Katika mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari, Riyad Hijab
amesema kwamba, baada ya miezi 17 ya maandamano dhidi ya serikali,
utawala wa Assad umedhoofika sana. Katika mkutano huo uliofanyika mjini
Amman, Jordan, Hijab amesema kwa uzoefu wake, utawala huo unaporomoka
kimaadili, kivifaa na kiuchumi.
Ingawa ni vigumu kuthibitisha idadi ya maeneo ambayo waasi
wanayadhibiti, lakini ushahidi wa kimazingira unaonesha kuwa Assad
amepoteza baadhi ya maeneo ya mpakani, kaskazini na mashariki mwa nchi
hiyo, na mapigano yamedhoofisha sana nguvu zake katika miji mikubwa kama
vile Aleppo na Homs.
Hijab amewasifu waasi kwamba mapinduzi yao yamekuwa "kigezo cha juhudi
na kujitoa muhanga kwa ajili ya uhuru na heshima." Ingawa Hijab hakuwa
sehemu ya watu muhimu wanaomzunguka Assad, lakini akiwa waziri mkuu na
afisa wa ngazi za juu, kuondoka kwake kumekuwa pigo kubwa kwa utawala
huo na kuongeza morali kwa upande wa waasi.
Hata hivyo, kwenye medani ya kivita ukweli bado haujabadilika. Bado
wanajeshi wa serikali wanashambulia kwa kutumia ndege na mizinga. Hijab
aliwataka maafisa wa jeshi kujiunga na upinzani na pia makundi mbali
mbali ya waasi kuungana dhidi ya utawala wa Assad ambao ameuita "adui wa
Mungu."
No comments:
Post a Comment