Saturday, July 7, 2012

Madaktari wakubali yaishe hospiali za serikali


Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uuguzi MOI, Bernadina Rambau
Hali ya utoaji wa huduma katika hospitali mbalimbali hapa nchini zimeanza kurejea baada ya madaktari kusitisha mgomo wao na kurejea kazini.

Katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), imeongezeka baada ya uongozi wa taasisi hiyo juzi kuwatangazia wananchi kuwa huduma zimerejea.



Akizungumza na NIPASHE lililofika katika taasisi hiyo na kushuhudia idadi kubwa ya wagonjwa eneo la mapokezi, Kaimu Mkurugenzi wa  Idara ya Uuguzi MOI, Bernadina Rambau, alisema kuwa  jana idadi ya wagonjwa iliongezeka baada ya kutolewa taarifa ya kurejea kwa huduma.

Kwa mujibu wa Rambau, ongezeko hilo limesaababisha idadi ya Madaktri waliokuwepo kuzidiwa na kazi.

Aliyataja makundi hayo kuwa ni madaktari bingwa (specialists) na wale walioajiriwa (registrars) na kuongeza kwamba madaktari wa mafunzo kwa vitendo (interns) waliogoma na kuambiwa kwenda kuonana na uongozi wa Wizara ya Afya leo (Ijumaa), walikuwa ni wachapakazi na kwa jinsi hiyo kupunguza mzigo wa kazi.

“Madaktari wamekuwa wakipita wodini kuangalia na kuwahudumia wagonjwa waliolazwa….leo (jana) idadi ya wagonjwa imeongezeka kutokana na tangazo la kurejea kwa huduma,” alisema Rambau na kuongeza:

“Overworking ipo (kuzidiwa na kazi), kwasababu  madaktari  waliopo ni specialists (madaktari bingwa) na registrars (waliojiriwa). Pia hao registrars wamegawanyika, leo (jana) wengine wapo kwenye mitihani…na kutokuwepo kwa wale interns walioambiwa waende wizarani  ambao kwa kweli ni wachapakazi haswa,” alifafanua Kaimu Mkurugenzi huyo.

Pia NIPASHE lilipata fursa ya kuzungumza na Faki Mmadi, mkazi wa kisiwani Mafia, aliyefika jana MOI kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa wa maendeleo ya mguu wake wa kushoto baada ya kuvunjika na kuwekewa vvuma ambapo alikiri kuhudumiwa vizuri na madaktari mara baada ya kufika hospitalini hapo.

“Nilikuja kuchunguza maendeleo ya mguu wangu ambao ulifanyiwa upasuaji na kuwekewa vyuma baada ya kuvunjika..lakini baada ya  kufika hapa nimehudumiwa vizuri na sasa nasubiri tu usafiri niondoke,” alisema Faki Mmadi.

Kwa upande wake Afisa  Uhusiano Mwandamizi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Aminiel Aligaesha, akizungumza na NIPASHE ofisini kwake jana, alisema kuwa madaktari wanaendelea kuwahudumia wagonjwa waliolazwa wodini kama kawaida.

Aliongeza kuwa idadi ya wagonjwa waliokuja  hospitalini hapo si kubwa ambapo alitoa wito kwa wananchi kupeleka wagonjwa wao kwa madai ya kwamba huduma hakuna mgomo wowote na madaktari  wanatoa huduma.

Hata hivyo NIPASHE lilishuhudia lenyewe katika hospitali hizo ambapo madaktari walikuwa na pilika nyingi ili  kuwahudumia wagonjwa  huku baadhi ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wakisukumwa kwenye vitanda vyao na wauguzi kupelekwa wodini.

Katika za Temeke  na Amana jijini Dar es Salaam zimeendelea kuimarika baada ya idadi ya wagonjwa kuongezeka baada ya madaktari kurejea kazini.

NIPASHE  jana ilitembelea katika hospitali hizo na kujionea huduma zikiwa zinaendelea kama kawaida huku bado kukiwa na idadi ndogo ya wagonjwa wanaohudhuria hospitali hizo.

Wakizungumza na NIPASHE baadhi ya wagonjwa katika hospitali hizo walisema wanapatiwa huduma kama kawaida na hakuna tatizo lolote la madaktari.

“Ninashukuru sana tangu nilipofika hapa jana nimepokelewa vizuri na kupatiwa huduma na madaktari wananiangalia mara kwa mara,” alisema Maria Khamisi ambaye amelazwa Amana

Katibu wa Afya katika hospitali ya  Amana, Tunu Mwachally, alisema japokuwa baadhi ya madaktari hawajarejea kazini lakini asilimia kubwa wamesharejea na wanafanya kazi kama kawaida.

Katika hospitali za Mbeya na Dodoma hali ya utoaji wa huduma nazo imeripotiwa kwamba zimerejea kama kawaida.

Habari hii imeandikwa na Gwamaka Alipii, Isaya Kimbili na Elizaberty Zaya


 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment