliwa wakiwa kwenye vituo vyao vya kazi."

Aliwataka watendaji wakuu wa serikali, bodi za wakurugenzi wa mashirika ya umma na madiwani kuhakikisha wanashiriki ipasavyo katika kusimamia fedha za umma kwa mujibu wa sheria, taratibu, miongozo na kanuni zilizopo.

Awali, katika hotuba hiyo Pinda aliwaagiza wakurugenzi watendaji wa mamlaka za serikali za mitaa kubandika kwenye mbao za matangazo za makao makuu ya halmashauri na katika vituo vyote vya utoaji huduma kiasi cha fedha kinachopokelewa kila mwezi na matumizi yake.

Alisema hatua hiyo itawezesha wananchi kufuatilia matumizi ya fedha zilizopelekwa kwa ajili ya utoaji  huduma kwenye maeneo yao.

RUSHWA, DAWA ZA KULEVYA

Alisema pia katika mwaka mpya wa fedha wa 2012/2013, serikali itaendelea kuchunguza tuhuma 2,729 za rushwa zilizopo na mpya zitakazopokelewa pamoja na kuendelea na uchunguzi maalum wa tuhuma zilizobainishwa kwenye taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu ubadhirifu katika taasisi mbalimbali za serikali.

Kuhusu dawa za kulevya, alisema hali siyo nzuri na ni dalili tosha kuwa nguvu zaidi zinahitajika ili kukabiliana na janga hilo kubwa kwa jamii.

POSHO ZA MADIWANI


Pinda alisema zoezi la kuangalia upya viwango vya posho za madiwani kwa lengo la kuviongeza limekamilika na kwa hiyo, kuanzia mwaka huo wa fedha, watalipwa viwango vipya vya posho vilivyoboreshwa.

ULINZI NA USALAMA

Waziri Mkuu alisema kwa mwaka 2012/2013, jumla ya vijana 5,000 wataanza tena kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria.

Alisema pia serikali itaendelea kuyawezesha majeshi kwa vifaa na zana za kivita na upatikanaji wa mahitaji muhimu.

MIUNDOMBINU, NISHATI

Alisema katika mwaka huo pia serikali imejipanga kujenga kilomita 414 na kukarabati kilomita 135 za barabara kwa kiwango cha lami pamoja na kujenga madaraja 11 katika barabara kuu.

Vilevile, alisema serikali itajenga kilomita 573 kwa kiwango cha changarawe na kilomita 32 kiwango cha lami katika barabara za mikoa pamoja na madaraja 27.

Alisema katika kipindi hicho Mfuko wa Barabara unatarajiwa kuingiza zaidi ya Sh. bilioni 400, ambazo zitatumika kwa ajili ya matengenezo, ujenzi na usimamizi wa miradi mbalimbali ya barabara zinazosimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na mamlaka za serikalki za mitaa.

Kuhusu nishati, Pinda alisema miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na serikali kutatua tatizo la umeme nchini, ni kushirikiana na Serikali ya Marekani kubaini vikwazo vinavyozuia sekta binafsi kuwekeza kwenye miradi ya umeme.

Alisema kazi hiyo inafuatiwa na utekelezaji wa Mpango Maalum wa Pamoja wa Miaka Mitano utakaoanza kutekelezwa mwaka wa fedha wa 2012/2013, lengo likiwa ni kuzalisha umeme wa Megawati 2,700 ifikapo mwaka 2016.

Pinda alisema hivi karibuni makampuni yanayofanya utafiti wa gesi asilia nchini yamegundua kiasi kikubwa cha gesi hiyo yenye futi za ujazo trilioni tatu na kwamba, imegundulika kwenye kina cha maji marefu baharini takribani kilomita 80 kutoka nchi kavu Mashariki mwaka Mkoa wa Lindi.

Alisema ugunduzi huo unafanya kiasi cha gesi kilichogundulika hadi sasa kwenye kina cha maji marefu baharini kufikia futi za ujazo trilioni 20.97.

Pinda alisema kwa kuzingatia fursa zinazotokana na kasi kubwa ya ukuaji wa sekta ya gesi nchini, serikali imejipanga kuhakikisha kwamba, taifa linanufaika kikamilifu na ugunduzi wa rasilimali hiyo.

AFYA

Katika mwaka wa fedha wa 2012/2013, serikali itaendelea na utekelezaji wa Mpango wa Kuangamiza Viluwiluwi vya Mbu kwa kutumia njia za kibaiolojia kwa ushirikiano na serikali ya Cuba.


 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment