Maelfu ya raia nchini Pakistan wanatarajiwa kuingia mitaani
baada ya swala ya Ijumaa kuandamana, kupinga filamu inayoukashifu
Uislamu, na vikaragosi vya Mtume Muhammad vilivyochapishwa na jarida
moja nchini Ufaransa.
Serikali ya Marekani yajitenga na filamu hiyo
Filamu hiyo imesababisha maandamano katika mataifa yasiyopungua 20 tangu vipande vyake viwekwe kwenye mtandao wa Youtube, na zaidi ya watu 30 wameuawa katika vurugu zinazohusiana nayo. Wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani imewaonya raia wake dhidi ya kusafiri kwenda Pakistan, na utawala mjini Washington umelipia matangazo katika vituo vya Televisheni nchini Pakistan katika jaribio la kujitenga na filamu hiyo.
"Tangu kuanzishwa kwetu, Marekani imekuwa nchi inayoheshimu dini zote. Tunapinga juhudi zozote zinazolenga kushusha hadhi ya dini za watu wengine," anasemarais Barack Obama katika sehemu ya tangazo hilo.
Pia, waziri wa mambo ya kigeni, Hillary Clinton anaokena akisistiza kwamba serikali ya Marekani haikuhusika kwa namna yoyote ile na video hii na kwamba serikali hiyo inapinga kwa nguvu zote, yaliyomo kwenye filamu hiyo pamoja na ujumbe wake.
Je,wapakistan wataulewa ujumbe huo?
Ingawa ujumbe huo wa rais Obama na waziri Clinton siyo mpya, wizara ya mambo ya kigeni inasema haukuwafikia vizuri Wapakistani na ndiyo maana Marekani imeamua kutumia kiasi cha dola elfu 70 kuulipia. Ubalozi wa Marekani mjini Islamabad pia umetuma maafisa wake mitaani wakifanyiwa mahojiano na vyombo vya habari kujaribu kubadilisha mtizamo wa raia wa Pakistan dhidi ya Marekani kuhusiana na filamu hiyo.
Lakini Mhariri wa jarida la Foreign Policy la Marekani, anasema ujumbe huo hautokuwa na athari kwa raia hao ikizingatiwa kuwa wamekuwa na historia ya kuichukia Marekani. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni Victoria Nuland, alisema waliamua kulipia ujumbe huo kwa kuwa serikali ya Pakistan iliwashauri wafanyehivyo.
Ufaransa nayo katika mtihani
Ufaransa nayo imejikuta katika wakati mgumu kufuatia kuchapishwa kwa michoro ya katuni zinazomuonyesha mtume Muhammad na jarida la Charlie Hebdo, zikiwemo mbili zinazomuonyesha akiwa uchi. Serikali ya Ufaransa ilipinga maandamano yaliyopangwa siku ya Jumamosi mbele ya msikiti mkuu wa Paris na imetangaza kufunga balozi na shule zake katika mataifa 20 leo.
Viongozi wa jumuiya ya kiislamu nchini Ufaransa, ambayo ndiyo kubwa zaidi barani Ulaya wamesema miito ya kuwepo na utulivu itasomwa misikitini nchini kote, lakini pia wamelaani kitendo cha jarida hilo kuchapisha michoro hiyo. Mhariri wa jarida hilo, Stephane Charbonnier, aliwadhihaki waliochukizwa na vikaragosi hivyo kwa kuwaita 'vichekesho', huku akiikosoa serikali kwa alichokiita kuwaendekeza na kuungana nao kulikosoa jarida hilo.
No comments:
Post a Comment