Wednesday, July 4, 2012

Uharibifu wa maeneo ya kitamaduni waendelea Timbuktu

Waasi wa kiislamu nchini Mali wameuvunja mlango wa Karne ya 15 wa msikiti mmoja mjini Tumbuktu, huku washirika wao wa kundi la kigaidi la Al Qaeda wakitega mabomu ya ardhini mjini Gao, kaskazini mwa nchi hiyo. 

Katika mji wa Timbuktu waasi wa Ansar Dine, ambao wanaaminika kuwa washirika wakuu wa kundi la kigaidi la Al Qaeda, wanaendelea kuyaharibu maeneo ya kitamaduni mjini humo, hatua iliolaaniwa vikali na jamii ya kimataifa.

Baadhi ya wakaazi walitokwa na machozi pale waasi walipouvunja mlango wa msikiti wa Sidi Yahya uliofungwa kwa miongo mingi kwa kuamini kwamba pindi utakapofunguliwa, huenda kukawa na msiba au bahati mbaya katika eneo hilo.

 
Waasi hao wanasema kwamba wanaharibu maeneo hayo kwa kuwa yanakwenda kinyume Uislamu na kuwa kuwatukuza masheke wa kale ni kinyume na mafundisho ya dini hiyo.

Mjini Gao Taarifa zinasema, wanamgambo wa kundi la Al Qaeda wametega mabomu ya ardhini mjini humo, huku msemaji wa kundi la waasi wa Watuareg, Mossa Ag Attaher, akiwashtumu waasi hao kwa kuuteka nyara mji huo. Mabomu yametegwa ardhini ili kuzuia shambulio lolote kutoka kwa majeshi ya jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Africa Magharibi, ECOWAS, au hata mashambulio kutoka kwa wapiganaji wa Watuareg.

Wakaazi mjini Timbuktu wakijaribu kuyahama maeneo hayo Wakaazi mjini Timbuktu wakijaribu kuyahama maeneo hayo
Hadi sasa waasi wa Tuareg wanadhibiti kwa pamoja eneo la Gao na waasi walio na itikadi kali za kiislamu.
Msemaji wa kundi la waasi wa Watuareg, MNLA, amesema kwa sasa wakaazi wengi mjini Timbuktu wanajaribu kuyahama maeneo hayo kwa kutumia mabasi na kuelekea mjini Bamako kwa hofu ya kutokea kwa ghasia zaidi, lakini waasi wa kiislamu wanawazuia kufanya hivyo. 

Katika Video iliopatikana na chombo cha habari cha AFP, inaonesha waasi waliovalia vitambaa kichwani wakisema kwa sauti Allahu Akbar, yaani Mwenyezi Mungu ni mkubwa, huku wakiendelea na uharibifu kwa makaburi ya masheke wa kale nchini humo kwa kutumia majembe.


Rais wa Cote d'Ivoire,  na pia mwenyekiti wa ECOWAS Alassane Ouattara Rais wa Cote d'Ivoire, na pia mwenyekiti wa ECOWAS Alassane Ouattara
Huku hayo yakiarifiwa, viongozi wa kiafrika watakutana mwishoni mwa wiki hii hii katika mji mkuu wa Burkina Faso, Ouagadougou, kuzungumzia mzozo wa Mali. Waziri wa mambo ya kigeni wa Burkina Faso, Djibrill Bassole, amesema viongozi hao watakutana siku ya jumamosi na wanasiasa wakuu wa Mali kuzungumzia pia namna ya kusonga mbele na kuwa na serikali ya muungano nchini humo. 

Viongozi wa nchi zitakazokutana kwa mazungumzo hayo ni pamoja na mwenyeji, Burkina Faso, Benin, Liberia, Niger, Nigeria, Togo na rais wa Cote d'Ivoire, Alassane Ouattara, ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Africa Magharibi, ECOWAS.

No comments:

Post a Comment