Watu 20 wameuawa leo nchini Nigeria baada ya watu wenye silaha kuwafyatulia risasi wafuasi wa dini ya Kiislamu walipokuwa wakitoka kwenye msikiti mmoja kaskazini mwa nchi hiyo.
Kiongozi wa jadi na diwani wa Birnin Gwari, Abdullahi Muhammad, amesema kuwa shambulio hilo limetokea katika kijiji cha Dogo Dawa katika Jimbo la Kaduna.
Hakuna taarifa za haraka zenye kuhusisha kundi au mtu na shambulio hilo. Kama ilivyo kwa maeneo mengi ya Kaskazini mwa Nigeria, Jimbo la Kaduna linakabiliwa na mashambulizi yanayofanywa na kundi lenye itikadi kali za Kiislamu la Boko Haram.
Kwa kawaida kundi hilo hushambulia vikosi vya usalama, maafisa wa serikali au Wakristo, lakini siku za nyuma lilikuwa likishambulia misikiti na Waislamu wasiopenda kufuata sheria zao zenye itikadi kali. Hata hivyo, Abdullahi anasema kuna uwezekano mkubwa shambulio hilo kufanywa na kundi la uhalifu katika mitaa ya eneo hilo.
No comments:
Post a Comment