Baba Mtakatifu Benedikt wa 16, amemteua Askofu Gerhard Ludwig
Müller wa jimbo la Regensburg, Ujerumani, kuwa mkuu wa jopo lenye
kusisitiza juu ya kutekelezwa kwa imani halisi ya kanisa Katoliki.
Uteuzi wa Müller si wa kushangaza. Kwa miezi kadha kumekuwa na tetesi kwamba yeye ndiye atakayechaguliwa na Papa Benedikt kumrithi kadinali Levada, Kabla ya uteuzi huo, Müller alikuwa amechaguliwa na Papa Benedikt kuwa mjumbe katika taasisi mbalimbali za kanisa katoliki.
Kadinali William Levada anayemaliza muda wake
Müller anaelekea kuwa chaguo bora kwa kuongoza jopo la kusimamia
mafundisho ya kanisa: Ni mwanatheolojia aliyebobea katika masomo yake,
mtu mwenye kushikilia kwa nguvu mafundisho ya kiasili ya kanisa na
anayezungumza lugha mbalimbali.Ingawa ana umri wa miaka 64, ambapo kwa kawaida watu hustaafu, Müller amepata nafasi ya kupanda cheo kwa sababu ya vipaji alivyo navyo.
Müller alizaliwa mwaka 1947 katika familia ya hali ya chini. Baada ya kumaliza masomo yake ya sekondari, alipata shahada ya uzamifu kabla ya kuwa padre.
Baadaye aliitwa kuwa Professor wa elimu ya imani ya dini katika chuo kikuu cha Munich, Ujerumani.
Kiongozi asiyependa kukosolewa
Miaka 10 iliyopita, Baba Mtakatifu Johanne Paulo wa pili alimteua Müller kuwa askofu wa jimbo la Regensburg. Tangu wakati huo pamekuwa na mgongano baina ya uongozi wa kanisa na waumini wanaotaka pawepo na mabadiliko ya sera za dini.
Müller ameonyesha kuwa mtu asiyependa kukosolewa, hasa na waumini wa kanisa lake. Kiongozi huyu wa dini ana sifa ya kuwa na mtazamo wa kihafidhina na asiyependa kujadili kuhusu njia za kulileta kanisa katoliki karibu zaidi na makanisa ya kiprotestanti.
Papa Benedikt wa 16.
Müller amekuwa maarufu kwa sababu ya kumuunga mkono Gustavo Gutierrez
kutoka Peru, ambaye ni mwanzilishi wa mafundisho ya imani ya ukombozi.
Papa Johanne Paulo wa pili pamoja na Papa Benedikt wa 16 wamepinga
mafundisho hayo yanayopigania haki za watu maskini.Kila mwaka, Müller husafiri kwenda Peru kumtembelea Gutierrez. Mwaka 2008 aliyatetea mafundisho ya imani ya ukombozi katika chuo kikuu cha kikatoliki, Peru. Chuo hicho kilimpa Müller shahada ya uzamifu ya heshima. Müller anatarajiwa kuanza kazi katika siku chache zijazo.
Miongoni mwa majukumu atakayokuwa nayo ni kushughulikia kesi za unyanyasaji wa kijinsia uliofanywa na watumishi wa kanisa.
No comments:
Post a Comment